HEADER AD

HEADER AD

DC RORYA AANZISHA KAMPENI YA NG'OMBE ZIZINI


>>Apiga marufuku ng'ombe kuzurura 

>> Aagiza wasiokuwa na mazizi salama washughulikiwe

>> OCD Utegi asema amepokea agizo atalitekeleza

Na Dinna Maningo Rorya

MKUU wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Juma Chikoka ameanzisha kampeni ya ng'ombe zizini inayomtaka mtu yeyote mwenye mifugo kuhakikisha anakuwa na zizi salama ama kuhifadhi mifugo kwenye mazizi ya pamoja.

Akizungumza wakati akipokea msaada wa madawati 180 kutoka kwa mjumbe wa mkutano mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Sango Kasera Gungu , katika kijiji cha Utegi Machi, 29 , 2024 , amesema kampeni hiyo ni amri yake inayolenga kuhakikisha mifugo inahifadhiwa kwa usalama.

       Mkuu wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Juma Chikoka

Mkuu huyo wa wilaya ametoa amri kwa maafisa watendaji , maafisa tarafa na Polisi kuhakikisha wanawashughulikia wafugaji wasiokuwa na mazizi salama pamoja na wanaoacha mifugo yao kulandalanda ovyo mitaani.

"Nimekuja rasmi na kampeni hii  ya ng'ombe zizini , hii inakwenda kuweka amri ya mkuu wa wilaya kwamba mtu yeyote anayefuga ni lazima ajue wapi anapohifadhi mifugo yake.

"Ni marufuku ng'ombe kuzurura kiholela. Tumeruhusu mazizi salama na mazizi ya pamoja yanayoonesha usalama wa mifugo upo wa kutosha. Nahitaji jeshi la Polisi likipita kufanya doria linajua leo tupite kitongoji hiki kina zizi hili, kwasababu linafanya doria kutokana na jiografia ya mahali husika" amesema DC Chikoka.

Amesema kuwa wapo wakaidi ambao hawataki kuhifadhi ng'ombe kwenye mazizi ya pamoja hivyo anawahimiza wawe na mazizi yao nyumbani ambayo ni salama.

" Ukikaidi onesha zizi lako ambalo ni salama maana kampeni inasema ng'ombe zizini, kila mfugaji ni lazima kuonesha ni wapi unapohifadhi mifugo yake.

"Nimeshawapa nguvu maafisa tarafa na watendaji, nitakwenda tarafa zote. Naomba viongozi wakiwamo jeshi la Polisi yeyote ambaye mtakuta ng'ombe wake wanazagaazagaa huyo ameamua kuwavutia wahalifu hivyo washughulikiwe" amesema.

Amessma Kampeni ya ng'ombe zizini imelenga kuhakikisha inatokomeza wizi wa mifugo " Nilimwambia mkuu wa mkoa nakwenda na hii kampeni, najua yapo malalamiko yatakufikia, yakikufikia jua kijana wako nakwenda na hii kampeni na yeye akaniambia songa mbele.

"Na mimi nawahakikishia nasonga mbele na hiyo kampeni kwa maslahi mapana ya mifugo ya wanarorya, lengo kuona wanarorya mifugo yao ikiwa salama na wakifuga vizuri itawapa maendeleo " amesema Chikoka.

Mkuu wa Polisi wilaya ya kipolisi Utegi, SSP Festo Ukulule amesema ameipokea Kampeni hiyo ya ng'ombe zizini na ataitekeleza kuhakikisha kila mfugaji anaonesha zizi na liwe zizi salama.

       Mkuu wa Polisi wilaya ya kipolisi Utegi, SSP Festo Ukulule.

"Kampeni ya mazizi salama mazizi ya pamoja na kauli mbiu ya ng'ombe ni zizi mimi nimeipokea kwa asilimia 100 kwa utekelezaji" amesema.

Ameongeza kuwa wilaya ya Rorya kuna watu wanalaza ng'ombe nje kwa kuzifunga kamba na imekuwa ni mazoea hali inayosababisha kuibwa.



No comments