KATA YA NYARERO YAPATA BILIONI TATU MIRADI YA MAENDELEO
Na Dinna Maningo, Tarime
DIWANI wa Kata ya Nyarero John Mhabasi ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuwezesha fedha zaidi ya Bilioni tatu ambazo zimetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.Aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa mkutano katika kata hiyo ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Mara, Julius Kambarage Masubo.
Diwani Mhabasi alisema katika uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zaidi ya Bilioni tatu zimepelekwa kwenye kata yake na miradi imejengwa zikiwemo, shule, mradi wa maji na Zahanati.
"Kata yangu imepata pesa nyingi, madarasa yamejengwa, watoto hawakai chini,tumepata mradi wa maji na tayari bomba zimelazwa chini, tulikuwa na changamoto ya mwalimu wa hisabati kwa sekondari lakini tumeshaletewa.
"Zahanati ya Soroneta imepata sh. milioni 10, Rozana tumepeleka milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa soko na milioni 40 zingine kwa ajili ya soko zinakuja, miradi mbalimbali imejengwa tunaipongeza serikali kwa kutoa fedha" alisema Diwani Mhabasi.
Mkazi wa Kijiji cha Soroneta Chacha Marwa alisema kuwa serikali imeboresha miundombinu ya shule, barabara na afya hivyo kwa sasa hawasumbuki kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya na elimu.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM mkoa wa Mara, Julius Kambarage Masubo aliwasisitiza wazazi kuwapeleka watoto shule ili wakapate elimu.
Post a Comment