HEADER AD

HEADER AD

DC RORYA ASEMA RORYA ITAJENGWA NA WANARORYA, AMPONGEZA SANGO KWA MSAADA WA MADAWATI

>> Asema hawezi kukataa misaada

>>Ded awakaribisha wadau kuchangia maendeleo Rorya

>>Sango Kasera asema hadi sasa ametoa madawati 510.

>>Asema lengo ni kuzifikia kata zote 26

Na Dinna Maningo, Rorya

MKUU wa wilaya ya Rorya, mkoani Mara, Juma Chikoka amesema kuwa Rorya itajengwa na wanarorya na kwamba hawezi kukataa misaada inayotolewa na wadau wa maendeleo.

Amesema kuwa Serikali peke yake haiwezi kufanya mambo yote ya maendeleo, hivyo wadau,wahisani mbalimbali wa maendeleo wana haja ya kusaidia maendeleo Rorya.

Dc Chikoka ameyasema hayo Machi, 29, 2024, katika senta ya Utegi, Kata ya Koryo wakati akipokea madawati 180 yaliyotolewa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi ( CCM), Sango Kasera Gungu kwa ajili ya shule za msingi zilizopo Kata ya Ikoma, Kirogo na Komuge.

      Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Utegi wakati akipokea madawati ya msaada  180 yaliyotolewa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa Sango Kasera.

" Serikali peke yake haiwezi kufanya haya mambo lazima wadau, wahisani, watu wa maendeleo kuweza kusaidia pale ambapo Dk. Samia anafanya. Tumeendelea kupokea misaada kutoka kwa wadau mbalimbali.

"Mimi, mkurugenzi na timu ya serikali tulipokea msaada kutoka taasisi ya NMB ambapo walitoa misaada takribani Tsh. Milioni 87, walitoa mabati, simenti na kuna eneo wamejenga bweni, hayo ndio mambo tunayoyahitaji. CRDB nao walitoa misaada na wahisani wengine wameendelea kutoa misaada mbalimbali hayo ndiyo mambo tunatamani kuona. 

Ameongeza kusema " Juzijuzi tu alhamis iliyopita mimi mwenyewe kuna wadau walioungana walileta vitanda 26 vya dabodeka sawa na vitanda 52, wakatatua changamoto ya vitanda Bweni la Nyathorogo ambapo watoto wengi wamekuwa wakitembea umbali mrefu hali iliyosababisha mimba za utotoni, na shule hiyo ni miongoni mwa shule zilizokuwa hazifanyi vizuri " amesema DC Chikoka.

        Sango Kasera wa pili kulia akiwakabidhi madawati, Mkuu wa wilaya ya Rorya wa pili kushoto,  Mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya Rorya (wa kwanza kushoto), na afisa elimu msingi aliyevaa kitenge.

DC Chikoka amempongeza Sango Kasera kwa msaada wa madawati huku akiwakaribisha wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali kuleta maendeleo Rorya.

" Naendelea kukaribisha wahisani mbalimbali na ndiyo maana nilipopata taarifa yupo muhisani mjumbe wa mkutano mkuu Taifa Sango Kasera anafanya jambo lake mimi nilisema jambo hili lisiende kimya kimya liletwe kwa serikali ili lipate baraka ya Serikali.

"Nitumie fursa hii kumpongeza Sango na wadau mbalimbali, kama alivyosema mkurugenzi uhitaji wa madawati bado unahitajika. Rorya itajengwa na wanarorya, turudi nyumbani tuungane tuwe na kauli moja ya kutatua changamoto za wanarorya ili Rorya iendelee kusonga mbele" amesema Chikoka.

Amesema Rorya anayoitaka yeye ni Rorya ya maendeleo " Rorya ninayoitaka kama mkuu wa wilaya nataka tuifanye iwe kanda maalum ya maendeleo na hili linawezekana, lakini haliwezekani kwa mtu mmoja wote tukiungana tukazungumza lugha moja itawezekana " amesema Chikoka.

     Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka na viongozi wengine pamoja na baadhi ya wananchi wakiwa wameketi kwenye madawati  yaliyotolewa na Sango Kasera baada ya kuyakabidhi serikalini

DC Chikoka amesema pamoja na misaada hiyo lazima kuwe na utaratibu wa utoaji wa misaada ambapo wadau wote wa maendeleo ambao wataenda kugusa taasisi yoyote ya serikali kama vile shule, Zahanati, Hïospitali lazima serikali itambue msaada huo  na upitie ofisi ya mkuu wa wilaya.

"Ukifika kwa mkuu wa wilaya mimi na mkurugenzi tutaangalia uhitaji upo kwenye maeneo gani , mkurugenzi ndio anayeendesha taasisi zote, tukishapokea tunapeleka pale ambapo inahitajika , sio kupita kimyakimya. Akipita kimyakimya mimi nikasema huyo asimame mimi nitakuwa na lawama?.

"Jambo liwe rasmi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya. Na mimi niseme kamwe sitakuwa katika ofisi hii nikaona kuna msaada ambao unawagusa wanarorya, unawagusa watoto wetu wa Rorya alafu nikaukataa kamwe haitawezekana, jambo la msingi utaratibu ufuatwe, lazima ofisi ijue "amesema DC Chikoka.

Chikoka amesema wamepokea madawati hayo ambapo amemtaka Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Rorya Abdul Mtaka kutengeneza utaratibu mzuri kupitia kwa afisa elimu kisha kwa afisa elimu Kata kwenye maeneo misaada itakakokwenda.

       Viongozi wakifurahia baada ya kupokea madawati yaliyotolewa na Sango Kasera

Tunatarajia kuona viongozi wa serikali ndio wakiwa kinara kupokea na kukabidhi walimu kwenye hayo maeneo , kwahiyo mdau utashirikiana na afisa elimu kata ambazo madawati yanaenda kuhakikisha misaada hiyo inawafikia na kuendelea kuwa salama" amesema Dc Chikoka.

Pia mkuu huyo wa wilaya amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za maendeleo katika wilaya hiyo ambapo Tsh. Bilioni 3.6 zimetolewa kujenga miundombinu ya elimu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, Abdul Mtaka amesema halmashauri hiyo ina changamoto ya uhaba wa madawati katika shule za msingi pamoja na viti na meza katika shule za sekondari.


Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, Abdul Mtaka akizungumza na wananchi wakati wa kupokea madawati 180 yaliyotolewa na Sango Kasera

" Kwa juhudi za Serikali pamoja na halmashauri tumefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha tunapunguza hii changamoto ya madawati shule za msingi pamoja na viti na meza shule za sekondari.

"Kwenye bajeti ya mwaka 2024- 2025 tumetenga fedha Tsh. Milioni 170 kwa ajili ya madawati kwa shule za msingi na viti na meza kwa sekondari. Jitihada hizi za serikali haziwezi kukamilisha kutatua hili tatizo kwa asilimia 100 kwamba fedha hizo zitamaliza tatizo la madawati, viti na meza shule zote.

      Baadhi ya wananchi wakiwasikiliza viongozi wakati walipofika kijiji cha Utegi kupokea madawati yaliyogolewa na Sangi Kasera

"Tunafanya kwa kiasi fulani, tunashukuru kwa hiki ambacho amekifanya Sango tunampongeza sana. Nitoe wito kwa wadau wengine ambao wapo tayari kutusaidia watusaidie, wanapofanya hivyo wanaisaidia serikali lakini pia wanaisaidia jamii yetu ya wanarorya" amesema Abdul.

Ameongeza kuwa wadau wakipatikana wengi au watoto wakaelimishwa wakapata elimu na wenyewe watakuwa wadau ambao watakuja kuchangia maendeleo . 

      Wananchi wakitazama madawati yaliyotolewa na Sango Kasera

Amesema Halmashauri itatoa ushirikiano kadri watakavyoweza kukamilisha zoezi hilo ili changamoto isiwepo kwenye wilaya hiyo.

Mjumbe wa Mkutano mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi, ( CCM) Sango Kasera Gungu amemshukuru mkuu wa wilaya hiyo, Mkurugenzi wa halamshauri na wakuu wa Idara kwa kubariki zoezi lake la utoaji wa madawati katika shule za msingi na kusema kwamba madawati 180 ni kati ya madawati 510 ambayo ameyatoa katika baadhi ya Kata wilayani humo.

 Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka (kushoto) akisalimiana na Sango Kasera baada ya kupokea madawati.

"Nashukuru mkuu wa wilaya, mkurugenzi na wakuu wa idara kwa kubariki hili zoezi langu la utoaji wa madawati kwa shule za msingi. Wilaya yetu ina chagamoto nyingi, tunazo shule za msingi zaidi ya 132 , wanafunzi wengi wanakaa chini .

" Baada ya kupokea maombi mbalimbali nimeona angalau kwa kile nilichonacho kidogo nitoe, marafiki zangu akiwemo Airo na Ochele nilipowaomba sapoti wamenisapoti. Zoezi hili lilianza rasmi tarehe 9 na kata baadhi ikiwemo kata ya Bukura Bukwe, Koryo na Nyathorogo zimepata madawati.

"Madawati haya 180 katika awamu hii yataenda kata ya Ikoma, Kirogo na Kata ya Komuge kila kata itapata madawati 60 ambapo jumla ya madawati yote ni 510, kila dawati wanakaa wanafunzi watatu ambapo kwa madawati 510 ni sawa na wanafunzi 1,530 wameweza kukaa kwenye madawati.

Baadhi ya madawati yaliyotolewa na Sango Kasera na kupokelewa na mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka

"Hayo ya mbeleni mwenyezi Mungu ndiye anajua hatujui kesho yake , kutokujua kesho yetu haituzuii sisi kushiriki maendeleo. Bado tuna upungufu wa madawati mengi.

" Tunaomba watu waje watusaidie Zahanati zetu zina changamoto nyingi tushirikiane na wadau wengine ambao wapo nje tuweze kusambaza vitanda kwenye Zahanati mbalimbali na hata kwenye sekta mbalimbali .

Amesema si vyema kuiachia serikali pekee ifanye kila kitu kwani haiwezi kufanya kila kitu peke yake na kwamba Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inaruhusu wadau kushirikiana na Serikali kuchangia maendeleo hivyo wadau washirikiane na serikali kuiletea Rorya maendeleo.

Diwani wa Kata ya Koryo Ores Simba amewashukuru wadau wote wa maendeleo wanaoelewa kwamba rorya inahitaji maendeleo ili kumsaidia Rais Samia kuhakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa.

    Diwani wa Kata ya Koryo Ores Simba akizungumza na wananchi wakati wa kupokea madawati

Wakati huohuo, Mkuu huyo wa wilaya amewapongeza wazazi, walimu na halmashauri kwa wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani ambapo katika mkoa wa Mara wilaya ya Rorya imekuwa ya pili  ikitanguliwa na wilaya ya Musoma.

Amesisitiza wazazi kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni. Hata hivyo amesikitishwa kwa kitendo cha wanafunzi kuanza kidato cha kwanza wakiwa wengi lakini wanapohitimu kidato cha nne idadi inapungua.
















No comments