TGNP YAELEZA SABABU ZINAZOKWAMISHA WANAWAKE KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI
>>Idadi ya Wabunge wanawake wakuchaguliwa ni 24
>> Madiwani 204
>> Wenyeviti wa vijiji ni 246 ,Wenyeviti wa Mitaa 528, wa vitogoji ni 4,171
Na Gustafu Haule, Dar es Salaam
MKURUGENZI Mtendaji wa Mtandao wa Kijinsia hapa nchini(TGNP) Lilian Liundi, ametaja sababu zinazokwamisha wanawake kushindwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuwa ni pamoja na kuwepo kwa vitendo viovu vya ukatili wa Kijinsia hususani wa kingono na rushwa ya ngono.
Liundi amesema sababu nyingine ni mila kandamizi, desturi na mitizamo hasi dhidi ya ushiriki wa wanawake katika maamuzi pamoja kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa mifumo rasmi na wezeshi ya Kikatiba, na Kisheria katika usawa wa nafasi za uongozi.
Liundi ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari kutoka Mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es Salaam juu ya kuandika habari Kwa mtazamo wa kijinsia na namna ya kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi .
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ofisi za TGNP zilizopo Jijini Dar es Salaam yamefanyika kuanzia Machi 21 mwaka huu yameratibiwa na TGNP kwa kushirikiana na TADIO kwa udhamini wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women).
Liundi amesema kuwa sababu hizo zimekuwa mwiba kwa wanawake katika kufikia malengo yao kwani hata wanapokuwa na dhamira ya dhati katika kuwania nafasi hizo wanakutana na vikwazo hivyo ambavyo mara nyingi hupelekea wanawake kukata tamaa.
Amesema ni wakati muafaka kwa sasa kuona kuwa wanawake wanaweza kuongoza na kushika nafasi hizo huku akiomba jamii hususani wanaume kuondoa dhana potofu na hivyo kutoa nafasi kwa wake zao kugombea nafasi za uongozi.
AmesemaTanzania imeweka historia kubwa ya kuwa na Rais mwanamke kwa mara ya kwanza tangu nchi hipate Uhuru ambaye ni Dkt.Samia Suluhu Hassan na ameonyesha dhamira ya kuongeza usawa wa Kijinsia na kwamba watanzania wanapaswa kuiga mfano wake.
"Tumekuwa na Maspika wa Bunge Wanawake wawili ambao ni Anne Makinda na Dkt.Tulia Ackson na sasa tunao mawaziri wanawake walioshika nafasi katika Wizara zinazoaminika kuwa ni za Wanaume kama vile Waziri wa Ulinzi Stigomena Tax,Wizara ya Mambo ya Nje Liberata Mulamula,Katibu wa Bunge Nenelwa Mhambi na Mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu Zuhura Yunus,"amesema Liundi.
Ameongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa viongozi hao wanawake lakini bado hakuna uwakilishi wa kutosha wa wanawake katika nafasi za uongozi za kuchaguliwa na kuteuliwa katika ngazi mbalimbali za uongozi .
Amesema kwa sasa kuna unafuu ikilinganishwa na tulipotoka kuna mabadiliko chanya katika ushiriki wa wanawake katika uongozi.
Baadhi ya Wandishi wa habari wakiwa katika mafunzo yaliyotolewa juzi Jijini Dar es Salaam na Mtandao wa Kijinsia (TGNP) kuhusu masuala ya nafasi za uongozi kwa wanawake .
Amesema takwimu zinaonyesha kuwa bado kuna idadi ndogo ya ushiriki wa wanawake katika masuala ya kiuongozi huku akisema kwa nafasi ya wabunge wanawake idadi yao ni ndogo ukilinganisha na hali halisi ya wabunge wote waliopo Bungeni.
Amesema wabunge wanawake wa kuchaguliwa idadi yao ni 24 kati ya wabunge 264 ambao ni sawa na asilimia 9.1 na idadi ya wabunge wanawake wa viti maalum ni 113 ambao ni sawa na asilimia 29 ya wabunge wote na kwamba jumla ya wabunge wanawake ni 141 sawa na asilimia 37 ya wabunge wote ambao ni 393, idadi ambayo ni ndogo ukilinganisha na lengo la kufikia 50 kwa 50.
Kwa upande wa madiwani takwimu zinaonyesha kuwa madiwani wanawake wa kuchaguliwa kutoka kwenye Kata 204 ni sawa na asilimia 3.8 ya madiwani wa kuchaguliwa 3,946.
Afisa uhusiano wa Mtandao wa Kijinsia nchini (TGNP) Monica John akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mafunzo ya kuwajengea uwezo
" Madiwani wanawake wa Vitimaalum ni 1,407 sawa na asilimia 26.2 ya madiwani wote ambapo kwa ujumla wanawake madiwani ni 1,611 sawa na asilimia 30 ya madiwani wote Nchini ambao ni 5,353" amesema.
Kuhusu wenyeviti wa serikali za Vijiji na Vitongoji Liundi amesema wenyeviti wa serikali ya Vijiji wanawake ni 246 kati ya wenyeviti 11,915 nchi nzima sawa na asilimia 2.1. Wenyeviti Serikali za Mitaa wanawake ni 528 sawa na asilimia 12.7 kati ya wenyeviti 4,171 nchi nzima.
Katika ngazi ya Vitongoji wanawake wenyeviti ni 4,171 kati ya 62,612 ambayo ni sawa na asilimia 6.6.
Afisa mahusiano wa TGNP Monica John amesema kuwa kutokana na hali hiyo wameona ni vyema wakashirikiana na vyombo vya habari vya kijamii katika kuendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo ili waweze kuandika habari za kuhamasisha jamii ya kuondokana na dhana kandamizi kwa wanawake.
Waandishi wa habari Mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa mafunzo kuhusu masuala ya nafasi ya uongozi kwa wanawake
Monica amesema Waandishi wa habari endapo watatumia kalamu zao vizuri juu ya kuelimisha jamii anaimani itakuwa fursa ya jamii kuondokana na dhana hasi kuhusu wanawake kugombea nafasi za uongozi na hivyo kufikia malengo ya 50/50 .
"Mwaka huu kuna uchaguzi wa serikali za Mitaa kwahiyo tunaimani mafunzo haya ni maandalizi mazuri kwa Waandishi wa habari katika kuhamasisha wanawake wajitokeze kugombea masuala ya uongozi na hasa kutoa elimu juu kuepuka na mila kandamizi na mitazamo hasi ya Kijinsia, amesema Monica.
Hatahivyo Monica amesema mafunzo hayo yamejumuisha Waandishi wa habari 57 kutoka Mikoa minne wanaofanya kazi zao katika magazeti,Televisheni ,Redio na mitandao mbalimbali ya kijamii zikiwemo blog na kuwataka kutumia mafunzo hayo kikamilifu kwa faida jamii na Taifa kwa ujumla.
Post a Comment