POLISI TARIME : MJANE UNAPOPATA TATIZO DAWATI LA JINSIA LIPO KWA AJILI YAKO
Na Dinna Maningo, Tarime
JESHI la Polisi mkoa wa Polisi Tarime, Rorya limewahimiza wanawake wakiwemo wajane wanapopatwa na matatizo yakiwemo ya ukatili wa kijinsia wafike Dawati la Jinsia la Polisi ili wapate msaada wa kisheria.
Hayo yameelezwa wakati wa maadhimisho ya wiki ya wanawake Duniani ambapo halmashauri ya mji wa Tarime kwa kushirikiana na wanawake wa Tarime mjini kupitia kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo ikiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati, Noellah Gachuma wameadhimisha Machi, 5, 2024 katika viwanja vya shule ya msingi Kibumaye.
Wanawake wakiwa kwenye maadhimisho wiki ya wanawake Duniani katika viwanya vya shule ya msingi Kibumaye
Baadhi ya wanawake, viongozi wa ngazi ya Kata, wanawake kutoka vyama vya siasa, Polisi, Walimu, wanafunzi wa kike, Taasisi mbalimbali, baadhi ya wanaume, wafanyabiashara na wajasiliamari wameshiriki.
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Polisi Tarime, Rorya Rizi Amiri Freddy akizungumza katika maadhimisho hayo, amesema Jeshi la Polisi lina dawati linaloshughulikia masuala ya jinsia na watoto kama njia ya kusaidia wanawake na watoto ambao wananyanyasika katika jamii.
Msaidizi kutoka Jeshi la Polisi Tarime, Rorya ,Rizi Amiri Freddy akizungumza, kushoto ni Noellah Gachuma
" Sisi kama Jeshi la Polisi tunapokea kesi mbalimbali katika dawati letu na kutatatua matatizo ya aina mbalimbali katika dawati letu la jinsia, hivyo basi akina mama wakiwemo wajane ukipata changamoto zozote hata pale unapokuwa umepigwa, umevamiwa njoo dawati la jinsia.
" Wewe kama mwanamke jua kuwa Jeshi la Polisi lina uwezo wa kukutetea kupitia dawati la jinsia, dawati linalosimamiwa na wanawake wa Jeshi la Polisi, pia kuna wanaume lakini wengi ni wanawake" amesema Rizi .
Amesema kuwa kuanzishwa kwa dawati hilo ilibainika kuwa, mwanamke ana uhuru wa kuongea na mwanamke mwenzake anapoenda kuelezea changamoto zake kuliko anapomwelezea mwanaume.
" Jeshi la Polisi linaimarisha dawati kwa ajili ya kutetea wanawake na watoto. mama mjane, mwanamke unapopata tatizo dawati la jinsia lipo kwa ajili yako, lilianzishwa kwania mahususi kwa ajili ya wanawake.
" Kwasababu jamii yetu huku tunajua mwanamke katika jamii hana nafasi kubwa na mama ameweza kupata nafasi ya kusema hivi karibuni" amesema Rizi .
Pia amewaomba wanafunzi wanapofanyiwa ukatili kutoa taarifa kwa walezi wa shule au watendaji ili wamsaidie kupata haki zao katika dawati la jinsia.
"Ukiwa na tatizo muone mlezi wa shule au mtendaji waeleze kisha atakuleta dawati la jinsia ambalo linashughulika na watoto. Pinga ukatili ukiwa mtoto ili utakapokuwa mkubwa usaidie wengine katika kupinga ukatili.
" Mfano kuna kesi moja tulipokea mwezi wa 12 mwaka jana, kuna mtoto alichomwa na baba yake kwasababu ya kuchukua mboga. Msikae na watu wanaofanya ukatili, kama anamchoma mtoto wake aliyemzaa atashindwa kukuchoma wewe asiyekuzaa?.
Amehimiza jamii kuepukana na ukatili na badala yake wawekeze kwa watoto wa kike waliopo shuleni wakiwa bado wadogo.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani halmashauri ya mji Tarime, Noellah Gachuma amesema kuwa dawati la jinsia linafanya kazi lakini baadhi ya wanawake hutoa taarifa za kufanyiwa vitendo vya kikatili lakini siku chache zikipita umalizana na wahusika.
Noellah Gachuma akizungumza, kulia ni Diwani Kata ya kitare aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho siku ya wanawake Halmashauri ya Mji Tarime
"Wanatoa taarifa baadae wanamalizana kinyumbani na muhusika, kesi inashindwa kuendelea na hivyo kurudisha nyuma jitihada za polisi katika kukomesha vitendo vya ukatili.
" Mwanamke anapompeleka mwanaume dawati sio kwamba hana nidhamu anakwenda kutafuta haki. Kumekuwa na msemo kuwa ukiona mwanamke anampeleka mme polisi ujue mwanamke huyo sio mzuri, hapana wanaenda kutafuta haki " amesema Noellah.
Pia amewaasa wanawake kuwaheshimu waume wao na kuwapenda, wakiwaheshimu hawawezi kupigwa na kwamba Vikoba visiwaharibu kwani sikio halizidi kichwa.
Katika Maadhimisho hayo wajane wapatao 20 wamepata msaada wa sukari, sabuni, mafuta ya mboga, shuka mbuli, mchele unga wa ngano kila mmoja, vilivyotolewa na wanakamati na baadhi ya wadau.
Wajane wakiwa pamoja na Kamati ya maandalizi ya maadhimisho siku ya wanawake Duniani pamoja na viongozi wengine ambao ni wanaume
Kauli mbiu katika maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani 2024 inasema "Wekeza kwa mwanamke kuharakisha maendeleo ya Taifa na ustawi wa Jamii''.
Post a Comment