HEADER AD

HEADER AD

SHIRIKA LA HSF, POWER LIFE WATEMBELEA WODI YA MAMA NA MTOTO HOSPITALI YA RUFAA MARA

Na Dinna Maningo, Musoma

DUNIA huadhimisha siku ya wanawake duniani kila tarehe, 8 ya kila mwaka , ukiwa ni utekelezaji wa azimio la umoja wa mataifa la mwaka 1977 ambalo lilizitaka nchi wanachama kuadhimisha siku hii kwa lengo la kuenzi mchango wa mwanamke kwenye ujenzi wa Taifa.

Chimbuko la siku hii ni jitihada za wanawake wafanyakazi wa sekta ya Viwanda nchini Marekani ambao mwaka 1911 walifanya maandamano ya kupinga mazingira duni ya kazi.


Mazingira hayo ni kama vile ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira ikiwemo wanawake kulipwa mshahara mdogo kwa kazi sawa na ile ya wanaume.

Uamuzi wa umoja wa mataifa wa kuanzisha siku ya wanawake duniani ulitokana na kwamba masuala ya haki, maendeleo na usawa wa kijinsia yalihitaji msukumo maalum na wa kipekee kutoka ndani ya jamii husika.


Tanzania ilianza kuadhimisha siku ya wanawake Duniani mwaka 1997 ambapo kufikia mwaka 2005 Serikali ilifanya maamuzi kuwa, maadhimisho hayo yafanyike kila mwaka ngazi ya mkoa.

Pia yale  ya kitaifa yafanyike kila baada ya miaka mitano kwa lengo la kutoa muda wa utekelezaji wa maazimio na kupima hatua za mafanikio yaliyofikiwa kitaifa.


Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani inasema " Wekeza kwa mwanamke kuharakisha maendeleo ya taifa kwa ustawi wa jamii".

Katika kuadhimisha siku ya wanawake Duniani Shirika la Health & Safe Delivery Baby Foundation (HSF) lililopo Nyamongo linalojihusisha na maswala ya mama na mtoto lililoanzishwa na Mwanamke ambaye ni Mkurugenzi wa shirika hilo, Emmyliana Julius Range limetoa msaada katika wodi ya mama na mtoto hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.


Shirika hilo kwa kushirikiana Mwanamke mwenzake Mkurugenzi na mwanzilishi wa Shirika la Power Life linalojihusisha na masuala ya kuelimisha afya na uchumi kwa wanawake na vijana, Mariam Selemani wakiwa wameongozana na wanawake wenzao wametoa msaada kwa wajawazito na wanaosubiri kujifungua kwa kuwapaa sabuni, kanga za kujistili,  majani ya chai ya tiba na taulo za kike.

Akizungumzia afya ya mama na mtoto Mkurugenzi Emmyliana anasema serikali inafanya kazi kubwa kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinapungua, hivyo basi katika kuunga juhudi za serikali wao kama HSF wanaunga juhudi za serikali kuhakikisha wanatoa elimu kusaidia wanawake katika kuhakikisha vifo ya mama na mtoto vinapungua na msaada.

    Mkurugenzi shirika la HSF Emmyliana Julius Range akimpatia mzazi msaada

"Tupo hapa Kwangwa sisi kama wadau wa mama na mtoto, tumekuja kuongea nao, pia kutoa elimu ya unyonyeshaji wa mtoto. Tunaelimisha akina mama kuhudhulia mapema kliniki pale tu wanapokuwa wajawazito.

" Siku ya wanawake tumekutana kujua changamoto zinazowakabili wodi ya mama na mtoto, wagonjwa lakini pia wauguzi ili sisi kama wadau tuweze kuangalia namna ya kushirikiana na serikali ili kuweza kupunguza changamoto hizo" anasema Emmyliana.

Mkurugenzi wa Shirika la Power Life Mariam Selemani, anasema taasisi yake imejikita kumsaidia mama kiafya na kiuchumi.

       Mkurugenzi na mwanzilishi wa Shirika la Power Life Mariam Selemani

" Leo hii tumefika hapa katika hospitali hii kama wadau wa maendeleo kuwaona wanawake wenzetu katika wiki ya wanawake, tuko Nyamongo tunaendelea na maonesho ya bidhaa na utoaji elimu ya afya kwa siku 14.

"Kuwa mwanamke ni jambo jema sana kwasababu bila mwanamke hakuna taifa, kwahiyo tunaamini kabisa ukimwinua mwanamke ukamwelimisha, kumpongeza ni jambo kubwa katika jamii" anasema Mariam.

Ghati Magige mkazi wa Kata ya Nyamwaga wilayani Tarime ambaye alipata rufaa kwenda hospitali ya rufaa anasema anamshukuru Mungu kwa kujifungua salama.

         Mkurugenzi Emmyliana akimjulia hali mzazi aliyejifungua mtoto

" Mimi ni mama wa watoto wawili nina miaka 21, natokea Tarime nilikuwa mjamzito nikaletwa hapa kujifungua, nimefanyiwa upasuaji. Namshukuru Mungu nimejifungua salama na nimehudumiwa vizuri sana.

"Tunashukuru kupata msaada wa vitu hasa kwa sisi tunaokaa muda mrefu hospitali vinatusaidia sana , tunaomba na watu wengine watoe msaada hospitali kwasababu kuna wagonjwa wengine wanakaa muda mrefu hospitali kwa ajuli ya matubabu hadi ndugu zao wanawakimbia wanabaki kuwa mzigo wa hospitali" anasema.

Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Tarime Nyamjungu Emmanuel, anayakumbusha mashirika na taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali kujitokeza kusaidia jamii kwa ukaribu ili kuangalia changamoto zinazowakabili wakina mama.

    Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Tarime Nyamjungu Emmanuel

"Tupo katika mwezi wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, basi na taasisi zingine ziguse na maeneo mengine siyo hospitali tu katika kusaidiana na serikali kuhakikisha changamoto za akina mama au jamii zinatatuliwa kwa pamoja ili kuweka jamii kuwa na usawa na kuleta maendeleo katika jamii" anasema Nyamjungu.

Daktari Kiongozi Hospitali ya mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dkt. Osmundi Dyegura anayashukuru mashirika hayo na wadau wengine kufika hospitali kuwatembea wagonjwa na kuwapa mkono wa pole.

     Daktari Kiongozi Hospitali ya mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dkt. Osmundi Dyegura

"Hii ni wiki ya maadhimisho ya siku ya  wanawake tumepokea wageni mbalimbali kutembelea wajawazito, waliojifungua na akina mama wenye matatizo mbalimbali, wamekuja kwa ajili ya kutoa faraja na misaada. Tunashukuru sana kwa kuja kuwaona wajawazito na wazazi waliojifungua " anasema.

Daktari huyo wa hospitali anaishukuru Serikali kwa ujenzi wa hospitali na kutoa vifaa tiba katika wodi ya mama na mtoto ambavyo vimesaidia kurahisisha huduma huku akiwaasa watumishi kutoa huduma zinazoendana na matarajio ya wananchi na zinazozingatia utu na thamani ya binadamu .

" Tunaishukuru serikali kwa uwekezaji huu wa ujenzi wa hospitali na vifaa mbalimbali katika maeneo ya kutolea huduma zikiwemo za dharura.

"Nawaasa watumishi wenzangu kwa uwekezaji huu ambao serikali inafanya , unakuwa unakosa maana pale ambapo huduma zinatolewa haziendani na matarajio ya wananchi ambao wanakuja kupata huduma.

Anaongeza kusema " kwahiyo niwaombe na kuwaasa huduma tunazozitoa zizingatie utu ili ziwe na staha na ziendane na taratibu na miongozo ya Wizara kuhakikisha tunatoa huduma zinazoleta hutu na thamani ya binadamu " Anasema Dkt. Osmund.










No comments