WAMWELEZA MWENYEKITI JUMUIYA YA WAZAZI CHANGAMOTO KATA YA MURIBA
Na Dinna Maningo, Tarime
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara na Wilaya ya Tarime kimeombwa kuingilia kati kusaidia changamoto zilizopo Kata ya Muriba ziweze kutatuliwa kwa wakati.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi ambapo Mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi mkoa wa Mara, Julius Kambarage Masubo, Diwani wa Kata ya Muriba, Mniko Msabi Mariba amesema kuwa tangu awe Diwani kuna mabadiliko makubwa isipokuwa bado kuna changamoto zinahitaji kutatuliwa.
Diwani amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na tatizo la upatikanaji wa maji, ubovu wa miundombinu ya barabara, vitongoji vingi kutofikiwa na umeme, Wanafunzi 400 katika shule ya sekondari Muriba kukaa chini na ukosefu wa walimu akiwemo mwalimu wa somo la kingereza.
"Naomba chama changu muingilie kati changamoto hizi zitatuliwe maana zinawagusa wananchi wengi moja kwa moja, katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM tuliahidi huduma ya maji lakini kijiji cha Bungurere hakijafikiwa na mradi wa maji.
"Barabara katani kwangu ni tope TARURA haijatengeneneza huwa naona aibu namna wananchi wangu wanavyopita wanateleza, wanaanguka. Umeme ni shida vitongoji vingi havina umeme hata kitongoji nachoishi mimi hakuna umeme umeme umepita tu barabarani" amesema Diwani Mariba.
Akizungumzia mafanikio yaliyofanyika kata ya Muriba Diwani amesema hadi sasa Kata hiyo imepata Bilioni 1.5 zilizotolewa kutekeleza miradi ya maendeleo.
"Pamoja na changamoto hizo naipongeza serikali kwa kuto fedha ambazo zimetekeleza miradi mbalimbali ukiwemo ujenzi wa madarasa, zahanati. Tunaomba watumishi waajiriwe ili wananchi wapate huduma kwa wakati" amesema Diwani.
Wakati huohuo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kaya ya Itiryo Magahu Peter Muhere ameiomba kamti ya siasa isaidie shule zipate walimu kwani kata yake ina changamoto za uhaba wa walimu ikiwemo shule ya msingi na sekondari Kangariani.
"Shule ya msingi na sekondari Kangariani wanafunzi wamefeli sana kwa sababu walimu ni wachache hii ni changamoto kubwa tunaomba kamati ya siasa mtusaidie mlifanyie kazi" amesema Muhere.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Mara Julius Kambarage Masubo amewapongeza wanachama wa CCM na viongozi kwa kufanya vizuri kazi ya chama na hivyo chama hicho kuendelea kushika dora huku akiahidi chama hicho kitafuatilia kuhakikisha changamoto za wananchi zinatatuliwa.
Post a Comment