HEADER AD

HEADER AD

WANAWAKE CCT WAWAKUMBUKA WAFUNGWA, MAHABUSU GEREZA LA MASWA

Na Samwel Mwanga, Maswa 

WANAWAKE wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) wilaya ya Maswa mkoani Simiyu kupitia Idara ya wakinamama wametoa misaada mbalimbali kwa Wafungwa na Mahabusu waliopo katika Gereza la Maswa.

Akizungumza kwa niaba ya Wanawake hao Machi Mosi mwaka huu katika viunga vya gereza hilo, Mwenyekiti wa CCT, Idara ya Wakinama, Edith Masasila amesema kuwa wamefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya siku ya maombi ya Wanawake Duniani ambayo yamefikia kilele leo.

     Mwenyekiti wa CCT wilaya ya Maswa, Idara ya Wakinamama,Edith Masasila (kulia) akimkabidhi mchele kwa mkuu wa gereza la Maswa, ASP,Omari Mbwambo (kushoto) kwa ajili ya wafungwa na mahabusu wa gereza hilo.

Amesema kuwa waliona ni vyema waweze kufika katika gereza hilo ili kuweza kuwasalimia wafungwa na mahabusu walioko ndani gereza hilo ambao ni wanawake na Wanaume  kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali ili nao waweze kuona ya kuwa japo wako ndani ya gereza lakini kuna watu wanawakumbuka.

“Asubuhi ya leo Mungu ametupa kibali kufika mahali hapa katika gereza la Maswa ili tuweze kuwasalimia hawa ndugu zetu walioko hapa ili tuweze kuwapatia vitu mbalimbali ili nao waweze kufurahi na kuona ya kuwa kuna watu walioko nje wanawakumbuka,”amesema.

Amesema kuwa misaada ya vitu mbalimbali walivyotoa imetokana na michango iliyotolewa na wanawake wa madhehebu ya Kikristo katika wilaya ya Maswa wanaounda Jumuiya hiyo.



Amevitaja vitu ambavyo wamevitoa ni pamoja na Nyama Kilo 20, Mchele Kilo 100, Sabuni Katoni 4, Mafuta ya kupaka Katoni 9 na Taulo za kike vyote vikiwa na thamani ya Sh 600,000.

Mkuu wa gereza la Maswa, Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASO) Omari Mbwambo amewashukuru Wanawake hao waliowasilisha misaada hiyo kwa niaba ya wenzao huku akisisitiza ya kuwa itatumika na kuwasaidia walengwa kama ilivyokusudiwa.

Mwenyekiti wa CCT wilaya ya Maswa,Idara ya Wakinamama, Edith Masasila (kulia) akimkabidhi boksi la Sabuni , Mkuu wa gereza la Maswa, ASP,Omari Mbwambo (kushoto) kwa ajili ya wafungwa na mahabusu wa gereza hilo.

Amesema kuwa gerezani ni mahali salama kwani wanaokuja humo hasa wafungwa wanakuja wakiwa waovu kutokana na makosa mbalimbali waliyoyatenda katika jamii lakini wao wanawarekebisha.

“Kwanza niwashukuru kwa ninyi kufika katika eneo hili la gereza kwani ni watu wachache sana wanaopata mawazo twende Magereza.


" Nishukuru kwa misaada hii yote iliyoletwa kwa ajili ya wafungwa na mahabusu yote itafika ila niwaeleze kwa ufupi magereza ni sehemu salama kwani wanakuja wakiwa waovu lakini wakitoka wakiwa wazima tunawarekebisha,”amesema.

Naye Mwenyekiti wa CCT Wilaya ya Maswa, Mchungaji Jacobo Ocholla ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa La Afrika Inland Church(AIC)Shanwa amewapongeza wakinamama hao kwa kuhitimisha siku ya maombi hayo kwa malengo mazuri ya kuleta huduma katika gereza la Maswa.

      Viongozi wa Jumuiya na Kikristo Tanzania (CCT) wilaya ya Maswa wakiwa na Viongozi wa gereza la Maswa walipofika na wanawake wa jumuiya hiyo kutoa misaada kwa wafungwa na Mahabusu wa gereza hilo.

“Leo ni siku ya maombi ya wanawake duniani na leo tarehe moja ni siku ya hitimisho na mimi nitumie nafasi hii kuwapongeza wakinamama wote kwa kuwa na hitimisho zuri na kwa malengo mazuri ya kuleta huduma kwa wenzetu waliko katika gereza la Maswa.

"Mungu awabariki sana na sadaka yenu Mungu aikumbuke na muendelee kufanya hivyo kwa utukufu wa Bwana,”amesema.

       Wanawake wa CCT wilaya ya Maswa wakiwa na bango wakati wa maandamano ya kuhitimisha siku ya Maombi ya Wanawake duniani.

     Sehemu ya Wanawake wa CCT wilaya ya Maswa waliofika katika Gereza la Maswa kutoa misaada kwa Wafungwa na Mahabusu wa Gereza hilo.

No comments