HEADER AD

HEADER AD

VYOO SHULE ZA MSINGI KATA YA IKOMA NI HATARISHI

>>Wanafunzi  1,140 Bugire wanatumia choo kilichotitia

>>Wanafunzi 1,019 Kogaja wanatumia choo kisicho na ubora

>>Wanafunzi 851 Nyamasanda hawana choo, kilichojengwa kwa muda kimejaa

>> Ded Rorya asema Milioni 250 zimetengwa kujenga vyoo 125 shule za msingi

Na Dinna Maningo, Rorya

SHULE za msingi zilizopo Kata ya Ikoma, wilaya ya Rorya mkoani Mara, zinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyoo vya kisasa jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa wanafunzi.

Shule ya msingi Bugire inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa choo cha kisasa huku wanafunzi 1,140 wakilazimika kutumia choo cha matundu matano ambacho si salama kutokana na kuchakaa.

         Shule ya msingi Bugire

Hali hiyo imepelekea ofisi ya afya wilaya kutoa siku 60 kujengwa vyoo vipya vinginevyo shule zitafungwa na kwamba muda uliotolewa tayali umekwisha na choo hakijajengwa, wananchi wapo kwenye hatua ya uchimbaji shimo.

Hayo yameelezwa na Kaimu Afisa Elimu Msingi Kata ya Ikoma ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bugire, Jackson Nyangubo wakati Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa (CCM) Sango Kasera Gungu alipofika katika kata hiyo na kukabidhi msaada wa madawati 50 kwa ajili ya shule za msingi zilizopo katika kata hiyo.

       Kaimu Afisa elimu Msingi Kata ya Ikoma ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bugire, Jackson Nyangubo alieleza changamoto za shule

"Natoa shukrani kwa Sango kwa namna ambavyo ameona uhitaji mkubwa katika elimu. Tunashukuru kwa msaada wa madawati 50, ni kweli tuna upungufu wa madawati 469 kata nzima. 

"Pia tuna shida sana ya vyoo katika shule zetu za msingi. Shule ya Burige mahitaji ya matundu ya choo ni 51, yaliyopo hakuna maana choo cha matundu matano kimetitia na bwana afya wilaya ya Rorya alitoa siku 60 kijengwe choo kingine bora. Wananchi wapo kwenye hatua ya kuchimba shimo na siku 60 zimeisha bado ujenzi wa choo haujakamilika" amesema Mwl. Jackson.

Akizungumzia changamoto ya choo shule ya msingi Kogaja amesema shule ina jumla ya wanafunzi 1,019, mahitaji ya matundu ya choo ni 45 yaliyopo ni 6 pungufu ni 39  na shule hiyo imepewa siku 60 kujengwa choo kipya.

Katika shule ya msingi Nyamasanda ina wanafunzi wapatao 851, mahitaji ni matundu 38 yaliyopo hakuna, choo kilichojengwa kwa muda kimejaa, pungufu ni matundu 38 na hivyo shule zote kuwa na jumla ya mahitaji ya matundu ya vyoo 134, pungufu ni matundu 128 yaliyopo 6 ambayo hayana ubora.

" Tunashukuru wananchi wamepambana na kuchimba shimo la matundu 12 wanaendelea na utaratibu wa kukusanya fedha japo jamii yetu uelewa bado ni mdogo, tunakuomba Sango kwasababu umeona umuhimu wa elimu tujali kwa hilo pia"amesema Jackson.

Sango Kasera akatoa Tsh. 100,000 kwa ajiri ya ununuzi wa saruji mifuko 5 ujenzi wa choo shule ya msingi Bugire na kuahidi kushirikiana nao.

Wakizungumza kwa njia ya simu Diwani wa Kata ya Ikoma Laurent Adriano (CCM) amesema changamoto ya vyoo ameshaizungumzia kwenye halmashauri na kuahidiwa fedha zitakapopatikana zitapelekwa kujenga vyoo.

"Taarifa za shule za Bugire zipo ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri, nishazungumza pia kwenye vikao vya Baraza la Madiwani. Kabla ya taarifa kuwasilishwa kwa madiwani zinafika kwa mkurugenzi alafu mkurugenzi anaziandaa vizuri na kuzitengenezea kablasha alafu anatuletea.

"Majibu nayopewa ni kwamba tunatafuta pesa mahitaji ni mengi hivyo akipata pesa zitapelekwa. Wananchi wangu wa Ikoma wanajitahidi kuchangia maendeleo ila mkwamo upo halmashauri kulingana na ufinyu wa fedha." amesema Laurent.

DIMA Online imemuuliza Diwani huyo kufahamu yeye amechangia vipi ujenzi wa vyoo akiwa Diwani wa Kata hiyo, naye amesema ;

"Kuchangia pesa haina tatizo sasa utachangia simenti wakati pesa yenyewe haijatoka halmashauri ! , hujawahi kusikia simenti zilikuwa zinatolewa nyingi baadhi ya sehemu zikaganda!.

" Kwa uzoefu niliokaa halmashauri wananchi wanatakiwa wachangie sehemu na halmashauri ichangie, kuna maombi yakifika halmashauri fedha zinatengwa kulingana na bajeti " amesema Laurent.

DIMA Online imewasiliana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya Abdul Mtaka kufahamu kama ofisi yake ina taarifa ya changamoto za vyoo shule za msingi Kata ya Ikoma, naye amesema;

" Sijapata taarifa hizo kwenye ofisi yangu ndiyo wewe unaniambia habari hiyo. Hata hivyo katika bajeti ya fedha ya 2024/2025 tumetenga fedha Milioni 250 kwa ajili ya vyoo 125 katika shule za msingi na Milioni 58 kwaajili ya vyoo 33 shule za sekondari wilayani Rorya.

"Kwakuwa umeniambia nitafuatilia ili kufahamu mahitaji na ikiwezekana pesa ipelekwe. Kunapotokea dharura halmashauri hupeleka fedha kupitia mapato ya ndani kutatua changamoto za dharura, mfano Kwibuse, Nyamaguku tulipeleka milioni tano kila shule. 

Ameongeza "Shule ya msingi Gukona ilikuwa na changamoto wananchi walijenga boma na halmashauri tukapeleka fedha za kukukamilisha ujenzi wa choo  na shule zinginezo " amesema Ded Abdul.


No comments