HEADER AD

HEADER AD

RC PWANI AWAONDOA HOFU WAWEKEZAJI KUHUSU UMEME

Na Gustafu Haule, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amefungua Baraza la Biashara la Mkoa huku akiwatoa wasiwasi wawekezaji kuhusu suala la umeme  kwakusema changamoto hiyo inakwenda  kuisha kwakuwa Serikali imeweka mipango mizuri.

Kunenge amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya kutengeneza miundombinu ya umeme ikiwemo ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere lililopo Wilayani Rufiji ambalo tayari mpaka sasa limeanza kufua umeme Kwa kuwasha mtambo mmoja unaozalisha megawati zaidi ya 200.

   


Kunenge amesema hayo wakati akifungua baraza hilo leo Machi 06 lililofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa uliopo Mjini Kibaha kikao ambacho kimehudhuriwa na wawekezaji mbalimbali wa viwanda, viongozi wa chemba ya biashara mkoa, Taasisi wezeshi za Serikali,Watendaji ofisi ya Biashara Mkoa pamoja wawakilishi kutoka Baraza la Taifa la biashara.

Amesema kuwa mkoa wa Pwani unahitaji kuwa na wawekezaji wengi ndio maana wamejipanga vizuri katika kila idara na kwamba hakuna mwekezaji ambaye atashindwa kuwekeza kwa changamoto ya kufelishwa na wakuu wa idara au taasisi wezeshi ikiwemo TRA,OSHA, ,TANESCO,TARURA,TANROADS na DAWASA.

     Kikao cha Baraza la Biashara Mkoa wa Pwani kilichofanyika  Machi 06,2024 Mjini Kibaha

Amesema juhudi za uwekezaji zinazofanyika mkoa wa Pwani zinatokana na nguvu kubwa ya Rais Samia ambaye ndiye aliyetengeneza mazingira mazuri na wezeshi kwa wawekezaji hivyo lazima yafanyike mazuri ambayo Rais anayataka.

Kunenge amesema kuwa Rais Samia anatambua changamoto ya umeme inayowakabili wawekezaji ndio maana ameelekeza nguvu nyingi katika kuhakikisha umeme unapatikana ili kusaidia katika kuongeza uwezo wa uzalishaji na kwamba wawekezaji wasiwe na hofu juu ya umeme.

"Suala la umeme tunaona namna ambavyo Rais wetu anavyolipambania kwahiyo tuwaombe wawekezaji mtuvumilie kidogo kwani muda si mrefu mtapata umeme wa uhakika na hivyo kuongeza uzalishaji,"amesema Kunenge.

      Wajumbe wa kikao cha Baraza la Biashara Mkoa wa Pwani kilichofanyika Machi 06  ,2024 Mjini Kibaha.

Rc Kundnge amesema kuwa mkoa wa Pwani unajumla ya viwanda 1,533 lakini viwanda 33 vimepatikana kipindi cha Rais Samia tangu aingie madarakani na viwanda 7 vimetoka kuwa viwanda vya kati kuwa viwanda vikubwa na kwamba vingine vinaanzishwa.

Kuhusu migogoro ya ardhi Kunenge amesema kuwa migogoro ipo lakini tayari kuna hatua zimechukuliwa kwani wapo watu ambao wamechukuliwa hatua za kisheria  ikiwemo kupelekea mahakamani  huku akisema hatokubali kuona utapeli wa ardhi unafanyika ndani ya mkoa wake.

Katibu wa Baraza la Biashara la Taifa Dkt.Godwin Wanga amesema kuwa mkoa wa Pwani unafanya vizuri katika masuala ya uwekezaji na Biashara huku akitaka kuongeza juhudi ili wafanye vizuri zaidi.

         Katibu wa Baraza la Biashara la Taifa Dkt.Godwin Wanga

Wanga amesema mwaka huu kuna tuzo Kwa ajili ya mkoa utakaofanya vizuri katika masuala ya uwekezaji na biashara huku akisema hana mashaka na mkoa wa Pwani kwakuwa vigezo vyote muhimu wanavitimiza.

Wanga ametaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na hupatikanaji wa ardhi , hupatikanaji wa taarifa na uwazi wa kushughulikia masuala biashara, kuondoa sera kandamizi katika biashara na uwekezaji, kazi na mafunzo, huduma za kusaidia biashara, kipaumbele katika uwajibikaji na vigezo vingine.

Hatahivyo, afisa mahusiano wa kampuni ya MMI Abubakar Mlawa, ameipongeza juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na hasa katika kushughulikia changamoto mbali huku akiomba utaratibu wa ukaguzi kwa wafanyakazi viwandani huwe shirikishi baina ya taasisi moja na nyingine huku akitolea mfano wa OSHA na TMDA.

    Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara Mkoa wa Pwani Said Mfinanga ,akizungumza katika kikao cha Baraza la Biashara kilichofanyika Machi 06,2024 Mjini Kibaha

No comments