AFISA MADINI MARA AWAHIMIZA WANANCHI KUTUMIA MAFUNZO UGANI KUWASILISHA KERO ZAO
Na Jovina Massano, Musoma
WANANCHI wanaomiliki wa ardhi, wadau wa sekta ya madini wilayani Tarime wametakiwa kutumia fursa ya mafunzo ugani kuwasilisha kero zao.
Hayo yamesemwa March 6,2024 na Afisa madini mkazi mkoa wa Mara, Mhandisi Amin Msuya wakati akiwasilisha taarifa ya mtambo wa uchorongaji madini kwenye kikao cha Baraza la ushauri la mkoa katika ukumbi wa uwekezaji.
Msuya amesema kuwa ofisi ya madini imeweka utaratibu wa kukutana na wadau wa sekta hiyo na kuwapa elimu ya mafunzo ugani kila wiki ya kwanza ya mwezi.
Mbali na mafunzo hayo wadau wanapata fursa ya ufafanuzi wa sheria, taratibu, kanuni za wachimbaji ikiwemo kusikiliza changamoto mbalimbali na kutolea ufafanuzi na kuchukua maamuzi kwa kadri ilivyo.
Amesema lengo la elimu na mafunzo hayo ni kuisaidia jamii na wadau kutambua taratibu na sheria za madini na wajibu wao kisheria.
Amesema katika kudhibiti kasi ya utoroshaji wa madini ofisi inaendelea kutoa elimu ya mlipa kodi, ya undeshaji uchimbaji na biashara ya madini kwa kufuata sheria ya madini na kanuni zake, kaguzi za mara kwa mara katika maeneo ya uchimbaji, uchenjuaji na masoko sambamba na kufanya vikao na wachimbaji, wachenjuaji na wafanya biashara.
Ili kuhakikisha Ofisi inatimiza majukumu yake kwa ufanisi zaidi amesema ofisi hiyo imeweka mipango madhubuti kwa kufanya vikao mara moja kwa mwezi kutoa huduma ikiambatana na kutatua migogoro kwa wakati.
Pia kuendelea kuboresha mahusiano na taasisi fungamani kuhakikisha mashine ya uchorongaji inatumika ipasavyo ili kuboresha eneo la utafiti na kuongeza uzalishaji katika migodi iliyopo na kuanzisha migodi mipya.
"Hii itaenda sambamba na utekelezaji wa Sera ya Madini 2030 Madini ni maendeleo na utajiri, kusimamia kwa ufanisi timu ya umeme na barabara migodini kuwasaidia wawekezaji wanaofanya uchimbaji wa kati na Technical Support katika maeneo ya Bunda, Serengeti (Changshen mining) na Musoma (MMG, Polygold na Idera) ili kuongeza uzalishaji" amesema Msuya
Afisa huyo wa madini amesema ufunguzi wa vituo vya ununuzi Suguti na Serengeti utasaidia kupeleka huduma karibu na wananchi na kudhibiti kwa ukaribu mnyororo wa biashara ya dhahabu.
" Ofisi inashirikiana STAMICO na NEMC kuanzisha mialo miwili ya mfano na CPI ya kuhudumia wachimbaji wadogo kwa kushirikiana na mgodi wa North Mara kuona uwezekano wa kutenga maeneo kwa wachimbaji wadogo ili kupunguza uvamizi mgodi hapo" amesema Msuya.
Amesema kutokana na miundombinu rafiki ya barabara Ofisi ya madini imekuwa inayafikia maeneo yote yenye uchimbaji wa madini kwa majira yote.
"Madini yanayopatikana katika mkoa ni pamoja na dhahabu, fedha (Tarime) dhahabu shaba, fedha, chuma (Bunda, Rorya na Butiama), chokaa (Bunda), soapstone(Bunda na Serengeti) na madini ya ujenzi lakini pia Kuna Madini yanayochimbwa kibiashara mpaka sasa ambayo ni dhahabu, fedha na madini ujenzi.
"Ofisi ya madini kwa kiasi kikubwa inategemea madini ya dhahabu kwa kuwa ndio yanayozalishwa kwa wingi katika mkoa wetu. Hivi sasa leseni za madini ya shaba ziko kwenye utafiti na ni mategemeo zitakuwa na mchango katika mkoa kwa kipindi cha karibuni", amesema Msuya.
Aidha ameainisha malengo ya makusanyo ya ofisi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni takribani Tsh. Bilioni 153 ambapo hadi kufikia mwishoni mwa Februari, 2024 ofisi imekusanya kiasi cha Tsh. 77,336,141,536.49 sawa na asilimia 51.6 ya lengo la mwaka.
"Mwaka 2022/2023 ofisi ilipewa lengo la kukusanya Tsh.Billioni 149 na ikafanikiwa kukusanya Tsh. Bilioni 120.57 sawa na asilimia 80.9 ya lengo.
"Mkoa una jumla ya leseni za utafiti wa madini zipatazo 75 aidha leseni kadhaa zinaendelea kufanyiwa kazi kama Sheria na Kanuni za Madini zinavyoelekeza lakini pia hadi kufikia Februari, 2024 jumla ya leseni za uchimbaji mkubwa, wakati na ndogo zipatazo 1,732 zimetolewa" amesema.
Ameeleza kuwa, mkoa una Soko kuu la Madini moja katika Manispaa ya Musoma,Vituo vya ununuzi wa madini (buying centres) vinne (4) ambavyo ni Bunda, Nyamongo, Irasanilo na Tarime .
"Hivi sasa kituo kipya cha Suguti kilichopo halmashauri ya Musoma Vijijini kipo katika hatua ya mwisho kuanza kazi lakini pia ofisi ya madini ipo mbioni kuanzisha kituo cha ununuzi katika Wilaya ya Serengeti ambapo kuna uchimbaji wa dhahabu kwa wachimbaji wadogo" amesema.
Amesema wazo hilo lilitolewa na wadau katika mojawapo ya vikao vya kila mwezi vinavyofanyika kwa kuwakutanisha wadau wa sekta ya madini pamoja na idara zinazofungama na sekta ya madini katika mkoa.
Pia amesema kwamba, kituo cha Nyamongo kiko kwenye mpango wa ujenzi wa kisasa kwa CSR ya North Mara ambapo kiasi cha Tsh. Milioni 800 imetengwa.
"Katika kipindi cha Mwezi Julai 2023 hadi Februari 2024, ofisi ya Madini Mara imefanikiwa ukusanya shillingi 77,336,141,536.49 sawa na asilimia 50.6 ya lengo la mwaka 2023/2024 la Tsh Billioni 153" amesema.
Ameongeza kuwa ofisi ya madini katika kuendelea na majukumu yake inaendelea kusikiliza, kuwatembelea na kuwahudumia wateja kwa weledi, na ujali ili kuhakikisha inatatua changamoto mbalimbali za kichimbaji zinazojitokeza, kuanzisha vikao vya kila mwezi vyenye lengo la kusikiliza maoni mbalimbali.
" Kutatua changamoto za wachimbaji, kutoa elimu ya Sheria ya Madini na Kanuni zake kwa Wachimbaji na Wafanyabiashara wa madini,vikao hivi pia huwakutanisha wachimbaji na maafisa wa taasisi mbalimbali fungamani katika sekta ya madini kama vile TRA, Halmashauri, Zimamoto na uokoaji, Polisi, TANESCO, na TARURA" amesema Msuya.
Post a Comment