HEADER AD

HEADER AD

FEDHA ZA MFUKO WA JIMBO KUSAIDIA VIJIJI VINNE KUKAMILISHA UJENZI WA ZAHANATI

>>Vifaa vya Milioni 30 vyanunuliwa 

>>Mbunge Maswa Magharibi asema ni moja ya vipaumbele vya wanakijiji.


Na Samwel Mwanga, Maswa

MBUNGE wa Jimbo la Maswa Magharibi wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu, Mashimba Ndaki amekabidhi vifaa vya ujenzi  vyenye thamani ya Tsh Milioni 30 vilivyonunuliwa kwa fedha za mfuko wa jimbo.

Lengo ni kuunga mkono juhudi za wananchi wa vijiji vya Mandela, Malekano, Ilobi na Kulimi katika ujenzi wa zahanati.

      Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Mandela wilayani Maswa.

Katika ziara ya kikazi aliyoifanya Machi 30 mwaka huu kwa nyakati tofauti katika vijiji hivyo mbunge huyo amekabidhi mifuko ya saruji, mbao, na mabati ili kusaidia nguvu za wananchi walioanzisha ujenzi huo, nia ikiwa ni kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa karibu kwenye maeneo yao.

Akizungumza na wananchi katika kijiji cha Mandela kilichoko Kata ya Sengwa amesema kuwa aliwahaidi wananchi wa kijiji hicho kuwa pindi watakapomaliza ujenzi wa boma katika zahanati yao atahakikisha kazi ya kuezeka ataifanya ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada zao walizozifanya katika ujenzi huo.

       Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akikabidhi sehemu ya mbao ambazo kuchangia ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Mandela.

“Nilipofika hapa katika kijiji chenu mliniambia moja ya vipaumbele vyenu mnahitaji kuwa na zahanati ya kijiji na tulikubaliana ya kuwa ninyi mjenge boma halafu mkimaliza mniachie kazi mimi ya kuezeka.

" Nimekuja na bati zote, mbao zote, misumali yote na waya za kenchi vifaa hivi vyote vina thamani ya Sh 11,730,000/- hivyo niombe uongozi wa serikali ya kijiji msimamie na vitumike kama vilivyokusudiwa,”amesema.

Mbunge Mashimba akiwa katika kijiji cha Malekano katika Kata ya Kadoto alizungumza na wananchi na kabidhi mifuko 150 ya saruji yenye thamani ya Sh 3,600,000 ili kusaidia ujenzi wa boma la zahanati ya kijiji hicho.

     Sehemu ya saruji mifuko 100 iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki kuchangia ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Ilobi wilayani Maswa.

Pia katika kijiji cha Ilobi kilichoko Kata ya Jija aliukabidhi uongozi wa kijiji hicho mifuko 100 ya saruji  yenye thamani ya Tsh. 2,400,000 ili kuunga mkono jitihada zao za kujenga zahanati.

“Naomba mifuko hii ya saruji niliyoikabidhi ajili ya kusaidia ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Ilobi na kijiji Malekano itumike kama ilivyokusudia ili tuweze kuendelea kusaidia na kuhakikisha hizi zahanati zinakamilika nah ii ndiyo kazi ya mbunge na siyo maneno maneno,”amesema.

Katika kijiji cha Kulimi kilichoko katika Kata ya Kulimi mbunge huyo alikabidhi mabati, mbao, misumari na waya za kenchi vifaa vyote vikiwa na thamani ya Tsh 11,224,000 huku akisisitiza iwapo vifaa hivyo vitabaki baada ya kazi ya kuezeka kumalizika hivyo vitumike katika ujenzi wa nyumba ya Mganga wa zahanati hiyo itakayojengwa siku za usoni.

   Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki(wa pili kulia)akikabidhi Moja ya bati ikiwa ni sehemu ya Mabati aliyotoa kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa zahanati ya Mandela wilayani Maswa

Amesema kuwa vifaa hivyo vyote vimenunuliwa kupitia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo na kwa kipindi hiki aliona ni vizuri kuelekeza fedha yote ya mfuko huo kwa ajili ya kuhakikisha anasaidia ujenzi wa zahanati hizo kwani wananchi wasipopata matibabu afya zao zitadhoofika na nguvu kazi ya taifa itapungua.

“Binafsi nataka siku mkisema sasa umetosha kututumikia nipumzike na ubunge niwe nimeacha alama yangu katika kila kijiji cha jimbo hili la Maswa Magharibi na vifaa.

    Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki(aliye kati)akikabidhi Mfuko mmoja wa saruji ikiwa ni sehemu ya mifuko 150 ya saruji aliyotoa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Malekano.

" Vifaa hivi vyote ambavyo nimevitoa katika vijiji vinne vimetokana na fedha za mfuko wa maendeleo wa jimbo na kwa kipindi hiki nilielekeza fedha hizi niwasaidie wananchi walionyesha jitihada katika ujenzi wa zahanati kupitia nguvu zao mwenyewe, ”amesema.

Aidha amesema kuwa zahanati hizo zitakapomalizika kwa kuezekwa ataubeba mzigo huo tena ili kuhakikisha ya kuwa zinakamilika na zinaanza kutumika na wananchi wanapata huduma ya matibabu kwenye zahanati ambazo walianzisha ujenzi wao wenyewe.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Ndila Mayeka ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kadoto pamoja na kumshukuru mbunge huyo kwa kutoa vifaa hivyo kwa kupitia fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo amempongeza kwa juhudi zake ambazo anazionyesha katika kuleta maendeleo katika jimbo hilo kupitia sekta mbalimbali.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Ndila Mayeka akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Malekano wakati wa Mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki

“Kwa kweli mbunge umetushika mkono katika shughuli hizi za ujenzi wa zahanati kwa kweli tunakushukuru sana na tangu umeingia madarakani na kuwa mbunge wa jimbo hili sasa kipindi cha pili umefanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo na yanaonekana kwa macho katika sekta mbalimbali kwa kweli umeweka alama ya maendeleo katika kila eneo la jimbo letu la Maswa Magharibi,”amesema.

  Sehemu ya Wananchi wa Kijiji cha Kulimi waliojitokeza kumsikiliza Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki (hayuko pichani)

No comments