SANGO ATOA MADAWATI KATA YA IKOMA, KIROGO
>>Wenyeviti wa Vijiji, Maafisa elimu Kata, Wananchi wazungumza
Na Dinna Maningo, Rorya
MJUMBE wa Mkutano Mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Sango Kasera Gungu ametoa msaada wa madawati 50 kwa ajili ya shule za msingi zilizopo Kata ya Ikoma na madawati 60 Kata ya Kirogo, Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Akikabidhi madawati hayo April, 2, 2024 katika shule ya msingi Kogaja, mjumbe huyo wa mkutano mkuu ametoa mgawanyo wa madawati hayo katika Kata ya Ikoma ambapo madawati 17 ni ya shule ya msingi Kogaja, madawati 17 shule ya msingi Nyamasanda na madawati 16 shule ya msingi Bugire.
Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Sango Kasera Gungu akizungumza katika kijiji cha Kogaja wakati alipopeleka madawati
" Ilani ya Chama cha Mapinduzi inasema maendeleo yataletwa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na mimi ni miongoni mwa wadau na ni mwana rorya ,mimeguswa na hili nikaamua kusaidia madawati.
"Rorya itajengwa na wana rorya naomba ndugu zangu wa rorya waliopo nje ya rorya nao waje watuunge mkono, kila mtu akileta madawati 50 naamini changamoto ya madawati itapungua kwa kasi kubwa " amesema Sango.
Ameongeza kusema " Nimekabidhi jumla ya madawati 50, afisa elimu wilaya amepanga utaratibu wa mgao, madawati 17 ni kwa shule ya msingi Kogaja, madawati 17 ni ya shule ya msingi Nyamasanda na madawati 16 shule ya msingi Ikoma" amesema.
Viongozi ngazi ya Kata, vijiji na wananchi wamemshukuru Sango kwa msaada wa mabati ambapo mwananchi Magreth
Oweso amesema.
"Tunakushukuru Sango na Lakairo kwa kutupatia madawati Mungu azidi kuwaongezea , maana watoto wanakaa chini wakija nyumbani wamechafuka nguo zinakuwa vumbi tupu. Tunamuomba Rais wetu Samia atutatulie changamoto ya upungufu wa madawati watoto wanateseka kukaa chini" amesema Magreth.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kogaja, Sylivanus Ochieng Gradus, ameshukuru kwa msaada wa madawati.
" Tumepokea madawati 17 yaliyotolewa kwa shule ya msingi Kogaja, namshukuru sana Sango kwani wapo watu wana pesa lakini hawasaidii maendeleo kwenye vijiji vyetu, tunamuomba asiishie hapa aendelee kutusaidia" amesema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kogaja, Sylivanus Ochieng Gradus akimshukuru Sango Kasera kwa utoaji madawati
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Ikoma Benard Ochieng' Nastory amesema " Tunakushukuru sana Sango kwa tukio hili la madawati.
"Tunachangamoto kubwa ya madawati hivyo tunazidi kukuombea ili uendelee kutukumbuka pamoja na wadau wengine ili watoto wetu waendelee kusoma kwa ubora " amesema Benard.
Kaimu Afisa elimu Kata ya Ikoma ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bugire, Jackson Nyangubo ameshukuru kwa msaada wa madawati huku akieleza changamoto ya ukosefu wa vyoo hali inayopelekea matundu matano kutumiwa na wanafunzi 1, 140.
"Natoa shukrani kwa Sango kwa namna ambavyo ameona uhitaji mkubwa katika elimu, ni kweli tuna upungufu wa madawati yapatao 469 kata nzima. Pia tuna shida sana ya vyoo shule ya msingi Bugire ina matundu matano ya vyoo yanayotumiwa na wanafunzi 1,140.
" Matundu matano yametitia tumepewa tangazo la siku 60 kuhakikisha choo kimejengwa na muda umeisha. Tunashukuru wananchi wamepambana na kuchimba shimo la matundu 12 wanaendelea na utaratibu wa kukusanya fedha japo jamii yetu uelewa bado ni mdogo, tunakuomba Sango kwasababu umeona umuhimu wa elimu tujali kwa hilo pia"amesema Jackson.
Sango akatoa sh. 100,000 kwa ajiri ya ununuzi wa saruji mifuko 5 ujenzi wa choo na kuahidi ushirikiano, kisha akafunga safari hadi nyumbani kwao kata ya Kirogo na kutoa madawati 60 kwaajili ya shule za msingi zilizopo katika kata hiyo.
Sango Kasera (wa pili kushoto) akiwa na viongozi Kata ya Kirogo wakionesha dawati baada ya kuipatia kata hiyo madawati 60
Sango amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika ujenzi wa miundombinu ya elimu ukiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa.
" Rais wetu mama Samia kafanya kazi kubwa ya miundombinu ya elimu, na mimi nimeona nimuunge mkono kwa kusaidia madawati katika shule za msingi kwasababu bado kuna upungufu wa madawati.
Mjumbe wa Mkutano mkuu Taifa CCM, Sango Kasera akizungumza na wananchi wa Kirogo wakati alipofika kukabidhi madawati 60
"Tayali nimeshagawa madawati 510 na zoezi linaendelea. Lengo ni kuzifikia kata zote 26, zoezi hili ni hatua ya kuunga juhudu za Rais Samia, kuunga utekelezaji wa Ilani ya Chama CCM na kuunga mkono mpango wa serikali wa miaka mitano wa kuboresha sekta ya elimu nchini." amesema Sango.
Afisa Elimu Kata ya Kirogo Justine Masau amesema bado sekta ya elimu ina changamoto kubwa ya upungufu wa madawati huku akimshukuru Sango kwa kuwapatia madawati.
Ameongeza kuwa kuna upungufu wa madawati 342 katika shule za msingi zulizopo kata ya Kirogo na kwamba madawati 60 yaliyotolewa yatasaidia kupunguza changamoto ambapo upungufu utakuwa umebaki wa madawati 282.
Diwani Kata ya Kirogo Nyoswede Justine amesema " Tunakukaribisha Kirogo Mjumbe wa mkutano mkuu Taifa ,hii ni moja ya Kata iliyokupa kura nyingi kuhakikisha unapata nafasi ya mjumbe mkutano mkuu Taifa.
"Tunakushukuru kwa namna ambavyo umerudi kutoa shukrani , umetupa heshima ya madawati ,tunashukuru sana hii ndio maana ya chama cha mapinduzi kina mtandao mkubwa wa watu ambao wanashiriki fursa za maendeleo.
Post a Comment