HEADER AD

HEADER AD

RC MARA : BENKI YA TADB HAMASISHENI KILIMO CHA KAHAWA


Na Dinna Maningo , Tarime

MKUU wa mkoa wa Mara Said Mtanda ameishauri Benki ya Maendeleo ya Wakulima (TADB) kufika katika Kata zinazojihusisha na kilimo haramu cha bangi katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, kutoa elimu kwa wakulima kulima kilimo cha Kahawa.

Amesema kuwa wilaya ya Tarime kuna ardhi nzuri ya kilimo cha kahawa na kwamba wakulima wakilima kahawa kwa wingi kiwanda kitapata malighafi na kitaweza kujiendesha.

Pia amesema kuwa TADB itafika na kuzungumza na wakulima na kuwahamasisha kulima nyasi za mifugo kisha ikawakopesha ng'ombe wa kisasa wa maziwa itasaidia wakulima wengi kuachana na kilimo cha bangi.

RC Mtanda amesema hayo, Januari, 31,2024 wakati akizindua Kiwanda cha kuchakata kahawa kavu na mbivu kilichojengwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima mkoa wa Mara (WAMACU LTD).

     Mkuu wa mkoa wa Mara, Said Mtanda akifurahia baada ya kuzindua kiwanda cha kuchakata kahawa kilichopo mjini Tarime

Mtanda amesema kwamba hivi karibuni walikwenda kifyeka na kuteketeza mashamba ya bangi zaidi ya ekari 1,000  katika bonde la mto Mara.

"Benki ya TADB angalieni maeneo ya Tarime yapo maeneo mazuri kwa ajili ya kilimo, badala ya wananchi kulima bangi tuwahamasishe walime majani kwa ajili ya mifugo, au walime kahawa, mpunga na mazao mengine.

Hapa Tarime tunakumbuka tulikwenda kufyeka mashamba ya bangi bonde la mto Mara, kumbe lile bonde wakulima wakishikamana na Benki ya Kilimo wanaweza kutumia bonde lile kuzalisha nyasi za mifugo, vikundi vikaundwa vikakopeshwa ng'ombe wa maziwa wa kisasa" amesema Mtanda.

Mkuu huyo wa mkoa ameongeza kusema " Bonde hilo wanalolitumia kulima bangi wakulima walitumie kulima nyasi alafu wakawa na kikundi cha maziwa, baadae wakaanza kukusanya maziwa na tukawa na kiwanda cha maziwa pia na kusindika maziwa.
 
     RC Said Mtanda akizungumza na wakulima wa Kahawa, kushoto kwake ni mkuu wa wilaya ya Tarime Michael Mntenjele.

" Niliwauliza kwanini mnalima bangi wakasema huku tukilima mpunga ndege ni wengi sana wanashambulia mpunga, lakini kumbe eneo lile tukilima pia kahawa na kiwanda kipo tunaweza inua uchumi wa wananchi Tarime " amesema Mtanda.

Mtanda amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amekuwa akitafuta fedha hata nje ya nchi kuwekeza katika benki ya TADB akiwa na uhakika kuwa benki hiyo ikihimalika na kuwa na mtaji mkubwa itasaidia kuwafikia wakulima wengi nchini.

" Benki yetu ya kilimo ni benki ambayo imewezeshwa sana na imekuwa kimtaji, ilianza na mtaji wa sh.bilioni 60 leo wanazungumzia zaidi ya bilioni 200.

" Nimeshuhudia pale Mwanza vimenunuliwa vifaa vya vizimba zaidi ya 50, Boti zaidi ya 120 lakini pia mwaka ujao wa fedha watatoa zaidi ya Boti 500 kwa wavuvu kwa hiyo maana yake benki ya kilimo imehimarika zaidi" amesema Mtanda.

       Mkuu wa mkoa wa Mara Said Mtanda akiwa kwenye picha ya pamoja na wakulima wa WAMACU

Mtanda amewataka wanachama, vikundi na mkulima mmoja mmoja kutumia fursa za benki hiyo kupata mikopo kama ilivyotoa mkopo wa ng'ombe wa maziwa kwa wakazi wa mkoani Kagera ili kujiongezea kipato.

Mkazi mmoja wa Kijiji cha Nkerege Kata ya Kiore Chacha Marwa amesema kuwa wakulima wakipata elimu ya kulima mazao mengine yenye faida na kipato kikubwa na wakawezeshwa mikopo wataacha kulima bangi.

Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima mkoa wa Mara, Samwel Gisiboye amesema chama kimeweza kununua na kusimika mashine kubwa ya kuchakata kahawa mbivu na kavu kwa thamani ya Tsh. 1, 303, 376, 250.

       Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima mkoa wa Mara, Samwel Gisiboye.

Amesema Chama kinakabiliwa na changamoto ya baadhi ya maeneo ya chama na vyama wanachama kuvamiwa na watu binafsi na taasiai zingine.

Hali hiyo upelekea kuwepo migogoro ya mara kwa mara inayodumaza maendeleo ya sekta ya ushirika katika mkoa huo na changamoto nyingine ni uwepo wa uzalishaji mdogo wa kahawa usio kidhi malengo ya kiwanda.

Pia mkuu huyo wa mkoa alipongeza chama hicho kwa kununua mashine za kuchakata kahawa kavu na mbivu na kwamba kiwanda hicho kitasaidia kuinua uchumi wa wananchi Tarime.

       Wanachama wa WAMACU

No comments