WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUBAINI TATIZO LA MIGONGANO YA BINADAMU, WANYAMAPORI
Na Andrew Chale, Bagamoyo
WAANDISHI wa habari wametakiwa kutumia mbinu sahihi za kubaini vyanzo vya migongano baina ya binadamu na wanyamapori kwa kuviibua ili kusaidia kupunguza tatizo hilo.
Hayo yamebainishwa na Anna Kimambo kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), ambaye ni Mshauri wa mradi wa kupunguza migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania kwa Ukanda wa Ruvuma.
Mradi huo unatekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii (MNRT), wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili, Februari 2024 ya Waandishi wa Habari hivi karibuni yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), Bagamoyo, mkoani Pwani.
Amewataka waandishi kuzingatia mafunzo waliyopatiwa kutoka kwa wawezeshaji kwani yanawapa taswira ya kile wanachoenda kuripoti hasa suala nyeti la migongano baina ya binadamu na wanyama hasa katika Wilaya za Liwale, Tunduru na Namtumbo.
‘’Niwashukuru kwa kuweza kupata mafunzo haya kwa siku mbili na mtaenda kufanyia kazi kupitia kile mlichojifunza kutoka kwa watoa mada mbalimbali, sasa muingie ‘field’ ilikubaini tatizo ambalo linatakiwa kutatuliwa.
"Sisi kama waandishi wa habari tuna sehemu yetu ya kutatua migongano hii kupitia kalamu zetu kwa kuandika makala na stori zetu zenye kuibua tatizo kwa kuripoti habari zaidi lakini pia tukitumia lugha sahihi kwa namna ya tulivyofundishwa.’’ amesema Anna.
Aidha amesema wanahabari wanatakiwa kuchimba ndani zaidi katika kuibua taarifa hili wananchi waelewe huku akiwataka wapiti taarifa za mipango na utekelezaji ya Wizara kuhusu mpango wa kuzuia migongano hiyo.
‘’Sisi kama wanahabari tunatakiwa kuliandikia lile tatizo pale kwamba kwa nini limekuwepo, nani anasababisha, tufanye nini ilituweze kuliondoa hilo tatizo. Nafikiri wananchi hapo ndio wataelewa na tunategemea sana, mabadiliko haya ya waandishi, yatasaidia sana taasisi za Siserikali kama TAWA, TANAPA, Ngorongoro na zingine.
"Sisi kama wadau wa uhifadhi iwe kama sehemu ya kutoa elimu, lakini pia na sisi waandishi wa habari tuna sehemu yetu kupitia kalamu zetu kwa kuandika habari, makala zetu" amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo amesema kuwa mradi wameanza mafunzo hayo katika hatua mbalimbali ikiwemo kukutana na waandishi Dar es Salaam, na Bagamoyo ambapo baadae waandishi kwenye vituo vyao eneo la mradi na kisha watapita kwenye vijiji 30 vya wilaya tatu.
‘’Hizi kazi hazikujengi wewe pekee yako, zinaijenga taasisi JET, zinaijenga GIZ, lakini pia zinaijenga Tanzania yetu. Naamini baada ya mafunzo haya tutarajie kazi nzuri na zenye kujenga.’’ amesema Chikomo.
Awali wawezeshaji wataalamu wametoa mada mbalimbali akiwemo, Dk. Danstan Kamanzi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Afisa Uhifadhi masuala ya wanyama wakolofi na waaribifu kutoka TAWA, Isaack Chamba, Edward Mhina kutoka TGNP.
Mafunzo hayo pia yamehusisha maafisa habari kutoka Halmashauri za Liwale, Namtumbo na Tunduru pamoja na waandishi wa habari zaidi ya 20 kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Post a Comment