WANAKIJIJI KYANYAMSANA WASEMA ZAHANATI IKIKAMILIKA ITASAIDIA KUPUNGUZA VIFO
>>Sango Kasera na Lameck Airo watoa mabati 82 Zahanati ya Kyanyamsana
Na Dinna Maningo, Rorya
BAADHI ya Wananchi wa Kijiji cha Kyanyamsana Kata ya Baraki wilayani Rorya mkoa wa Mara, wamesema kuwa ukosefu wa Zahanati unachangia vifo kwa wagonjwa na wajawazito kutokana na umbali mrefu wa kuifuata huduma ya Afya.
Wananchi hao , Diwani wa Kata ya Baraki Angelus Mwita pamoja na viongozi wa Chama cha Mapinduzi, Machi, 16, 2024 wakiwa katika kijiji cha Kyanyamsana walipongeza kupewa msaada wa mabati ya kuezeka Zahanati ya Kijiji.
Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Sango Kasera Gungu ametoa mabati 50 huku mbunge mstaafu Jimbo la Rorya, Lamack Airo (LAKAIRO) akitoa mabati 32 na ahadi ya Milioni moja ya saruji kwa ajili ya Zahanati.
Lameck Airo (wa tatu kulia) na viongozi wengine wakiwa wameshika bati ambayo yametolewa na Mjumbe wa mkutano mkuu Taifa, Sango Kasera (hayupo pichani)
Nyanswi Mahamba mkazi wa kijiji hicho amesema " Kijiji cha Kyanyamsana hakina zahanati akina mama tunateseka sana kufuata huduma ya afya mwendo wa zaidi ya masaa matatu kwa mguu.
"Ukosefu wa zahanati umechangia watu kupoteza maisha wakiwamo wajawazito wanaokwenda kujifungua, kwakuwa ni mbali mgonjwa anatembea umbali mrefu anachoka akifika hospitali anakuwa kazidiwa na kupoteza maisha.
" Wajawazito wengine wanajifungulia njiani wakati wakienda hospitali na wengine inawabidi wazalishwe na wakunga wa jadi nyumbani badala ya kwenda kujifungulia hospitalu" amesema Nyanswi.
Fatuma Maulid amesema ili mtu apate huduma ya jamii analazimika kutumia usafiri wa pikipiki kwa sh .10,000 kwenda Kituo cha afya Kinesi na Irengo na nyakati za usiku gharama ni sh. 20,000 na kwamba amempongeza Sango na Lameck kwa msaada huo.
"Watoto wanakufa kabla hawajafika hospitali kwasababu ya umbali wa huduma ya afya, alishawahi kufariki mjamzito alikuwa anaenda kujifungua hana pesa akatembea kwa miguu akafa wakati anakwenda hospitali."amesema.
Diwani wa Kata Baraki Angelus Mwita amesema kuwa ujenzi wa zahanati ni moja ya ahadi yake wakati wa kampeni za uchaguzi na kwamba zahanati hiyo imejengwa kwa nguvu za wananchi, Diwani na wadau mbalimbali wa maendeleo.
"Sina mfuko wa maendeleo ya Kata nyie wananchi na wadau mblimbali wa maendeleo ndio tumejenga hii zahanati kuanzia msingi hadi ilipo ni nguvu zetu. Niliahidi wakati wa uchaguzi kuwa mkinichagua lazima ntahakikisha tunakuwa na Zahanati na ushirikiano wenu umeleta matokeo mazuri.
"Jukumu kubwa la Diwani ni maendeleo , nyinyi wananchi mkishapiga kura mnaenda nyumbani kwenu hamna mshahara, mshahara wenu ni kuona maendeleo. Viongozi tunapochaguliwa ni kuhakikisha ndani ya miaka mitano tumepata maendeleo na sio kufikilia uchaguzi ujao, uchaguzi ujao ni ziada" amesema Diwani.
Katibu Mwenezi Kata ya Kyang'ombe Chacha Mtatiro amesema Lakairo ni Kamanda wa maendeleo Rorya kwani baadhi ya viongozi wakishastaafu nafasi zao huwa wanaacha kuchangia maendeleo.
Diwani Mstaafu Kata ya Baraki Emmanuel Manyama amesema Lakairo ni mtu wa watu na amewekeza kwa watu huku Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kata ya Baraki, Veronica Damas amemshukuru Sango na Airo kwa msaada walioutoa na kuwaomba wasiishie hapo kwani bado wanawahitaji.
Mbunge mstaafu Jimbo la Rorya Lameck Airo amesema" Osango aliniomba nifike hapa nimwakilishe kukabidhi mabati 50 ili zahanati hiezekwe akina mama wasiende mbali kupata huduma.
"Na mimi natoa pesa ya bando mbili za bati hapahapa na naahidi Milioni moja ya kununua Simenti, na msichoke kutusumbua pale mtakapopungukiwa simu zetu zipo tupigieni" amesema Airo.
Akizungumza kwa njia ya simu mjumbe wa mkutano mkuu Taifa, Chama cha Mapinduzi (CCM) Sango Kasera amesema kuwa yeye kama kiongozi ana wajibu wa kumsaidia Rais Samia kutatua changamoto za kimaendeleo zinazowakabili.
Pia kiongozi wa chama anaposaidia kutatua matatizo ya wananchi anakuwa ametekeleza Ilani ya chama cha Mapinduzi kuhakikisha jamii inapata maendeleo.
"Tunaomba ikiwezekana Lakairo na Sango mtusaidie kutujengea au kukarabati darasa la saba, darasa hilo ni giza halifai kutumiwa na wanafunzi ,linahitaji sakafu, madirisha na mlango" amesema Bunini.
Pia barabara inayotoka hapa kijijini kuelekea Nyamaguku ni mbaya sana ukipita msimu wa mvua ni matope tupu unachafuka tunawaomba mtusaidie kuturahisishia mawasiliano ya barabara iwe nzuri ili tunapokwenda wilayani tufike kwa urahisi" amesema Bunini.
Mkuu wa shule ya msingi Kyanyamsana Bunini Mashauri Bunini.
Diwani wa Kata Baraki Angelus Mwita
Post a Comment