TMDA YASHINDA TUZO YA UMAHIRI WA MAWASILIANO BORA NA VYOMBO VYA HABARI
Na Andrew Chale, Dar es salaam
MAMLAKA ya Dawa na vifaa tiba nchini (TMDA ) kupitia kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma imeshinda tuzo ya Umahiri katika Mawasiliano ya umma iliyobeba dhima ya “The best winner in media relations category for the year 2023 ” ikiwa na maana mshindi wa Tuzo Kundi la mahusiano bora na Vyombo vya Habari nchini.
Tuzo za kipekee za umahiri zimetolewa na Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST)hafla iliyofanyika April, 2024, katika Ukumbi wa St. Peter’s jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Winfred Mahundi (wa tatu kushoto ) akimkabidhi tuzo ya ushindi Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Gaudensia Simwanza.
Mgeni rasmi katika utoaji wa tuzo hiyo alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Winfred Mahundi.
Ushindi huo umetokana na mchango mkubwa unaotolewa na kitengo hicho cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma kwa vyombo vya habari mbalimbali nchini.
Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Gaudensia Simwanza akipokea tuzo hiyo amewashukuru wadau wote kwa namna wanavyoshirikiana TMDA katika kuhabarisha umma.
"Tuzo hii ni kwa ajili ya yetu sote na Waandishi wa habari wote ikiwa ni mchango wao katika kutoa elimu kwa jamii.
"Kwa niaba ya uongozi wa TMDA tunawashukuruni sana wadau kwa kuwa nasi kipindi chote hadi kuibuka kidedea na kupata tuzo hii. Asanteni kwa ushirikiano na tuendelee kudumisha huu ushirikiano." Amesema Gaudensia Simwanza.
TMDA ilianzishwa mwaka 2003, hadi sasa ina miaka zaidi ya 20 ikiwa na majukumu ya kulinda afya ya jamii huku ikiwa na ofisi zake katika Kanda mbalimbali nchini sambamba na kuwa na maabara zenye kuhakikisha ubora, usalama na ufanisi wa vifaa tiba na dawa.
Aidha , katika hafla hiyo Taasisi na Masharika mbalimbali yameshiriki katika mashindano hayo ya tuzo katika vipengele tofauti.
Post a Comment