HEADER AD

HEADER AD

TAKUKURU KAGERA YABAINI MIRADI 16 YA BILIONI 4.2 YENYE MAPUNGUFU

Na Alodia Babara, Bukoba

TAASISI ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa mkoa wa Kagera kwa kipindi cha Oktoba-Desemba 2023, imefuatilia miradi 19 yenye thamani  zaidi ya Tsh. Bilioni 6.1 ambapo kati ya hiyo miradi 16 yenye thamani zaidi ya Tsh. Bilioni 4.2 imebainika kuwa na mapungufu yaliyohitaji marekebisho.

Kamanda wa Taasisi hiyo mkoani humo Pilly Mwakasege amesema kuwa kiasi hicho ni sawa na asilimia 68.50 ya fedha za miradi ambapo kumekuwa na ongezeko la asilimia 18.77 ya miradi hiyo, ukilinganisha na kipindi cha Julai-Septemba mwaka jana.

Mwakasege ameeleza hayo leo Februari 06,2024 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yao kwa kipindi cha robo tatu ya mwisho wa mwaka 2023 ambapo,miradi iliyohusika ni ya ujenzi wa miundombinu ya shule mpya za msingi na sekondari.

 Kamanda wa Taasisi hiyo mkoani humo Pilly Mwakasege

Miradi mingine ni maji, zahanati pamoja na ujenzi wa madarasa ya msingi na sekondari ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kuendana na thamani ya fedha iliyotumika.

Mwakasege amesema kuwa kwa kipindi hicho walipokea malalamiko 92 kati ya hayo 58 hayahusu rushwa ambapo 34 yanahusu rushwa na majalada yamefunguliwa ambapo 20 uchunguzi wake umekamilika na hatua stahiki zinatarajiwa kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.

“Idara zilizolalamikiwa ni Halmashauri ambapo idara ya fedha kesi ni moja, Elimu 10, Afya saba, utawala 12, biashara moja, kilimo nane, ardhi saba, mazingira tatu na mengine yalihusu sekta binafsi ambayo ni 12.

"Idara zingine zilizolalamikiwa ni idara ya maji kesi tatu, ujenzi kesi tisa, maliasili saba, nishati moja,uhamiaji mbili, polisi nne, mahakama tatu, uchukuzi moja na mamlaka ya mapato Tanzania moja"ameeleza Mwakasege.

 Amesema katika progaramu ya TAKUKURU rafiki ambayo inatekelezwa kwa kushirikisha wadau katika ngazi ya kata, wananchi hupata fursa ya kuibua kero zinazowakabili katika maeneo yao.

Amesema kwa kipindi cha Oktoba-Desemba walitembelea kata 11 na kupokea kero kuhusu sekta za Elimu, Afya, maji, fedha na nishati ambapo ufuatiliaji wake unaendelea.

Aidha amevitaja vipaumbele vya TAKUKURU kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka huu ambavyo ni kuelimisha umma kupitia njia mbalimbali ili kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika kuzuia vitendo vya rushwa.

Pia kutatua kero mbalimbali katika jamii kupitia programu ya TAKUKURU Rafiki na kuendelea kufuatilia rasilimali za umma kupitia ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuzuia ufujaji wa fedha za umma.

 Vipaumbele vingine ni kufanya chambuzi za mifumo kwa lengo la kuzuia rushwa zinazosababishwa na mapungufu yaliyopo kwenye mifumo ya utendaji wa sekta ya umma na sekta binafsi.

Amewahimiza wasimamizi wa miradi ya maendeleo kuwa waadilifu na kuhakikisha fedha zote za miradi zinatumika vizuri.

 

No comments