HEADER AD

HEADER AD

WATENDAJI MAUWASA WAPANDA MITI NA KUSAFISHA VYANZO VYA MAJI

Na Samwel Mwanga, Maswa

WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (MAUWASA) iliyoko katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imepanda miti na kufanya Usafi katika Vyanzo vya Maji.

Shughuli hizo zimefanyika Machi, 22 mwaka huu katika Mradi wa Maji wa Kijiji cha Mwashegeshi na kwenye mtambo wa kutibu na kuchuja Maji ulioko katika Bwawa la New Sola katika Kijiji cha Zanzui  ikiwa ni sehemu ya kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Maji mwaka huu.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa MAUWASA, Kassim Kaddo amesema kuwa katika Maadhimisho hayo wameamua kupanda miti kwenye mradi wa Maji katika Kijiji cha Mwashegeshi na kufanya usafi kwenye eneo la mtambo huo ili kuweza kutunza mazingira katika vyanzo hivyo vya maji.

   Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa MAUWASA, Kassim Kaddo akipanda mti katika eneo lilipojengwa tenki la maji katika kijiji cha Mwashegeshi wilayani humo.

Amesema kuwa ili waweze kutoa huduma bora ya maji kwa wananchi wa mji wa Maswa na Vijiji 12 pamoja na miji midogo ya Lalago, Malampaka na Sangamwalugesha ni lazima wavitunze Vyanzo hivyo vya Maji.

Amesema kuwa katika kipindi cha wiki ya maji wametoa elimu ya utunzaji wa Vyanzo vya Maji na miundombinu ya Maji ili mwananchi afahamu wajibu wake katika kutunza vyanzo hivyo vya maji.

       Tenki la kuhifadhi maji lililojengwa na Mauwasa katika kijiji cha Mwashegeshi kwa gharama ya Sh Milioni 500.

“Wakati wa wiki ya maji sisi MAUWASA tulitumia kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji kwani visipotunzwa tunaweza kukosa maji kabisa ambayo ni muhimu kwa matumizi yetu ya kila siku na jambo hili tumelisisitiza sana ili tuweze kuwapatia maji ya uhakika kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyoeleza,”amesema.

Amesema kuwa pia wameamua kufika katika mradi wa maji ya bomba katika kijiji cha Mwashegeshi ambao unatekelezwa na Mamlaka hiyo kwa gharama ya Sh Milioni 500 na ambao utawanifaisha zaidi ya wananchi 9000 walioko kwenye kijiji hicho.

     Wafanyakazi wa Mauwasa wakifyeks nyasi katika eneo la mtambo wa kutibu na kuchuja Maji ulioko katika Kijiji Cha Zanzui

“Mradi huu wa maji wa Mwashegeshi ni mpya na sisi Mauwasa ndiyo tunautekeleza kwa gharama ya Tsh. Milioni 500 na hizi fedha tumepatiwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan hivyo tunamshukuru sana na tumefika hapa ili tuweze kupanda miti na hili litakuwa ni zoezi letu endelevu kwa vyanzo vyetu vya maji".

“Pia tumeamua kufanya usafi katika mtambo wetu wa kutibu na kusafisha maji ulioko katika chanzo chetu cha maji ambacho ni bwawa la New Sola(Maarufu Bwawa la Zanzui)ili tuweze kutunza na kuhifadhi hiiki chanzo cha maji,”amesema.

Naye Emanuel Jidayi ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mwashegeshi pamoja na kuishukuru serikali kwa kuweza kujenga mradi huo wa maji katika kijiji hicho amesema kuwa kwa sasa wakinama wa kijiji hicho watatumia muda wao mwingi kufanya shughuli za uzalishaji mali kutokana na maji kupatikana maeneo ya karibu katika makazi yao.

     Wafanyakazi wa Mauwasa pamoja na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mwashegeshi wakiwa wamebeba miti kabla ya kupanda kwenye eneo la tenki la maji lililojengwa katika kijiji hicho.

“Kwanza kabisa nipende kuishukuru serikali yetu kwa kutupatia fursa hii ya kupata maji ya bombani kwani wakinamama walikuwa wanatumia muda mwingi sana kufuata maji takribani kilomita nne kwenye mito.

" Walikuwa wakitoka majira ya saa kumi na moja alfajili ila kwa sasa maji yatapatikana umbali mfupi tena yatakuwa safi na salama na vitongoji vyote vitatu wa Chugambuli, Ilambamakono na Mwamanonga vitanufaika na mradi huu,” amesema.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa kijiji cha Mwashegeshi, Deus Mboi amesema kuwa mradi huo wa maji wameupokea vizuri kwani umekuwa mkombozi kwa wananchi wa kijiji hicho.

    Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwashegeshi, Deus Mboi akipanda mti wakati wa kilele cha maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji katika kijiji cha Mwashegeshi

Amesema jijiji chake hakina huduma ya maji safi na salama licha ya kuwa kipo kandokando ya bwawa la New Sola na hivyo kuhaidi kuutunza na kuitunza miti yote iliyopandwa kwenye eneo ambalo limejengwa tenki la kuhifadhi maji.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya wiki ya maji ambayo ilianza Machi 16 hadi Machi 22 inasema kuwa “Uhakika wa Maji kwa Amani na Utulivu".

 


No comments