HEADER AD

HEADER AD

MUWASA YAPOKEA MILIONI 278 KUBORESHA CHANZO CHA MAJI NYANDURUMO


Na Dinna Maningo, Tarime

MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira( MUWASA ) Musoma- Kanda ya Tarime imepokea fedha kutoka serikalini kiasi cha Tsh. 278,000,000.00 kati ya 387,364,926.66 kwa ajili ya kuboresha ubora wa maji kupitia chanzo cha chemchemi ya Nyandurumo inayohudumia wakazi wa Tarime mjini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MUWASA) Mhandisi Nicas Mugisha amesema usanifu na tathmini ya kujenga mfumo wa kuchuja maji katika chanzo cha maji cha Nyandurumo umekamilika na kibali cha kuanza kujengwa kwa mtambo mdogo wa kuondoa tope kilishatolewa.

"Mradi huu unalenga kuboresha ubora wa maji , gharama za mradi ni 387,364,926.66, fedha zilizopekelewa 278,000,000.00, mfadhili ni serikali. Muda wa utekelezaji ni februari, 2024 mpaka Desemba, 2024.

"Kazi zitakazotekelezwa ni ujenzi wa chujio , na mradi upo katika hatua za manunuzi ya malighafi za ujenzi. Mradi huu ukikamilika utaongeza ubora wa maji Tarime mjini" amesema Mugisha.

Amesema kuwa chemchemi ya Nyandurumo ndiyo chanzo kikuu cha maji katika mji wa Tarime na utegemewa sana kuzalisha maji.

Amesema ubora wa maji katika chanzo hicho ni hafifu kutokana na kuzungukwa na shughuli nyingi za binadamu hasa kilimo.

"Pamoja na kuweka dawa ya kuua wadudu (Chlorine) ,changamoto kubwa katika chanzo hicho ni uwepo wa kiasi kikubwa cha tope katika maji kutokana na kutokuepo miundombinu ya kisasa ya kuondoa tope" amesema.

Ameongeza kuwa mamalaka ya maji safi na usafi wa mazingira Musoma -Kanda ya Tarime katika robo ya pili ya mwaka 2023/2024 imezalisha kiasi cha mita za ujazo 98,197.59 ambapo jumla ya wateja wanaopata huduma ya maji mpaka kufikia 31, 12, 2023 kutoka kanda ya Tarime ni 2,744.

Bhoke Marwa mkazi wa Rebu Senta  amesema kuwa chanzo hicho kikiboreshwa kitasaidia sana wananchi kwani mara kadhaa hasa vipindi vya mvua maji kutoka chanzo cha Nyandurumo ni machafu yanabadili rangi za nguo nyeupe.

No comments