MBUNGE NYONGO ATOA VIPAZA SAUTI STENDI YA MABASI MJINI MASWA
Na Samwel Mwanga, Maswa
MBUNGE wa Jimbo la Maswa Mashariki mkoani Simiyu,Stanslaus Nyongo amekabidhi vipaza sauti kwa Mawakala wa Mabasi katika Stendi ya Mabasi mjini Maswa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake kufuatia uongozi wa mawakala hao kuwasilisha ombi hilo siku za nyuma.
Akikabidhi vipaza sauti hivyo Machi 5 mwaka huu katika viwanja vya Stendi hiyo amesema kuwa ameona ni vizuri akatimiza ahadi yake ambayo aliitoa kwa Mawakala hao kufuatia ombi lililowakilishwa na uongozi wao kwa mbunge huyo.
Baadhi ya Mawakala wa mabasi katika Stendi ya Mabasi mjini Maswa wakiwa na Mamalishe katika stendi katika picha ya pamoja na Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki,Stanslaus Nyongo(mwenye shati jeupe)mara baada ya kukabidhi vipaza sauti.
Amesema kuwa vipaza sauti hivyo ni muhimu sana kwa ajili ya kutolea matangazo mbalimbali katika eneo hilo ili kuwajulisha abiria na watu wengine ambao ni watumiaji wa stendi hiyo masuala mbalimbali yanayoendelea ikiwemo muda wa mabasi kuondoka au kufika katika stendi hiyo.
“Kuna ahadi yetu ya nyuma ya kuweka vipaza sauti vya matangazo kwenye stendi yetu siku ile nakuja sikuja nazo leo nimekuja nazo ili niweze kuwakabidhi nanyi mtazitumia na mtazisimamia ninyi wenyewe kwa malengo yale ambayo mmeyakusudia mie kazi yangu kubwa ilikuwa ni kutimiza ahadi yangu ambayo niliitoa kwenu,”
“Naendelea kumshukuru Rais wetu Dkt Samia Sulluhu kutokana na miradi mbalimbali inayoletwa katika wilaya yetu ya Maswa na niwahakikishie hii stendi yetu hivi karibuni itabadilika na lengo tunataka kuhakikisha kuwa itakuwa ya kisasa”amesema.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo (aliyesimama) akizungumza na Mawakala wa Stendi ya Mabasi mjini Maswa.
Amesema kwa haya anayoyafanya ni machache lakini kwa siku zijazo atafanya mambo makubwa katika stendi hiyo ili watumiaji wa eneo hilo wawe katika mazingira mazuri kama vilivyo vituo vingine vya mabasi katika maeneo mbalimbali ambavyo kwa sasa vina stendi za mabasi za kisasa.
Naye Mwenyekiti wa Mawakala wa Mabasi Stendi ya Mjini Maswa,Hassan Bunango (Msemakweli) amemshukuru Mbunge huyo kwa kutimiza ahadi yake hiyo na kumhahidi kwamba vipaza sauti hivyo watavitumia kwa malengo ambayo yamekusudiwa.
Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo (Kulia) akikabidhi Spika moja kati ya Mbili kwa Uongozi wa Mawakala wa Mabasi katika kituo cha Mabasi mjini Maswa na aliye kati ni Mwenyekiti wa Mawakala hao,Hassan Bunango.
“Mbunge nachukua fursa hii kukupongeza na kukushukuru kwa kutimiza ahadi yako ambayo ulihaidi baada ya kuridhia ombi letu na leo watu wote wameshuhudia umekabidhi vipaza sauti hivyo tutakuwa tayari kuanza kurusha matangazo na hili lilikuwa hitaji letu ili tuweze kutangaza mabasi yanayoingia na kutokana katika stendi yetu pamoja na matangazo mengine,”
“Kwa wanaumoja niwaomba tutoe ushirikiano na tuhakikishe vyombo hivi vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kufanya jambo kinyume na hapo ni kumuangusha mbunge wetu ambaye ametupatia vyombo hivi vya matangazo,”amesema.
Vifaa hivyo vya matangazo vilivyokabidhiwa ni pamoja na Spika mbili,Kipaza sauti(Microphone)na Kichanganya sauti(Sound mixer) na vyote vikiwa na thamani ya Sh Milioni Moja.
Post a Comment