HEADER AD

HEADER AD

HALMASHAURI YA MASWA YAPONGEZWA KWA UTEKELEZAJI MIRADI YA KIMKAKATI


Na Samwel Mwanga, Maswa

HALMASHAURI ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imepongezwa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) kwa utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kutengeneza chaki na kuzitaka halmashauri nyingine kuiga mfano huo.

Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Stanslaus Mabula (Mb)Machi, 26 mwaka huu wamefanya ziara ya ukaguzi wa miradi miwili ya maendeleo ambayo imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa katika halmashauri hiyo ikiwemo Ujenzi wa kiwanda cha Chaki na Jengo la wagonjwa wa dharura katika Hospitali ya wilaya hiyo.

Kamati ya LAAC imetoa pongezi kwa Madiwani pamoja na wataalam kwa kubuni wazo zuri la kuanzisha mradi wa kimkakati wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha Chaki ambacho kitakuwa ni chanzo  cha mapato ya halmashauri hiyo na pia kitatoa fursa kwa wananchi wa wilaya hiyo kupata ajira.


Moja ya mitambo katika kiwanda cha Chaki kinachomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa

“Nami niwapongeze sana kwa ujenzi huu wa kiwanda cha Chaki huu ni moja ya mradi wa kipekee wa kimkakati na kamati mara nyingi imekuwa ikisema  halmashauri nyingi zinatamani kujenga stendi,masoko na vitu vingine vya namna hiyo lakini halmashauri ya wilaya ya Maswa kulingana na eneo lenu lilivyo, kulingana na malighafi ambayo mnaweza kuipata maeneo jirani mmebuni mradi mzuri sana wa kiwanda hiki,”

“Mradi ni mzuri sana na kamati inapenda kutoa wito kwa halmashauri zote nchini kupitia halmashauri ya wilaya ya Maswa kuwa wabunifu na kufikiria miradi mbadala ambayo itakuwa na uzalishaji bora itakayokuwa inatoa ajira na siyo ajira siyo za ndani tu hata nje kutokana na kuwawasaidia wengine na mradi huu utakapoanza mtaweza kuuza chaki nchi nzima na niendelee kusisitiza halmashauri ya wilaya ya Maswa ni mfano wa kuigwa,”amesema Stanslaus Mabula.

Wajumbe wa Kamati hiyo wametoa agizo kwa halmashauri hiyo  kuhakikisha  kiwanda hicho kinaanza uzalishaji ifikapo Mei ,15 mwaka huu ili thamani ya fedha  ya serikali iliyowekezwa katika kiwanda hicho.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wengine, Suma Fyandomo(Mb)mara baada ya kutembelea jengo la wagonjwa wa dharula katika hospitali ya wilaya hiyo amesema kuwa wameridhishwa na ujenzi wa jengo hilo ambalo thamani ya fedha imeonekana.

     Mjumbe wa Kamati ya LAAC,Suma Fyandomo (Mb)akizungumza mara baada ya kutembelea jengo la wagonjwa wa dharula katika hospitali ya wilaya ya Maswa

Amesema kuwa jambo jingine la kufurahisha ni vifaa vilivyoko kwenye jengo hilo ambavyo ni vya kisasa kwa ajili ya kumhudumia mgonjwa tofauti ya vifaa vya zamani huku akitolea mfano kuwa zamani mgonjwa alipokuwa akiongezewa hewa ya oksijeni alikuwa akilala na mtungi wa gesi kitandani lakini kwa njia ya kisasa mitungi iko chumba cha nje huku mgonjwa akiendelea kupatiwa huduma katika chumba maalum.

Aidha amewashauri wataalam wote  kutunza vifaa vilivyoko katika jengo hilo pamoja na kutunza jengo na miundombinu yake ambalo limejengwa kwa kiwango chenye ubora wa hali ya juu na linatoa taswira nzuri katika hospitali hiyo.

Awali Afisa Mipango kutoka Halmashauri ya wilaya hiyo, Ntobi Lufunga akitoa taarifa fupi ya kiwanda cha hicho kwa wajumbe hao, amesema kuwa katika kipindi cha bajeti ya mwaka 2018/2019 halmashauri ya wilaya ya Maswa ilikuwa ni miongoni mwa halmashauri 17 hapa nchini ambayo ilipatiwa fedha.

     Afisa Mipango halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Ntobi Lufunga(kushoto)akitoa taarifa ya kiwanda Cha Chaki kwa wajumbe wa LAAC

Fedha hizo ni kwa ajili ya kuendesha miradi ya kimkakati na wanatekeleza miradi miwili ukiwemo wa kiwanda cha chaki na kiwanda cha vifungashio na hadi sasa kiwanda hicho cha Chaki kimetumia gharama ya Shilingi Bilioni 10.16 hadi sasa.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa, Dr James Bwire amesema kuwa  jengo hilo la dharula kwa wagonjwa katika hospitali hiyo lilikamilika ujenzi wake mwaka Mwezi Julai mwaka 2021 na likaanza kutoa huduma Mwezi Machi mwaka 2022 baada ya vifaa vyote kukamilika vinavyotakiwa katika katika jengo hilo.

   Dk,James Bwire wa Hospitali ya wilaya ya Maswa,(mwenye koti jeupe)akitoa maelezo ya Vifaa katika jengo la wagonjwa wa dharula kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya LAAC

Amesema kuwa jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia wagonjwa wa dharula 450 kwa mwaka lakini tangu lianzishwe hadi sasa limeweza kuhudumia wagonjwa 587 sawa na wagonjwa 54 wa dharula kwa mwezi na jengo hilo limekuwa msaada kwao kutokana na kuwa na vifaa vya kisasa.

Amesema limewapunguzia gharama ya kusafirisha wagonjwa kwenda hospitali ya rufaa ya Bugando kwani kwa sasa wanapatiwa matibabu hapohapo na wataalam wamewezeshwa kwa ajili ya kutoa matibabu hayo.

     Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Maswa,Dk James Bwire(kushoto)akisoma taarifa ya jengo la wagonjwa wa dharula kwa Makamu Mwenyekiti Kamati ya LAAC,Mbunge Stanslaus Mabula(wa kwanza kulia, ).

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Paul Maige ametoa shukrani za dhati kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha halmashauri hiyo kuipatia fedha za miradi mbalimbali ikiwemo miradi hiyo ambayo imetembelewa na wajumbe wa kamati hiyo.

Nichukue fursa hii kumpongeza RaisWa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuletea fedha nyingi katika halmashauri yetu ambayo tunatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo hii miradi ambayo imetembelewa na kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa,” amesema

Mwonekano wa mbele wa jengo la wagonjwa wa dharula katika hospitali ya Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu lililotembelewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC)

"Nichukue fursa hii kumpongeza RaisWa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuletea fedha nyingi katika halmashauri yetu ambayo tunatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo hii miradi ambayo imetembelewa na kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa,” amesema.

      Makamu Mkt wa Kamati ya LAAC, Stanslaus Mabula(Mb)akizungumza katika kikao Cha majumuisho baada ya kumaliza ziara ya kutembelea miradi katika halmashauri ya Wilaya ya Maswa.


  Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC,Mbunge,Stanslaus Mabula(aliye kati mbele)akizungumza na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Paul Maige(wa pili kulia)mara baada ya kukagua jengo la wagonjwa wa dharula ktk Hospitali ya wilaya ya Maswa.

No comments