HEADER AD

HEADER AD

CCM SIMIYU : SIKILIZENI NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI

Na Samwel Mwanga, Maswa

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed amewataka viongozi wa chama hicho na viongozi wa serikali wa ngazi mbalimbali katika mkoa huo kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.

Pia amewataka Watumishi wa Serikali kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi kwani serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na  Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake.

Amesema hayo kwa nyakati tofauti katika wilaya ya Maswa katika maeneo ya Mji wa Malampaka, Maswa na Lalago katika mikutano aliyoifanya ya kuzungumza na wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi na kusikiliza kero zao.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu akizungumza na Wananchi wa Tarafa ya Mwagala katika wilaya ya Maswa.

Amesema kuwa ameaamua kufanya ziara ya kusikiliza kero na kuzitatua  za wananchi katika tarafa zote za mkoa huo kama aliyoagiza Mwenyekiti wa CCM Taifa ,Dkt Samia Suluhu Hassan  huku akiwasisitiza na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali kufanya hivyo.

“Nimeamua kufanya ziara ya kutembelea maeneo ya  makao makuu ya tarafa zote zilizoko katika mkoa wa Simiyu na lengo kubwa ni kuwasikiliza ninyi wananchi kero zenu na kuzitatua maana ninyi ndiyo mliotupa ridhaa kwa kukichagua chama chetu cha CCM kuongoza dola katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020”

“Pia viongozi wa CCM na viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali kuwa na utamaduni wa kutoa taarifa  kwa wananchi  juu ya miradi mbalimbali inayotekelezwa  au iliyotekelezwa na kueleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu katika maeneo wanayosimamia,”amesema.

Mwenyekiti huyo ametumia fursa hiyo kumpongeza Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge kwa kutatua kero za wananchi hao kwa kufanya mikutano mbalimbali katika Kata zote za wilaya hiyo hivyo kuwaomba na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali katika mkoa huo katika maeneo yao waweze kuiga mfano huo.
      Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed akisikiliza kero za wananchi wa Tarafa ya Mwagala wilayani Maswa katika shule ya sekondari Lalago.

“Katika ziara hii niliyoifanya katika wilaya ya Maswa nimejifunza jambo moja kero nyingi zilizozungumzwa ziko ndani ya uwezo wa wilaya na nyingi zimepatiwa ufumbuzi baada ya mkuu wa wilaya ya Maswa kuwa na utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi katika mikutano yake katika kila Kata huu ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine,”amesema.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amesema kuwa caham hicho hakitasita kuwafikisha, kwenye Kamati ya Maadili Viongozi wa Chama hicho ambao watabainika kuanza kuwatafutia watu nafasi za uongozi ikiwemo Ubunge na Udiwani kabla ya muda kufika.

“Viongozi wetu walioko madarakani ambao ni madiwani na wabunge waacheni wafanye kazi zao za kuwatumikia wananchi lakini kuna tabia imeanza kwa baadhi ya viongozi wa CCM kuanza kutembea na majina ya madiwani na wabunge wao hili jambo halikubaliki tuwaache wafanye kazi na muda ukifika na ukibainika tutakufikisha katika Kamati ya Maadili,”amesema.

Awali Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema kuwa wilaya hiyo imepokea fedha nyingi zaidi ya Sh Bilioni 10 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Afya, Elimu, Maji, Kilimo na mifugo na wanaisimamia vizuri ili kuhakikisha fedha iliyoletwa inafanya kazi iliyokusudiwa.

    Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akizungumza na Wananchi wa mji wa Malampaka.

Pia amesema kuwa ameweza kufanya mikutano mbalimbali ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua katika Kata mbalimbali za wilaya hiyo na kila siku ya Alhamisi ya kila juma amepanga kuwa ni siku ya kusikiliza kero za migogoro ya ardhi chini ya kamati aliyoiunda.

Ziara hii  ni ya Tarafa kwa Tarafa ambapo pamoja na kukagua uhai wa chama pia inasikiliza maoni ya wanachama na wananchi kuhusu miradi iliyotekelezwa katika maeneo yao.

    Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed akizungumza na Wananchi katika mji wa Lalago wilaya ya Maswa.

No comments