HEADER AD

HEADER AD

DC MASWA AMTIMUA MKANDARASI WA BARABARA


>> Asema haridhishwi na mwenendo wa Mkandarasi

>>Ataka Mkandarasi huyo afutwe kwenye orodha

>>Meneja TARURA asema Mkandarasi kashindwa kazi

Na Samwel Mwanga, Maswa

MKUU wa Wilaya ya Maswa  mkoa wa Simiyu, Aswege Kaminyoge amemfukuza Mkandarasi wa Kampuni ya ASA GENERAL SUPPLIERS AND CONSTACTION Co Ltd ya  Bunda mkoani Mara katika wilaya hiyo kutofanya kazi kutokana na kushindwa kutekeleza kwa wakati matengenezo ya barabara na ujenzi wa daraja.

Pia ameishauri serikali kumfuta mkandarasi na kampuni yake hiyo katika orodha ya Wakandarasi hapa nchini ili asiweze kufanya kazi mahali popote kutokana na kushindwa kuwa mzalendo kwa kuwachonganisha wananchi na serikali yao iliyoko madarakani.

        Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(wa kwanza kushoto)akuangalia Moja ya karavati lililojengwa katika Kijiji Cha Muhida wilayani humo.

Uamuzi huo umechukuliwa Aprili 9 mwaka huu na mkuu huyo wa wilaya aliyeongoza wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo kutembelea na kukagua Matengenezo ya barabara ya Njiapanda-Muhida-Jihu yenye gharama ya Sh 57,127,650.

Ujenzi wa daraja la Wigelekelo katika barabara ya Mwasayi-Masela-Wigelekelo lenye thamani ya sh 51,707,935 na Matengenezo ya barabara ya Bushashi-Ipililo yenye gharama ya Sh 130,277,000 ambazo amepewa mkandarasi wa kampuni hiyo.

      Sehemu ya daraja la Wigelekelo katika wilaya ya Maswa lililotembelewa na wajumbe wa Kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ipililo wilayani humo ambapo wajumbe wa kamati hiyo walihitimisha ziara yao amesema kuwa haridhishwi na mwenendo wa mkandarasi huyo katika kufanya kazi za barabara katika wilaya hiyo.

Amesema mkandarasi ameshindwa kutekeleza kwa wakati kazi zote alizoziomba na kupewa na kusababisha wananchi wa maeneo hayo kupata changamoto kubwa ya usafiri kwa kutumia vyombo vya usafiri yakiwemo magari.

         Sehemu ya barabara ya Bushashi-Ipililo wilaya ya Maswa ikiwa imeharibika licha ya Mkandarasi ASA GENERAL SUPPLIERS AND CONSTRACTION Ltd kupewa kazi hiyo lakini ameitelekeza.

Amesema kuwa hawezi kumvumilia mkandarasi huyo kutokana na kushindwa kufanya kazi hizo licha ya kuitwa mara kwa mara na uongozi wa wilaya na kupewa maelekezo lakini amekuwa hatekelezi licha ya serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu imetoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya miundo mbinu hiyo ya barabara.

Dc Kaminyoge amesema kuwa kwa sasa barabara hizo ambazo alipewa mkandarasi huyo hazipitiki hivyo wananchi kuhangaika na kushindwa kupeleka mazao yao kwenye masoko kwa ajili ya kuuza licha ya muda aliopewa kukamilisha ukiwa umekwisha.

       Baadhi ya Wananchi wa Kijiji Cha Muhida wilaya ya Maswa waliojitokeza kumsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo,Aswege Kaminyoge (hayupo pichani) wakati alipotembelea kuona ujenzi wa barabara ya Njiapanda-Muhida-Jihu.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu alitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo pamoja na kujenga daraja baada ya fedha kutolewa walitafutwa Wakandarasi kwa ajili ya kutekeleza maelekezo na maagizo ya Mh. Rais tangu mwezi Oktoba mwaka jana kwa mujibu wa taarifa ambazo zipo.

“Hadi leo mkandarasi aliyekabidhiwa hizo barabara hadi sasa hajamaliza na mwisho wa mkataba ulikuwa mwezi Machi mwaka huu barabara hazijaisha. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya imelizungumzia suala zaidi ya mara tatu na kumwita mkandarasi kumpa maelekezo.

"Hata kama anasema kuwa kuna mvua basi aweke hata kifusi kwenye makaravati aliyojenga,atengeneze maeneo korofi na achimbee mitaro ili ipitishe maji ya mvua yasiaharibu barabara lakini leo tumepita kwenye barabara hizo hasa ya Bushasi-Ipililo maji ni kama bahari,ziwa na mabwawa hakupitiki,”amesema.

Amesema kufuatia hali hiyo akiwa Mkuu wa wilaya ya Maswa ameungana na wananchi wa maeneo hayo kulalamika ubovu wa barabara hizo uliotokana na uzembe wa Mkandarasi licha ya serikali kutoa fedha za kutengeneza barabara hizo jambo hilo hawezi kulivumilia.

     Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(aliyenyoosha mkono)akitoa maagizo kwa Tarura mara baada ya kutembelea matengenezo ya barabara ya Njiapanda-Muhida-Jihu.

Pia amemwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini wilaya ya Maswa afanye manunuzi ya haraka ndani ya kipindi cha juma moja kuhakikisha barabara ya Bushashi-Ipililo inapitika na maeneo korofi katika barabara ya Njiapanda-Muhida-Jihu yanafanyiwa marekebisho ndani ya kipindi cha siku tatu.

Meneja wa Tarura wilaya ya Maswa, Mhandisi Justin  Lukanga amesema kuwa Mkandarasi huyo kazi hizo zimemshinda na TARURA walikuwa wakiandaa taratibu za kumfukuza kwani wamemwita mara kwa mara kuhudhuria vikao vyao(Site Meeting)zaidi ya mara tatu lakini hakuweza kuhudhuria licha ya kuzungumza naye ana kwa ana na kwa simu.

         Meneja wa Tarura wilaya ya Maswa,Mhandisi Justus Lukanga akitoa maelezo kwa Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(hayupo pichani,)juu ya ujenzi wa barabara wilayani humo.

Mhandisi Lukanga amesema kuwa kelele zimekuwa ni kubwa katika wilaya hiyo hasa za ubovu wa barabara kutokana na Mkandarasi huyo kushikilia sehemu kubwa ya kazi hizo na hivyo kushindwa kuzitekeleza hivyo anapaswa kufukuzwa.

“Mnaona kelele ni kubwa katika wilaya hii kwa sababu Mkandarasi huyu ameshikilia sehemu kubwa ya kazi za barabara katika wilaya ya Maswa ndiyo maana kila sehemu wanapiga kelele ana zaidi ya Sh Milioni 800 zote amezikalia tu hataki kufanya kazi, anaitwa hataki kuja tumfukuze,”amesema.

      Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(wa kwanza kulia)akitoa maelekezo kwa Meneja wa Tarura wilaya ya Maswa,Mhandisi Justin Lukanga(aliye kati mwenye kofia nyeusi)baada ya kutembelea Moja ya karavati katika barabara katika Kijiji Cha Muhida.

No comments