IDARA YA MAENDELEO YA JAMII TARIME MJI YASAJILI VIKUNDI 457
Na Dinna Maningo, Tarime
AFISA Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara, Vitus Gwanko amesema kuwa Serikali imekuwa ikiviwezesha vikundi ili kujikuza kiuchumi ambapo hadi sasa vikundi 457 vimesajiliwa.
Akizungumza hivi karibuni katika madhimisho ya kuelekea siku ya wanawake Duniani ambapo halmshauri ya mji wa Tarime kwa kushirikiana na baadhi ya wanawake wa Tarime mjini wakiongizwa na kamti ya maandalizi chini ya mwenyekiti wa kamati, Noellah Gachuma waliadhimisha katika Kata ya Ketare.
Aliyesimama ni AFISA Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara, Vitus Gwanko, Diwani wa Kata ya Ketare Daud Wangwe (katikati), na Noellah Gachuma.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika Machi, 5, 2024, yalienda sambamba na utoaji wa misaada ya vitu kwa wajane 20 ambapo kila mmoja alipata mafuta ya kula, unga wa ngano, sukari, sabuni, shuka mbili na mchele vyenye jumla ya Tsh. Milioni 2.5 vilivyochangwa na wadau mbalimbali pamoja na kamati ya maandalizi.
Vitus amesema kuwa Machi, 8 ya kila mwaka Dunia huadhimisha siku ya wanawake duniani ambapo kabla ya tarehe hiyo halmashauri hiyo iliadhimisha Machi, 5, 2024 katika Kata hiyo.
Amezitaja kazi zilizofanyika kwa wanawake wa halmashauri hiyo katika kuharakisha maendeleo kuwa ni pamoja na uhamasishaji wa maendeleo kwa vikundi vya huduma ndogondogo vya fedha ili kuwajengea uwezo wa kuweka hisa na kukopa kwa lengo la kupata mtaji wa kuanzisha biashara.
"Kama halmashauri imeenda sambamba na kauli mbiu ya siku ya mwanamke"Wekeza kwa mwanamke kuharakisha maendeleo ya Taifa na ustawi wa Jamii''. na kuwezesha vikundi 457 vilivyoweza kusajiliwa ambapo kati ya hivyo 40 vinatoka katika Kata hii ya Ketare.
" Halmashauri imesaidia vikundi mbalimbali kufikia malengo yao, baadhi ya vikundi vilipewa elimu ya utengenezaji wa sabuni za miche, mafuta ya kupikia, sabuni za maji na utengenezaji wa batiki ambapo katika halmashauri ya mji vikundi 10 vilipewa mafunzo hayo na shirika la VETA Bukoba" amesema Vitus.
Amesema Divisheni ya maendeleo ya jamii inaendelea kutoa elimu kwa wanawake ili waendelee kujiunga na vikundi vya kijamii ili kuendana sambamba na kauli mbiu ya wekeza kwa mwanamke kuharakisha maendeleo kwa taifa na ustawi wa jamii.
Vitus amewashukuru wanawake wote ambao wameweza kushiriki maadhimisho katika ngazi ya halmshauri ambapo kimkoa yanafanyika leo Machi, 8, wilayani Bunda.
Noellah Gachuma aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi amesema kuwa Idara ya maendeleo ya jamii inapata changamoto kubwa kutokana na baadhi ya vikundi kutorejesha kwa wakati fedha za mikopo.
"Watu wanakopa mikopo lakini wanashindwa kurejesha, shida kubwa ni namna ya kukopeshana, mfano maendeleo ya jamii inakopesha Tsh. Milioni 10 kikundi kina watu 5, sasa wale watu kwa sababu wanataka usawa watu wanapewa Milioni mbilimbili.
"Na kwenye kikundi watu hawalingani biashara unakuta yule mwenye biashara ya chini anashindwa kurejesha mkopo kwahiyo anakwamisha wengine" amesema Noellah.
Amewaomba wanawake kukopa fedha kwa maendeleo, wasikope kwasababu tu anastahili kukopeshwa na wakope mikopo ambayo wana uwezo wa kuirejesha.
Post a Comment