HEADER AD

HEADER AD

BARAZA LA MADIWANI MASWA LAPITISHA BAJETI BILIONI 52.4

Na Samwel Mwanga, Maswa

BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu limepitisha mapendekezo ya mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 kiasi cha Tsh. Bilioni 52.4.

Afisa Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Julius John akiwasilisha mapendekezo hayo katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Februari  24 mwaka huu amesema kuwa wanakadiria kukusanya na kutumia jumla ya Sh 52,495,521,000 ambapo kati ya hizo Sh 14,515,182,767 ni fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

         Afisa Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Julius John

Amesema kuwa bajeti hiyo imekuwa na ongezeko la Sh 6,541,526,000 sawa na asilimia 14 ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2023/2024 ya kiasi cha Tsh. 45,953,995,000

“Ongezeko hili mheshimiwa Mwenyekiti linatokana na kuongezeka kwa fedha za mishahara ya ajira mpya na upandishaji wa vyeo kwa watumishi 107,”amesema.

Amesema mapendekezo ya mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa mwaka 2024/2025 umezingatia Dira ya Taifa ya maendeleo (2025) sheria ya bajeti Na.11 ya mwaka 2015, mwongozo wa uandaaji wa mpango na bajeti wa mwaka 2024/2025 uliotolewa na wizara ya fedha na Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi(CCM) ya mwaka 2020/2025.

Akichangia mapendekezo hayo Diwani wa Kata ya Busilili, Nangale Ngussa amesema katika shule ya msingi Bushitala yenye wanafunzi zaidi ya 1000 lakini ina matundu ya saba tu ya choo.

       Baadhi ya madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani

Amesema hali hiyo ina hatarisha afya za wanafunzi hao wanapokuwepo shuleni hivyo ameomba shule hiyo iongezewe matundu ya vyoo kutoka 12 yaliyowekwa kwenye mapendekezo ya bajeti hiyo hadi matundu ya vyoo  24.

Naye Diwani wa Viti Maalum, Witnes Philipo amesema kuwa ni vizuri Mamlaka ya Mji mdogo wa Maswa iwekewe bajeti ya kutosha ili iweze kufanya kazi zake na kuondoa migogoro inayojitokeza ya mara kwa mara kati ya Mamlaka na Halmashauri ya wilaya.

      Naye Diwani wa Viti Maalum, Witnes Philipo

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Paul Maige amewasisitiza madiwani kuhakikisha wanawasimamia  watendaji katika kata zao juu ya ukusanyaji wa mapato na kuahidi kumpa ushirikiano wa karibu kudhibiti utoroshaji wa mapato.

“Madiwani wasimamieni hao watendaji wa kata waliopewa dhamana ya kukusanya mapato kwani tukikusanya mapato yetu kwa wingi tutafikia malengo ambayo tumejiwekea katika bajeti yetu hii, hasa katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi,’amesema.

      Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Paul Maige

Aidha amesema kuwa katika mapendekezo hayo  Kamati ya Mipango na fedha ya Halmashauri ya wilaya ya Maswa ilifanya maboresho ambayo ni pamoja na kuweka msawazo wa vyoo katika shule za msingi na sekondari ambazo zina uhitaji mkubwa wa vyoo kwa wilaya hiyo.

Amesema siyo matundu 35  tu kama bajeti ya awali ilivyopendekeza ambapo sasa matundu 228 ya vyoo yatajengwa katika Kata 19 ambazo zina changamoto zaidi.


No comments