BILIONI MOJA KUMALIZA TATIZO LA MAJI KIJIJI CHA IPILILO
Na Samwel Mwanga, Maswa
WANANCHI wa kijiji cha Ipililo katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wanaelekea kupata afueni ya changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi na salama ya bomba kufuatia kuanza ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji hicho kwa gharama ya Tsh. 1,320,234.415.50
Hayo yameelezwa April 9 mwaka huu na Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ipililo mara baada ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo kutembelea eneo la ujenzi wa mradi huo unaosimamiwa na Wakala wa maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA).
Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu anakazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wananchi wanakuwa na furaha katika maeneo yao ukiwemo usalama,utulivu na amani pamoja na utoaji wa huduma za kijamii na aliona kupitia viongozi wanaomsaidia kuwa katika kijiji hicho kuna changamoto ya upatikanaji wa maji na ndiyo maana ameleta mradi huo wa maji.
Amesema kuwa kwa sasa Mkandarasi amekwisha kupatikana kwa ajili ya kutekeleza mradi huo na tayari amekwisha kuanza kazi ya ujenzi wa tenki kubwa sambamba na kuchimba mitaro kwa ajili ya kusambaza mabomba ya maji kwa ajili ya kupeleka kwenye maeneo ambapo zilizo nyumbani za wananchi hao.
“Kupitia viongozi wenu mliowachagua ambao ni diwani na mbunge wamepeleka kilio chenu kwa serikali juu ya changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika kijiji cha Ipililo na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesikia na ametoa kiasi hiki cha fedha zaidi ya Tsh. Bilioni moja ili muweze kupata maji ya bomba.
“Na huyu Mkandarasi ambaye anatekeleza mradi huu mie namfahamu ni mzuri na amewahi kutekeleza mradi wa maji katika kijiji cha Isanga na alifanya vizuri sana hivyo sina wasiwasi naye hivyo ni vizuri mkampatia ushirikiano ili mradi huu uweze kukamilika.”amesema.
Dc Kaminyoge amesema kuwa mkataba wa kazi wa kutekeleza mradi huo ni kipindi cha mwaka mmoja lakini kwa kuwa nafahamu matatizo ya wananchi wa kijiji hiki nimemuaomba Mkandarasi aweze kukamilisha mradi huo kwa kipindi cha miezi miwili.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akizungumza na Wananchi wa Kijiji Cha Ipililo(hawapo pichani)“Najua changamoto yenu ya suala la upatikanaji wa maji katika kijiji cha Ipililo na leo hii nimemuomba huyu Mkandarasi aweze kukamilisha mradi huu kwa miezi miwili badala ya mwaka mmoja naye amenikubalia hivyo kufikia mwezi Mei mwaka huu mtaanza kutumia maji ya bomba ambayo ni safi na salama,”amesema.
Awali Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Maswa, Jofrey Kiama amesema kuwa mradi huu utakapokamilika utawanufaisha wananchi wapatao 8,361 katika kijiji hicho ambapo awali walikuwa wanategemea visima vya asili na visima vifupi vyenye pampu za mkono.
Amesema hatua hiyo ni utekelezaji ibara ya 100 ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo inaeleza kuwa hadi kufikia mwaka 2025 asilimia 85 ya wananchi waishiyo vijijini wawe wamepata huduma ya maji safi na salama.
“Hadi sasa mradi unatekelezwa na Mkandarasi yupo eneo la mradi na sisi Ruwasa wilaya ya Maswa tunatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassa kwa kutuletea fedha za utekelezaji wa ujenzi wa mradi huu wa maji katika kijiji cha Ipililo ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika kijiji hiki,”amesema.
Amesema kuwa chanzo cha maji katika mradi huo ni kisima chenye urefu wa mita 120 kilichopo kwenye kijiji hicho na chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 19,000 kwa saa sawa na lita 456,000 kwa siku na mahitaji kwa siku ni lita 359,893
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya URSINO Ltd, Mnandi Mnandi ambaye ndiye Mkandarasi wa Mradi huo amewahakikishia wananchi wa kijiji cha Ipililo ya kuwa kupitia ombi la Mkuu wa wilaya hiyo wataanza kupata maji safi na salama ya bomba kufikia mwezi Mei mwaka huu ili kuondoa adha ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya URSINO Ltd,Mnandi Mnandi ambaye ni Mkandarasi wa Mradi wa Maji katika Kijiji Cha Ipililo akieleza hatua za Utekelezaji wa Mradi huo.“Sisi ni Wakandarasi ambao tunatekeleza mradi wa maji katika kijiji cha Ipililo na tulikabidhiwa rasmi Machi 28 mwaka huu kazi zinaendelea kama mlivyoona na mtakumbuka wakati tunasaini mikataba ya kazi hizi pale kwa Mkuu wa mkoa alisisitiza tufanye kazi kwa uadilifu.
"Leo Mkuu wa wilaya ametembelea eneo la mradi na ametoa maelekezo ifikapo mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu wananchi wa Ipililo wanywe maji na tutaanza na baadhi ya vituo kupata maji maana serikali hii imewekwa madarakani na wananchi na haitaki wapate shida nasi tutatekeleza,”amesema.
Post a Comment