HEADER AD

HEADER AD

MWENYEKITI WA KITONGOJI NYAMONGO ANAYEDAIWA KUMSHAMBULIA, KUMJERUHI MHUDUMU WA BAR KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Na Dinna Maningo, Tarime

JESHI la Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya linamshikilia Silasi Nguka Nyamhanga (46) ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Majengo mapya katika kijiji cha Nyangoto Kata ya Matongo-Nyamongo, kwa tuhuma za kumjeruhi na kumshambulia mhudumu wa Bar ya Chimbo Pub, Jenipher Shaban (31) mkazi wa Nyamongo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya Mark Njera, amesema kuwa tukio hilo liliripotiwa Febuari 17, 2024 ambapo mtuhumiwa alimpiga kwa rungu, ngumi na mateke nakupelekea kung'oka meno mawili na jino moja  kupasuka.

        Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya, Mark Njera

Amesema katika mitandao ya kijamii ilionekana video ikisambaa ikimuonesha  Mwanamke huyo akiuguza majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake, huku msimulizi katika video hiyo akieleza kuwa mwanamke huyo alifanyiwa ukatili kwa kupigwa kwa marungu na mtu aliyefahamika kuwa Mwenyekiti wa Kitongoji.

Kamanda Njera amesema chanzo cha tukio ni mtuhumiwa kudaiwa pesa kiasi cha Tsh. 24, 000 alizokunywa pombe katika bar hiyo iliyopo kitongoji cha Nyagoto.

Amesema mtuhumiwa alimhadaa mwanamke huyo na kumpeleka nyumbani kwake ili akamlipe pesa hiyo badala yake alimfungia ndani ya uzio na kuanza kumshambulia 

Kamanda huyo amesema katika nyumba hiyo alikuwepo mke wake na kijana wake wa kiume ambaye ndiye aliyefungua mlango wa geti na mwanamke huyo kupata nafasi ya kujinasua katika shambulio hilo.

"Mlalamikaji alipatiwa PF. 3 kwa ajili ya matibabu na hali yake inaendelea vizuri . Baada ya taarifa hiyo kupelekwa jeshi la Polisi lilichukua hatua ya haraka kumsaka mtuhumiwa na kumkamata.

" Upelelezi wa shauri umekamilika, Jalada limepelekwa kwa Wakili wa Serikali kwa ajili ya kuandaa mashtaka ili aweze kufikishwa mahakamani" amesema Kamanda Njera.

Ametoa wito kwa wananchi kuacha vitendo vya ukatili kwani vitendo hivyo vya kinyama vina athari kubwa kwa jamii na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watendaji wa vitendo vya ukatili.

No comments