HEADER AD

HEADER AD

DC KAMINYOGE: UZENI SUKARI KWA BEI ELEKEZI

Na Samwel Mwanga, Maswa

WAFANYABIASHARA wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wametahadharishwa kuepuka kuuza bidhaa ya sukari kinyume na bei elekezi ya serikali kwani kufanya hivyo ni kosa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ametoa tahadhari hiyo Februari 28 mwaka huu wakati wa mkutano wake na wafanyabiashara wa soko kuu la mjini Maswa ikiwa ni mwendelezo wa mikutano yake ya kukutana na makundi mbalimbali pamoja na wananchi ili kusikiliza kero zao.

     Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge akizungumza na Wafanyabiashara katika soko kuu mjini Maswa kwa ajili ya kusikiliza kero zao.

Amesema kuwa  Serikali imetoa bei elekezi ya kuuza bidhaa ya sukari nchini kufuatia kuwepo kwa mfumuko wa bidhaa hiyo ambapo kwa Kanda ya Ziwa inayojumuisha Mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara bei ya rejareja ya sukari kwa kilo moja ni Tsh 2,800 hadi Tsh 3,000 huku bei ya jumla ni kati ya Tsh 2,650 hadi 2,80

Amesema kuwa uongozi wa serikali ya wilaya hiyo ulifanya utafiti na kubaini sukari kwa kilo moja inazwa Tsh. 4,000 katika mji wa Maswa lakini wafanyabiashara wa bidhaa hiyo kwa bei ya jumla walio wengi hawana risti za kuonyesha mahali ambapo wananunua bidhaa hiyo.

“Serikali imekwisha kutoa bei elekezi ya bidhaa hiyo ya sukari hivyo ni vizuri Wafanyabiashara wakawa wazalendo kwa kufuata bei hiyo ili kuepuka kuwanyonya watumiaji ambao ni wananchi wa kawaida”amesema.

Pia amesema kuwa wakati wanapita katika maduka ya bidhaa ya jumlajumla wamegundua ya kuwa wafanyabiashara walio wengi hawana risti za bidhaa zao mahali wanaponunulia jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria.

        Baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria mkutano wa kusikiliza kero ulioitishwa na Mkuu wa wilaya ya Maswa,aswege Kaminyoge kwenye soko kuu mjini Maswa.

“Mimi jana na kamati ya usalama ya wilaya  na Mkurugenzi tumepita kwenye maduka kati ya wafanyabiashara wa  maduka ya Jumla  Jumla kati ya saba tuliwatembelea ni wawili tu tulifanikiwa kupata risti zao walikonunua na zinapotueleza walinunua mfuko wa Kilo 25 ya sukari kwa shilingi kadhaa wengine hatukufanikiwa,usipokuwa na risti ya uliponunulia huko tunafikiri ulinunua kwa bei ndogo ili uweze kuwauzuia wafanyabiashara ya rejareja kwa bei kubwa,”

“Mnataka sasa mnilazimishe mimi Mkuu wa wilaya nimwagize Mkuu wa polisi wa wilaya na vyombo vingine vya usalama vifanye kazi ya kukagua bidhaa zote zinazoingia katika mji wa Maswa tuzikague kwa  sababu kutokuwa na risti ya bidhaa uliyonunulia iwe kubwa au ndogo ni kosa,sisi tunapotaka kuwasaidia tunakwama kwa vielelezo hivyo niwatake unaponunua bidhaa uwe na risti,”amesema.

Amesema sasa imefika wakati kwa wafanyabiashara kuacha kufanya kazi kwa mazoea hasa wa maduka kwa kushindwa kutoa risti kwa bidhaa wanazouza kwa wateja wao kwani kwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi.

Naye Afisa Biashara wa halmashauri ya wilaya hiyo,Maria Ndohelo  amesema kuwa sasa wilaya hiyo itaanza kuwasajili wafanyabiashara wadodo wadogo ambao watapatiwa vitambulisho ili waweze kufanya biashara zao kwa uhuru na gharama za kila kitambulisho ni Sh 20,000/-ambacho kwa muda wa miaka mitatu.

     Afisa Biashara wa wilaya ya Maswa,Maria Ndohelo akielezea utaratibu wa kuwasajili wajasiliamali na kisha kupatiwa vitambusho kwa gharama ya sh 20,000.

“Hivi karibuni tutaanza utaratibu wa kuwasajili wafanyabiashara wadogowadogo maarufu kwa jina la wajasiliamali kwa kipindi hiki tutatumia vitambulisho vya mpiga kura ili kupata taarifa sahihi za mfanyabiashara huyo na tutahakikisha kuwa kweli ni mjasiliamali kwa kuona sehemu yake ya biashara na gharama ya kitambulisho itakuwa ni Sh 20,000 na kitadumu kwa miaka mitatu,”amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo,Maisha Mtipa amesema kuwa kwa sasa wanaandaa mkutano mkubwa wa kukutana na wafanyabiashara wote wa wilaya ya Maswa ili waweze kukutana kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya pande hizo mbili pamoja na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili na kuweza kuzitatua.

      Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa akizungumza na wafanyabiashara katika soko kuu mjini Maswa

“Kwa sasa tutaandaa mkutano wa kukutana na wafanyabiashara wote wa wilaya ya Maswa ili tuweze kukutana kwa lengo kubwa la kuimarisha uhusiano kati yetu na wao na pia kuwasikiliza changamoto zao na kuzitatua na tunahitaji wafanyabiashara wafanye kazi zao kwa raha na utulivu,”amesema.

Mfanyabiashara Leticia Mayala pamoja na kumpongeza Mkuu wa wilaya ya Maswa kusikiliza kero za wananchi kwa makundi mbalimbali ameomba serikali iweze kuwasaidia wazee ambao kwa sasa hawajiwezi hata kujihudumia katika maisha yao ya kila siku.

        Mfanyabiashara,Leticia Mayala akitoa kero yake mbele ya Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge

No comments