BODI YA BARABARA YAVUTIWA NA UTENDAJI KAZI WA MENEJA TANROADS, TARURA PWANI
Na Gustafu Haule, Pwani
WAJUMBE wa kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Pwani wameridhishwa na utendaji kazi wa Meneja Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS)Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage wakisema amekuwa msimamizi mzuri wa miradi ya barabara inayotekelezwa mkoani humo.
Kauli za wajumbe kupongeza juhudi za meneja huyo zimekuja baada ya meneja huyo kumaliza kuwasilisha taarifa ya utekelezaji ya matengenezo ya barabara za mkoa na barabara kuu kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024 .
Mbali na taarifa hiyo lakini pia mhandisi Mwambage katika kikao hicho amewasilisha makisio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwa Tsh.Bilioni 18.9 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na Tsh. Bilioni 19.4 Kwa ajili ya maendeleo.
Kikao hicho kilichofanyika Machi 7, mwaka huu mjini Kibaha kiliongozwa na Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge ambapo wajumbe kwa umoja wao walifurahi kuona miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Tanroads Mkoa wa Pwani.
Taarifa iliyowasilishwa na Mwambage katika kikao hicho ilitaja miradi 18 ya kimkakati inayotekelezwa Mkoani Pwani ikiwemo ujenzi wa barabara ya mwendo wa haraka (Expressway) yenye Kilomita 220 inayoanzia Kibaha -Chalinze,Daraja la Wami, barabara ya Tamco-Vikawe yenye Kilomita 23, Makurunge -Saadan- Tanga.
Mingine ni Kibiti-Mloka iliyopo Wilayani Kibiti yenye Kilomita 100.8,Utete - Nyamwage yenye Wilayani Rufiji yenye Kilomita 33.7,Kibaha - Kisarawe (19.8),Maneromango -Vikumburu-Mloka na kuelekea katika mradi wa kufua umeme katika bwawa la Mwalimu Nyerere (198.71) na Makofia,Mlandizi- Maneromango(100).
Mbunge wa Jimbo la Kibiti Twaha Mpembenwe, akizungumza katika kikao hicho amesema kuwa mhandisi Baraka Mwambage amekuwa na ushirikiano mkubwa na hata kutoa ushauri ambao kwa namna moja au nyingine umeleta mafanikio makubwa katika Jimbo lake.
Wajumbe wa kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Pwani wakisikiliza taarifa ya utekelezaji wa miradi ya barabara iliyokuwa ikitolewa na meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani mhandisi Baraka Mwambage katika kikao cha Bodi hiyo kilichofanyika jana Mjini Kibaha.
Mpambenwe amesema sasa hivi anajivunia kuwa na meneja huyo kwani miradi mingi inatekelezeka na sasa Kibiti inafunguka kimaendeleo kwakuwa barabara zinapitika muda wote na wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao vizuri.
"Kiukweli meneja huyu lazima tumpongeze kwani anafanyakazi nzuri na amekuwa na ushirikiano mkubwa na mara nyingi amekuwa akitoa ushauri kuhusu fedha zinazotengwa za ujenzi wa barabara kuwa tuzipeleke babaraba fulani huku akitoa sababu ya kwanini fedha hizo tuzipeleke huko,"amesema Mpembenwe.
Mpembenwe amesema kuwa kwa ushauri wa Meneja wa TANROADS na hata meneja wa TARURA umekuwa ukichochea maendeleo ya Jimbo la Kibiti lakini hata kuweka vizuri katika masuala ya kisiasa.
Nae Mbunge wa viti -maalum Subira Mgallu amesema kuwa kazi inayofanywa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani na Meneja wa TARURA Leopold Runji ni kubwa na inaleta heshima kubwa kwa Mkoa wa Pwani.
"Mimi naungana na wenzangu waliotangulia kuchangia katika kikao hiki kiukweli huyu meneja wa TANROADS mkoa pamoja na meneja wa TARURA wanafanyakazi kubwa na nzuri na sasa hivi tunaona mabadiliko ya barabara ndani ya Mkoa wetu,"amesema Mgallu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini Erasto Makala ameunga mkono kauli ya wajumbe wenzake huku akisema barabara nyingi kwasasa zinapitika kutokana na juhudi za meneja wa TANROADS na TARURA.
Makala amesema zipo changamoto ndogondogo za madaraja lakini hatahivyo zinafanyiwa kazi na kwamba matumaini yake baada ya kipindi kifupi Kibaha Vijijini itakuwa na barabara zinazopitika wakati wote
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Benard Ghaty, amesema kuwa meneja wa TANROADS mkoa wa Pwani na meneja wa TARURA wamekuwa na ushirikiano mzuri ndio maana chama kinawasaidia kuwasemea pale pesa zinapokosekana za utekelezaji wa miradi husika.
Ghaty ametoa wito kwao kuhakikisha wanazisimamia vizuri fedha zinazokuja kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara kwani wakifanya vizuri watakuwa wameleta heshima kwa chama na kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anayepigania maendeleo ya Taifa.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amesema kuwa chama kuipongeza Serikali ni heshima kubwa na kwamba amekishukuru chama kwa msaada wanaotoa na wao wapo tayari kufanya yale yanayokusudiwa kwa heshima ya Rais Samia na Taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,akiongoza kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika Machi 7,mwaka huu Mjini Kibaha.
"Sisi wasaidizi wa Rais lazima tuhakikishe tunafanya yale yaliyokusudiwa hasa katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwatumikia Wananchi kwa kutatua kero mbalimbali na tukifanya hivyo tutakuwa tumemtendea haki Rais wetu,"amesema Kunenge.
Post a Comment