HEADER AD

HEADER AD

RC MARA AWATAKA WATAALAM WA KILIMO KUWATEMBELEA WAKULIMA

Na Dinna Maningo, Tarime

MKUU wa mkoa wa Mara Said Mtanda amewaagiza wataalam wa kilimo, mifugo na maafisa ugani kuwatembelea wakulima mashambani badala ya kukaa ofisini.

Mkuu huyo ameyasema hayo hivi karibuni mjini Tarime wakati akizindua kiwanda cha kuchakata kahawa kavu na mbivu kilichojengwa na Chama kikuu cha Wakulima wa Mara (WAMACU LTD).

       Mkuu wa mkoa wa Mara Said Mtanda akizungumza

RC Mtanda amesema kuwa Serikali ilitoa pikipiki kwa wataalam wa kilimo nchini ili kuwasaidia kuwafikia wakulima mashambani waweze kutatua changamoto zao na kuwapa elimu lakini wataalam hao hawawatembelei wakulima.

"Wataalam wetu wa kilimo wamewezeshwa sana kupitia wizara ya kilimo wana mapikipiki yana ma GPS kila kitu lakini bado hawaendi kwa wakulima.

"Bado hawavitembelei vikundi vya ushirika, kwahiyo kupitia hadhara hii nitoe wito waondoke kwenye maofisi wawafikie wakulima" amesema Mtanda.

Pia Mtanda amewataka wakuu wa idara ya kilimo na mifugo na wataalam wa kilimo, ugani na mifugo nao wawe na mashamba yao na mifugo ili wawe wa mfano.

       Mkuu wa mkoa wa Mara Said Mtanda akisalimiana na viongozi wa chama kikuu cha wakulima wa kahawa Mara pamoja na wadau wa kilimo.

"Afisa kilimo kutokuwa na shamba au afisa mifugo kutokuwa mfugaji ni fedheha ,tunataka tuone mashamba ya wataalam wetu ili tuone haya wanayotufundisha na kwenye mashamba yao je hayo wanayosema yapo hivi hivi?.

" Ukiongoza lazima na wewe uwe wa mfano uwe wa vitendo na sio kwa maneno, siku nyingine nikija hapa nitataka tutembelee mashamba ya wataalam kwanza tuyaone ndipo twende kwenye mashamba ya wananchi" amesema Mtanda.

Katibu wa mbunge wa jimbo la Tarime mjini Elias Samo amesema kuwa wataalam wakiwafikia wakulima watasaidia wakulima wengi kupata elimu ya kilimo bora na mashamba yataongezeka.

      Katibu wa mbunge wa jimbo la Tarime mjini Elias Samo

No comments