HEADER AD

HEADER AD

CCM SIMIYU : WABUNGE, MADIWANI TIMIZENI AHADI ZENU MLIZOAHIDI WANANCHI


>>Mwenyekiti CCM asema wakati wa kampeni Wabunge na Madiwani walitoa ahadi zao binafsi 

>>Awataka kutekeleza ahadi zao

>>Asema ambao hawakutimiza majukumu yao wasipewe nafasi

Na Samwel Mwanga, Meatu

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed amewataka wabunge na madiwani wa chama hicho katika mkoa huo kuhakikisha wanatimiza ahadi zao binafsi walizohaidi kwa wananchi wakati wa kampeni ili kutatua kero za wananchi na kuendelea kuaminika kwa wananchi waliowapa ridhaa ya kuwaongoza kwa miaka mitano.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi na wanachama tarafa ya Nyalanja katika Kata ya Mwamanongu wilayani Meatu ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kusikiliza kero za Wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla.

      Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed akizungumza na Wananchi wa Tarafa ya Nyalanja katika Kijiji cha Mwamanongu wilaya Meatu

Amesema ni vizuri kwa wabunge na madiwani kutimiza wajibu wao kwenye Majimbo na Kata zao kwa kutimiza ahadi zao binafsi walizozitoa kwa wananchi

Amesema kuwa zile ahadi ambazo CCM ilihaidi kupitia ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 zinaendelea kutekelezwa na serikali kupitia Mwenyekiti wa CCM Taifa,Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema kuwa kwa asilimia kubwa ya ahadi za CCM zilizoandikwa kwenye Ilani zimetekelezwa hadi kufikia mwaka 2025 zote zitakuwa zimekamilika na ushahidi unajionyesha wazi jinsi serikali inavyotoa fedha nyingi katika kutekeleza miradi katika sekta mbalimbali.

      Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed akizungumza na Wananchi wa Tarafa ya Nyalanja katika Kijiji cha Mwamanongu wilaya Meatu

" Kuna zile ahadi binafsi ambazo wabunge na madiwani waliahidi wananchi na kuwapa matumaini ya kuleta maendeleo katika maeneo yao ambayo wanaishi lakini wapo viongozi baadhi yao hadi leo hii bado hawajamaliza kutekeleza ahadi ambazo walizitoa kwa wananchi.

“Wakati CCM tunaomba ridhaa ya kushika dola katika uchaguzi wa mwaka 2020 tulitoa ahadi mbalimbali na zote ziko kwenye ilani yetu na kwa asilimia kubwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hasssan inatekeleza miradi mbalimbali.

Miradi hiyo ni pamoja na miradi katika sekta za elimu, afya, miundombinu ya barabara, maji, umeme nk na ndiyo maana kila sehemu mtaona fedha nyingi zimemwagwa hadi maeneo ya vijijini ambapo kuna miradi inayotekelezwa" amesema.

        Sehemu ya Wananchi wa Tarafa ya Nyalanja katika Kijiji cha Mwamanongu wilaya Meatu wakimsikiliza Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed(hayupo pichani)wakati wa Mkutano wa kusikiliza kero

Anaongeza kusema " Niwaombe ambao hamjatimiza ahadi zenu mzitimize kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mwingine na niwahakikishie wananchi yule mbunge au diwani au kiongozi yeyote aliyechaguliwa wakiwemo wenyeviti wa vijiji na vitongoji ambaye hakutimiza majukumu yake asitarajie tena kupewa nafasi hiyo hivyo timizeni wajibu wenu,”amesema.

Amesema kuwa CCM mkoa wa Simiyu itaendelea kusaidia kuleta maendeleo kwa wananchi wa mkoa huo katika sekta mbalimbali na ndiyo maana ameamua kufanya ziara hiyo ya tarafa kwa tarafa ili kuweza kusikiliza kero zinazowakabili wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

       Sehemu ya Wananchi wa Tarafa ya Nyalanja katika Kijiji cha Mwamanongu wilaya Meatu wakimsikiliza Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed(hayupo pichani)wakati wa Mkutano wa kusikiliza kero

“Tunaishukuru serikali ya wamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu kwa kusaidia kuboresha sekta ya Afya na Elimu katika mkoa wa Simiyu na wananchi wanaendelea kuwa na imani na serikali yake maana tunashuhudia kujengwa kwa hospitali,vituo vya afya,zahanati na ujenzi wa shule mpya za msingi nna sekondari pamoja na ukarabati wa shule kongwe za msingi katika mkoa wetu,”amesema.

Awali Joel Mbuga mkazi wa kijiji cha Mwamanongu akitoa kero yake mbele ya mwenyekiti huyo amesema kuwa licha ya serikali kutekeleza miradi mbalimbali katika wilaya hiyo lakini bado wapo baadhi ya madiwani na wabunge wameshindwa kutekeleza ahadi zao walizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni za kuomba kupewa ridhaa ya kuchaguliwa katika nyadhifa hizo.

    Joel Mbuga Mkazi wa Kijiji cha Mwamanongu aliyejitokeza kueleza kero yake katika Mkutano wa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed.

“Kuna mambo mazuri yanafanyika ya kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya yetu katika sekta mbalimbali hasa Elimu, Afya na Maji kupitia serikali yetu ya awamu ya sita lakini huku chini kwa madiwani na wabunge bado hawajatimiza ahadi zao mbalimbali walizozitoa kwenye kampeni.

" Niwaombe wazitekeleze kwani walizitamka kwa vinywa vyao wenyewe kwa hiyo sisi wananchi tunawasubiri watimize,” amesema.

No comments