WATOTO NJITI WALALA KITANDA KIMOJA HOSPITALI YA RUFAA MARA
Na Dinna Maningo, Musoma
UFINYU wa Wodi ya Watoto Njiti katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, unawalazimu watoto zaidi ya mmoja kulala kwenye kitanda kimoja.
Hayo yalibainika hivi karibuni wakati Wanawake kutoka shirika lisilo la kiserikali la Health & Safe Delivery Baby Foundation (HSF) lenye makao makuu Nyamongo Wilayani Tarime, likiongozwa na Mkurugenzi wa shirika hilo Emmyliana Julius Range pamoja na wanawake kutoka Shirika la Power Life Health & Wealth likiongozwa na Mkurugenzi Mariam Selemani walipotembelea wodi ya mama na mtoto.
Wanawake hao walifika katika hospitali hiyo wodi ya mama na watoto kuwajulia hali wajawazito na wazazi waliojifungua ambapo walitoa msaada wa vitu mbalimbali zikiwemo kanga, sabuni, taulo za kike na majani tiba ya chai ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani.
Muunguzi Kiongozi Kitengo cha watoto wachanga hospitali ya rufaa mkoa wa Mara, Stella Shengoma amesema kuwa wodi ya watoto njiti ina uwezo wa kupokea watoto 15-20 lakini wakati mwingine inapokea watoto hadi 37.
Muunguzi Kiongozi katika Kitengo cha watoto wachanga hospitali ya rufaa mkoa wa Mara, Stella Shengoma
akizungumza na wanawake kutoka shirika la Health & Safe Delivery Baby Foundation (HSF) na Shirika la Power Life Health & Wealth walipofika kutembelea wodi ya mama na mtoto."Tuna changamoto ya nafasi kama unavyoona wodi imejaa, kama msimu uliopita tulikuwa na watoto 30, hali hiyo inasababisha watoto zaidi ya mmoja kulala kwenye kitanda kimoja.
Amesema kuwa mbali na watoto kuchangia kitanda kimoja, ufinyu wa chumba unasababisha watoa huduma wasiweze kufanya kazi kwa ufanisi, hivyo anaiomba Serikali kuwajengea wodi pana.
" Ufinyu wa chumba unasababisha hata kupishana inakuwa shida, huduma haziwezi kwenda harakaharaka kama vile kungekuwa na nafasi ya kutosha.
"Naiomba Serikali yetu sikivu watusaidie watupanulie jengo la watoto njiti ili na sisi tufanye kazi kwa ufanisi zaidi maana tunafanya kazi kwa mbanano" amesema Dkt. Stella.
Daktari huyo ameongeza kuwa changamoto nyingine inayokabili kitengo hicho ni upungufu wa watumishi hivyo anaiomba serikali kuwaongezea watumishi ili watoe huduma bora.
Dkt. huyo amesema kuwa kitengo hicho kinapokea watoto wa aina mbili wale ambao mimba ilifika miezi tisa na aina ya pili ni wale ambao wamezaliwa mimba ikiwa haijafikia miezi tisa ( Watoto Njiti).
" Huwa tunawapokea katika kitengo hiki ambacho ni kituo mama katika mkoa wa Mara. Kwa maana hiyo watoto wote wanaozaliwa ndani ya mkoa wa Mara wale ambao wanachangamoto kwenye vituo walikozaliwa na ikaonekana hawawezi kuwahudumia, basi wote wanaletwa katika hospitali hii kuweza kupata huduma za viwango vya juu " amesema Dkt. Stella.
Akizungumza kuhusu vifaa katika kitengo cha watoto wachanga, Dkt.Stella ameipongeza Serikali kwa kuipatia hospitali hiyo vifaa vya kisasa na vya kutosha kuweza kuwahudumia watoto njiti.
Wanawake wakiwa wamewasili hospitali ya rufaa mkoa wa Mara kuwajulia hali wazazi wodi ya mama na mtoto
" Tunaipongeza sana Serikali yetu imetupatia vifaa vya kisasa vinavyotoa huduma kwa watoto njiti, kwakweli kwenye vifaa hatuna changamoto, tunaamini serikali yetu sikivu itatutatulia hizo changamoto zingine ili tutoe huduma bora na kufanya kazi nzuri zaidi kama inavyoleta vifaa vya kisasa" amesema Dkt. Stella.
Dkt. Stella amewakaribisha wana Mara kufika katika hospitali hiyo kwakuwa ina Daktari bingwa mbobezi katika magonjwa au maswala ya watoto.
"Mtoto akipata tatizo mlete kwa wakati usikae nae huko, wengine wanakaa nao huko kisha wanatuletea watoto wameshachoka. Pale unapowahi inakuwa ni rahisi kumsaidia mtoto kurudi katika hali yake ya kawaida " amesema.
Daktari Kiongozi Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara0 Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dkt. Osmundi Dyegura amesema tayali Serikali imeshaona changamoto hiyo ya ufinyu wa chumba na inatarajia kujenga jengo la mama na mtoto litakalosaidia kuondoa changamoto hiyo wodi ya watoto njiti.
Daktari Kiongozi Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dkt. Osmundi Dyegura (wa tatu kushoto) akizungumza na wanawake kutoka shirika la Health & Safe Delivery Baby Foundation (HSF) na Shirika la Power Life Health & Wealth walipofika kutembelea wodi ya mama na mtoto
Post a Comment