HEADER AD

HEADER AD

WILAYA YA NGARA, BUKOBA ZAONGOZA KWA KIWANGO KIKUBWA CHA UGONJWA WA MALARIA


Na Alodia Babara, Bukoba

MKOA wa Kagera ni miongoni mwa mikoa mitano ya Tanzania ambayo inakabiliwa na kiwango kikubwa cha ugonjwa wa Malaria.

Kutokana na utafiti wa viashiria vya ugonjwa huo kwa mwaka 2022 kiwango cha maambukizi ilikuwa asilimia 18 ambapo kiwango cha maambikizi kwa wagonjwa wanaopimwa ugonjwa huo katika vituo vya Afya mwaka 2023 ni asilimia 33.9.

Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwasa ametoa takwimu hizo Machi 06,2024 wakati wa ufunguzi wa kikao cha kamati ya ushauri cha mkoa huo kilichojadili mambo mbalimbali ikiwemo taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya mkoa huo katika mwaka 2023/2024 kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2023 pamoja na rasmu ya bajeti ya matumizi ya kawaida na mpango wa maendeleo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025.

       Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwasa

Amesema kutokana na utafiti huo ilionyesha Halmashauri ya Ngara ndiyo inaongoza kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria asilimia 49 ikifuatiwa na Bukoba asilimi 41 na Biharamulo asilimia 34.7 hivyo kutokana na ukubwa wa tatizo hilo wanapaswa kushirikiana wote kwa pamoja ili kuhakikisha maralia inaondoka katika mkoa huo kwa sababu hari kwa sasa inatisha.

Amesema sekta ya Afya mkoani humo  inakabiliwa na changamoto ya milipuko ya magonjwa ambapo mwaka jana walikabiliwa na mlipuko wa Marburg, Surua na Kipindupindu.

Amesema wagonjwa 161 walilipotiwa kuugua kipindupindu kati ya hao 151 walipona huku wagonjwa kumi wakifariki na sasa ugonjwa huo umedhibitiwa katika halmashauri ya Missenyi, halmashauri ya Bukoba na Manispaa ya Bukoba.

“Mlipuko wa ugonjwa huu unaendelea kuwepo katika kisiwa cha Goziba kilichopo Wilayani Muleba niendelee kuelekeza uongozi wa Wilaya hiyo kuimalisha zaidi usimamizi ili kudhibiti kabisa ugonjwa huo hii.

Pia kuwahimiza wananchi wa kisiwa hicho kuchimba vyoo na kuvitumia, magonjwa hayo ya mlipuko hususani kipindupindi yanaenea kutokana na uchafu wa mazingira hasa kutokuwa na vyoo kwa wananchi wanaoishi eneo hilo”amesema Mwassa.

Ameeleza kwamba usimamizi imara ukiwepo wa wananchi kwa kufuata kanuni za Afya kwa kuchimba vyoo na kuzingatia usafi wa mazingira itamaliza tatizo hilo.

Aidha katibu tawala wa mkoa wa Kagera Toba Nguvila amewataka watumishi wa idara ya Afya ambao wanahusika na kitengo cha lishe kutumia fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuondokana na udumavu ambao kwasasa ni asilimia 32 kwa mkoa huo, kuliko kuzitumia kulipana posho kama wanavyofanya hivi sasa.

“Kwa sasa kuna udumavu mkubwa katika mkoa huu unajiuliza tumekwama wapi hii ni jukumu letu sote kila Halmashauri tuone tunaondokana vipi na tatizo hili na kwenye bajeti inayopangwa tuisimmamie ili ikatende zile afua za lishe.

"Unakuta bajeti zinapangwa lakini matumizi yanaelekezwa kwenye posho, madhara ya udumavu hayaonekani kwa wakati huo lakini tunakwenda kuweka kizazi ambacho ufikiri wake ni mdogo na madhara ya udumavu yanasababisha kushuka kwa kiwango cha elimu" amesema Nguvila

Wakati huo huo, katika taarifa iliyosomwa na Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini na Mjini (RUWASA) Wilaya ya Ngara, Mhandisi Simeon Ndyamukama amesema Serikali katika rasimu yake imetengwa kiasi cha Tsh. Bilioni 19.7.

Amesema fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi 50 kupitia RUWASA kwa kipindi cha mwaka 2024/2025 ili kuwezesha wanachi kupata maji safi na salama ya uhakika ambapo kwa sasa mkoa wa Kagera upatikanaji wa maji umefikia asimilia 70.6.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Avit Theodori amesema Serikali imetoa kiasi cha Tsh. Milioni 982 kwa ajili ya kukarabati barabara mbalimbali mkoa wa Kagera zilizoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa.

Hata hivyo, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 mkoa wa Kagera ulipitisha bajeti  kiasi cha Tsh. Bilioni 353.5 ambapo hadi desemba 2023 kiasi kilichopokelewa ni Tsh. Bilioni 193.9 na kwa mwaka 2024/2025 na wanakisia kutumia zaidi ya Tsh. Bilioni 384.2.


No comments