HEADER AD

HEADER AD

DCC YARIDHIA KUUNDWA KWA HALMASHAURI MBILI WILAYANI MASWA


>> Yashauri mchakato wa kuvunjwa mamlaka ya mji mdogo wa Maswa uanze upya

>>Yasema sheria haikufuatwa azimio uvunjwaji mamlaka ya mji mdogo

Na Samwel Mwanga, Maswa

KAMATI ya Ushauri ya wilaya ya Maswa(DCC) katika mkoa wa Simiyu imeridhia kuundwa kwa halmashauri mbili katika wilaya hiyo ili kuweza kusogeza huduma karibu na wananchi.

Pia kamati hiyo imeshauri kusitishwa kwa mchakato wa kuivunja Mamlaka ya Mji mdogo wa Maswa kama ilivyoazimiwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kutokana na kutofuatwa kwa sheria na hivyo uanze upya kwani haukuwashirikisha wananchi.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ambaye ndiye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo amesema hayo Februari 22 mwaka huu katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu huyo wa wilaya.

     MKUU wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya wilaya hiyo katika Ukumbi wa Ofisi ya mkuu huyo wa wilaya.

Amesema kuwa azimio la kuanzishwa kwa halmashauri hizo ambalo lilipitishwa katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Februari 16 mwaka huu analiunga mkono na kuupatia Baraka ili uweze kuendelea kwa vikao vingine vya juu ila Azimio la kuivunja Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa ni lazima uanze upya kwa kufuata utaratibu wa kisheria.

“Kama mwakilishi wa Rais katika wilaya ya Maswa niwaombe mchakato huu urudi ukaanze upya kwa kufuata sheria lakini kwa ishu ya mapendekezo ya kuanzisha halmashauri mimi kama Mkuu wenu wa wilaya una baraka zote endeleeni.

" Lakini kwa hili la kuvunja mamlaka ya mji mdogo nadhani halijapata mashiko mazuri kwa dhana ile ya serikali za mitaa vyombo vya wananchi sharti kuanzishwa kwake na kuvunjwa kwake utokane na wananchi mimi ushauri wangu na msimamo wangu ndiyo huo,” amesema.

Amesema kuwa tangu azimio hilo lipitishwe la kuivunja mamlaka hiyo limekuwa na athari kubwa licha ya kuelezwa kuwa imeshindwa kujiendesha lakini halmashauri ya wilaya imeshindwa kuitengenezea mazingira mazuri ili iweze kufikia hadhi ya Halmashauri ya Mji.

       Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(mwenye miwani) akiongoza kikao cha Kamati ya Ushauri ya wilaya hiyo.

Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo amesema kuwa ni vizuri kuungana kwa pamoja iwapo mchakato wa kuunda halmashauri mbili hauzuii kuwepo kwa Mamlaka hiyo kisheria ni vizuri uendelee bila kuivunja kwani ni hatua ya maendeleo.

“Tuungane pamoja kama mchakato wa kuanzisha kwa halmashauri mbili hauzuiliwi na uwepo wa Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa basi mchakato wa halmashauri mbili uendelee bila kuivunja Mamlaka isipokuwa kama kuna mkanganyiko wa kisheria unaozuia mchakato kuendelea tuone namna ya kufanya ili tuweze kutekeleza.

       Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki,Stanslaus Nyongo (kushoto) na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Maswa,Mwalimu Onesmo Makota (kulia) wakiwa katika kikao cha kamati ya Ushauri ya wilaya hiyo.

" Lakini uanzishwaji wa halmashauri mbili ni jambo la msingi na uwepo wa mamlaka ya mji mdogo ni jambo la maendeleo iendelee kuwepo na kama kuna mapungufu basi yarekebishwe ili tuendelee na mchakato wa kupatikana kwa  halmashauri ya mji wa Maswa,”amesema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Maswa, Mwalimu Onesmo Makota amesema kuwa mchakato wa kuivunja mamlaka hiyo usimame na mchakato wa kuanzisha Halmashauri hizo uendelee na mamlaka ya mji mdogo wa Maswa iimarishwe ili iweze kufikia malengo ya kuwa Halmashauri ya Mji.

“Kama kuna mchakato wa kuunda halmashauri mbili uendelee lakini tusiivunje mamlaka ya mji mdogo wa Maswa na kama kuna uwezekano tuiwezeshe ili iweze kufikia malengo ya hadhi ya halmashauri ya Mji,”amesema.

Awali  Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Mwita Mwita akiwasilisha mapendekezo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo amesema kuwa maazimio hayo yalipitishwa na kikao cha baraza la madiwani wa wilaya hiyo.

Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Mwita Mwita akiwasilisha taarifa ya kuivunja Mamlaka ya Mji Mdogo wa  Maswa na kuanzishwa kwa Halmashauri mbili katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya wilaya hiyo.

Amesema sababu zikielezwa za kuitaka kuivunja Mamlaka hiyo ni pamoja na kushindwa kujipanua na kufikia ukubwa wa Kata 12 zinazohitajika ili Mamlaka ipewe hadhi ya Halmashauri ya Mji.

Pia imeshindwa kubuni na kaunzisha na kusimamia vyanzo vya mapato hivyo kuendelea kuwa mzigo kwa Halmashauri ya wilaya hiyo pamoja na kupewa vyanzo vyake vya mapatokatika kugharamia shughuli za kila siku za mamlaka.

Akizungumzia kuanzishwa kwa halmashauri hizo amesema kuwa wanapendekeza kuanzishwa kwa halmashauri mpya katika jimbo la Uchaguzi la Maswa Mashariki itakayoitwa Halmashauri ya Maswa Mashariki na nyingine itaitwa Halmashauri ya Maswa Magharibi. 

       Baadhi ya wajumbe wa kamati ya Ushauri ya wilaya ya Maswa wakiwa katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo mjini Maswa

“Halmashauri ya Maswa Mashariki itaundwa na Kata za Nyalikungu, Binza, Bugarama,Shanwa,Sola,Ng’wig’wa ,Nguligili,Ipililo,Senani,Mwamanenge na Sukuma. 

Kata nyingine ni pamoja na Mpindo, Dakama, Lalago ,Budekwa, Sangamwalugesha, Mbaragane na Mwabaraturu.

“Halmashauri ya Maswa Magharibi itaundwa na Kata za Kadoto, Shishiyu, Nyabubinza, Mwang’honoli, Kulimi, Malampaka, Badi, Mwabayanda, Mataba, Jija, Seng’wa, Masela, Isanga, Zanzui, Mwamashimba, Buchambi na Busangi,” amesema " Mwita.

No comments