MASWA KUNUFAIKA NA MRADI WA KUTAMBUA USAWA WA KIJINSIA
Na Samwel Mwanga, Maswa
WILAYA ya Maswa mkoa wa Simiyu inatarajia kunufaika na Mradi wa REACTS-IN ili kuhakikisha kwenye jamii kuna usawa wa kijinsia na kubadilisha mifumo ya lishe kwa wanawake, wasichana na watoto walio chini ya miaka mitano.
Hayo yameelezwa Machi 15 mwaka huu Katibu Tawala wa Wilaya ya Maswa, Athuman Kalaghe katika ukumbi wa Peace Hotel uliko mjini Maswa wakati wa Uzinduzi wa Mradi huo katika wilaya hiyo.
Katibu Tawala wilaya ya Maswa, Athuman Kalaghe (wa kwanza kulia) akipewa maelezo na mmoja wa Wajasiliamali wanaoongeza thamani ya bidhaa za Unga lishe katika ukumbi wa Peace Hotel mjini Maswa wakati wa maonyesho ya bidhaa hizo.Amesema kuwa Mradi huo ambao umejikita kutambua usawa wa Jinsia na mabadiliko ya mtazamo kwa mifumo ya kubadilisha lishe ni juhudi za pamoja inayojumuisha Nutrition International, HarvestPlus na Shirika la World Vision pamoja na wadau wao.
Amesema kuwa wakati HarvestPlus inazingatia kuimarisha afya kupitia mazao lishe, washirika hawa wamejitolea kukuza haki na hadhi ya wanawake na wasichana kwa kuongeza upatikanaji wa mazao lishe na bidhaa zake.
Kalaghe ambaye alimwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo amesema kuwa ameelezwa kuwa mradi huo utatekelezwa katika Kata 25 na Vijiji 50 katika wilaya ya Maswa kwa gharama ya dola Milioni 44 ambazo zitatoka Serikali ya Canada kupitia Global Affairs Canada(CAG)kwa kipindi cha miaka saba.
Baadhi ya Wadau wa lishe waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa REACTS-IN katika wilaya ya Maswa katika ukumbi wa Peace Hotel.Baadhi ya Wadau wa lishe waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa REACTS-IN katika wilaya ya Maswa katika ukumbi wa Peace Hotel.
“Tumekusanyika hapa na washirika wetu wa kimataifa na wa ndani chini ya mwongozo wa program ya HarvestPlus ni furaha kubwa kuwajulisha kuwa Mradi wa REACTS-IN utatekelezwa katika wilaya yetu ya Maswa ukifadhiliwa kwa dola milioni 44 na serikali ya Canada kupitia Global Affairs Canada (GAC) kwa kipindi cha miaka saba.
“Kati ya hizi dola milioni 41 zinatoka kwa serikali ya Canada, ikiashiria dhamira yao ya kuboresha maisha ya wanawake, wasichana, na watoto walio chini ya miaka mitano, HarvestPlus pamoja na washirika kama World Vision na Nutrition International, wamejitolea kwa moyo kufanya kazi pamoja nasi kufikia malengo ya mradi huu hivyo tuwape ushirikiano,”amesema.
Amesema kuwa mradi huo umekuja kwa muda muafaka kwani bado jamii ya wilaya hiyo na mkoa wa Simiyu kwa ujumla inakabiliwa na changamoto ya masuala ya lishe hasa kwa watoto chini ya miaka mitano licha ya serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt Samia Suluhu kuifanya agenda ya lishe kuwa ya kitaifa.
Aidha amesema kuwa ni muhimu pia kuzingatia kuboresha ujuzi na maarifa ya watoa huduma za afya ili kuzuia na kutibu utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano na kuhakikisha njia kamili kuelekea kushughulikia chanzo cha matatizo yanayohusiana na lishe.
Ester Simfukwe mwakilishi wa Meneja Mpango Harvest Plus, amesema kuwa malengo makuu ya mradi huo ni kushirikisha wanawake na wasichana katika uzalishaji na kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye vitamini A hasa mazao lishe yanayostahimili ukame, mazao mengi na yenye ukinzani wa magonjwa na hii italeta mabadiliko chanya kwa lishe na kuwawezesha kiuchumi.
Pia amesema kuwa mradi huo unalenga kuviwezesha vikundi vya wanawake wa ndani kutetea haki sawa katika shughuli na kiuchumi haswa kilimo na unakusudia kuvunja vizuizi vya kitamaduni vinavyoendeleza mila mbaya za kijinsia na kuimarisha mifumo ya afya kwa kuongeza upatikanaji, ufikiaji na ubora wa huduma za afya na lishe.
‘Tunapoanza safari hii ya mabadiliko, naomba tuazimie kufanya kazi kwa pamoja, tukiimarisha ushirikiano na ushirika kati ya Serikali, HarvestPlus na wadau wengine wa mradi huu kwa pamoja, tunaweza kuleta matokeo endelevu katika maisha ya wanawake, mabinti, na watoto na kujenga jamii yenye usawa na lishe bora,”amesema.
Amesema kuwa watajikita katika mazao ambayo watayaongezea thamani ambayo ni maharage lishe, mahindi lishe na viazi lishe ili kuhakikisha yanazalishwa na kutumika na jamii kwa lengo la kuboresha afya zao.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Robert Urassa amewashukuru HarvestPlus pamoja na wadau wote wa maendeleo na washirika wote kwa kujitolea kwao kushirikiana na halmashauri hiyo katika kupambana dhidi ya utapiamlo katika wilaya hiyo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Robert Urssa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa REACTS-IN katika wilaya ya Maswa katika ukumbi wa Peace Hotel.Amesema kuwa watahakikisha malengo ya Mradi huo yanafikiwa kwa kuhakikisha mazao ya Viazi lishe, Maharage lishe na Mahindi lishe yanazalishwa kwa wingi katika jamii pia watatoa msaada wa kitaalam na kiteknolojia na kusimamia kuboresha lishe ya jamiii.
“Kwa jitihada zetu za pamoja katika ya Serikali na hawa wadau wengine ambao wamekubali kushirikiana nasi katika masuala ya lishe nina amini tunakwenda kufanya mabadiliko chanya kwa jamii na vizazi vijavyo juu ya masuala ya lishe hivyo niwaombe maeneo yote ambayo mradi huu utatekelezwa kila mmoja atomize majukumu yake ili tuweze kufikia malengo ya maradi huu,”amesema.
Warsha hiyo imewashirikisha Wadau mbalimbali wa kilimo wakiwemo wasindikaji na wale wanaoongeza thamani ya mazao katika wilaya ya Maswa.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Robert Urssa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa REACTS-IN katika wilaya ya Maswa katika ukumbi wa Peace Hoteli
Post a Comment