HEADER AD

HEADER AD

AKAMATWA KWA KUTUMIA MWAMVULI WA DINI KUFANYA SHUGHULI ZA UGANGA, RAMLI CHONGANISHI

 Na Alodia Babara, Bukoba

JESHI la Polisi mkoani Kagera linamshikilia Domina Abrahamu (48) mkazi wa kilimahewa kata ya Kashai Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera kwa tuhuma za kutumia mwavuli wa dini kufanya shughuli za uganga wa kienyeji, ramli chonganishi na kutapeli watu fedha.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera, Blasius Chatanda ametoa taarifa hiyo Machi 25, 2024 wakati akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari mkoani humo.

Chatanda amesema kuwa mtuhumiwa huyo amekamatwa Machi 20, 2024 saa 12.00 jioni mtaa wa kilimahewa kata ya Kashai manispaa ya Bukoba.

Mtuhumiwa alikamatwa baada ya kudaiwa kumrubuni Charles Robert (41) fundi seremala mkazi wa kilimahewa kwa kumwambia kuwa yeye anatoa huduma ya maombezi kwa watu na kuwa ameonyeshwa na mwenyezi Mungu kwamba mke wake aitwaye Edina Sadoth ana matatizo ya kusumbuliwa na ndoto mbalimbali.

Ameongeza kuwa mtuhumiwa huyo alimtaka Charles atoe fedha kiasi cha Tsh. 70,000 kwa kipindi ambacho atakuwa akimfanyia  maombi akiwa nyumbani kwake.

       Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera, Blasius Chatanda akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake

"Baada ya jeshi la polisi mkoani hapa kupata taarifa hizo askari walichukua hatua za haraka kwa kufuatilia jambo hili na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa nyumbani kwake.

" Upekuzi ulifanyika katika makazi yake ambapo kulikuwa na ukumbi uliokuwa ukitumika kama kanisa na vyumba viwili ambavyo vilikuwa vinatumika kwa shughuli za tiba asilia/uganga wa kienyeji vikiwa na vifaa" amesema Kamanda.

Kamanda Blasius ameongeza kusema "Vifaa hivyo ni mikuki miwili, mmoja wa chuma na mwingine wa mbao, ngao mbili za mbao, upinde mmoja, mishale mitatu, kinanda cha mbao kimoja, fimbo za shanga mbili, kiti kimoja cha urembo, kichwa kimoja cha mkuki.

"Cheti cha tiba asili na mbadala chenye namba ya usajili s.a.20796, cheti cha usajili wa kuendesha shughuli za sanaa chenye namba za usajili b.s.t/00338 na barua ya utambulisho ya taasisi ya united kingdom of Afrika ya tarehe 13/10/2023 na makopo yenye dawa mbali mbali za tiba asili" amesema Kamanda.

Ameongeza kuwa, baada ya mtuhumiwa kufikishwa kituo cha polisi na kuhojiwa jeshi hilo limebaini kuwa mtuhumiwa anatumia mwavuli wa dini kufanya shughuli za uganga wa kienyeji na ramli chonganishi zinazopelekea migogoro kwenye familia na jamii kwa ujumla na kwamba mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara tu upelelezi na taratibu za kisheria zitakapokamilika.

Ametoa Rai kwa wananchi kujiepusha na watu ambao wanafanya shughuli za uganga wa jadi wakiwa hawajasajiliwa kwani haiwezekani mtu huyo huyo afanye kazi za uganga wa tiba asili na shughuli za maombezi.

No comments