GILBERT NYAMITAH MWENYE ULEMAVU WA VIUNGO AJENGA MADARASA, CHOO
Na Dinna Maningo, Rorya
Gilbert Simon Nyamitah mwenye ulemavu wa viungo, mzaliwa wa kitongoji cha Masara katika kijiji cha Randa, kata ya Kigunga wilaya ya Rorya mkoani Mara, amejenga madarasa mawili, choo cha walimu chenye matundu manne pamoja na kutoa madawati 30 katika shule ya msingi Masara.
Akikabidhi madawati hayo katika uongozi wa shule hiyo, Gilbert amesema kuwa madarasa hayo mawili yalianza kujengwa na wananchi waliochangia Tsh. Milioni sita fedha zilizofanikisha ujenzi kufikia usawa wa madirisha na kisha yeye kuendeleza ujenzi na kukamilisha madarasa hayo.
Gilbert Nyamitah mwenye ulemavu wa viungo aliyejenga madarasa mawili na choo
Pia amejenga choo cha walimu chenye matundu manne huku akimshukuru mbunge mstaafu jimbo la Rorya, Lameck Airo kwa kumlea na kumsomesha.
Gilbert amesema ameamua kulipa fadhila kijijini katika shule alikosoma darasa la kwanza hadi darasa la saba. " Madarasa haya mawili yalianza kujengwa na wananchi wakakomea kwenye usawa wa madirisha, mimi nimeendeleza nikakamilisha boma, nikapaua, nikapaka rangi na kuweka madirisha na milango, vigae na jipsam ndani ya madarasa hayo.
Madarasa mawili yaliyijengwa na Gilbert Nyamitah
"Nimetumia Milioni 30 kukamilisha madarasa mawili na milioni 10 zimetumika kujenga choo chenye matundu 4 na nimetoa madawati 30 . Hii ni shukrani baada ya mimi kulelewa na kusomeshwa na mwanajamii Lameck Airo." amesema Gilbert.
Gilbert amewasihi vijana wenzake, wazee, akina mama, akina baba wasichana wasiache kupambania maendeleo ya shule kwakuwa elimu ndio kila kitu, hivyo wajitahidi kadri wawezavyo wasichoke kwani siku zote penye ugumu ni mwanzo wa kuelekea kwenye wepesi.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Randa waliofika kushuhudia makabidhiano ya madarasa yaliyojengwa na Gilbert Nyamitah
" Walimu najua mnapambana katika mazingira magumu kusaidia ndugu zetu wanaosoma hapa. Niwatie moyo tupo pamoja pale ambapo tutaweza tutafika kusaidia. Najua saizi tumeanza mchakato wa sekondari, ni jambo ambalo limenifurahisha mno, nilifurahi sana niliposikia Masara tumepata sekondari .
Choo cha walimu shule ya msingi Masara kilichojengwa na Gilbert Nyamitah
" Ikikamilika na watoto wetu wakasoma ni kitu ambacho binafsi nitamshukuru Mwenyezi Mungu. Mimi ni mtu mojawapo ambaye nilipata changamoto na kujua uzito wa kuwa na shule ya sekondari umbali wa km 8, sio jambo jepesi.
" Tunapojaribu kujenga sekondari najua wengine watapiga vita , mtapingwa lakini msife moyo mimi kama mwanajamii wenu nipo pamoja na nyie. Niwashukuru wazee wa Masara kwa kunitia moyo na kunipa matumaini" amesema Gilbert.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi Lameck Airo aliyefika shuleni hapo kuzindua madarasa hayo yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi na Gilbert, Mwalimu Amos Dickson ametaja changamoto zinazoikumba shule hiyo.
" Shule ya msingi Masara ina jumla ya wanafunzi 535, kati ya hao wavulana ni 282 wasichana 253 na walimu 8 kati yao 6 wameajiriwa na serikali wawili wameajiriwa na wazazi.
"Shule imefanya vizuri kwenye matokeo kwa miaka mitatu mfululizo. 2021 wanafunzi waliosajiriwa kufanya mtihani walikuwa 48 waliofaulu 42, 2022 waliofanya mtihani walikuwa 42 waliofaulu 28 na 2023 waliofanya mtihani walikuwa wanafunzi 70 waliofaulu wanafunzi 53" amesema.
Mwalimu huyo amesema pamoja na mafanikio hayo shule ina mapungufu " Hakuna mashine ya kudurufu mitihani , nyumba za walimu hazitoshelezi, ukosefu wa tenki la maji chooni , kompyuta kwa ajili ya ufundishaji ,upungufu wa thamani za shule meza, viti, na viti vya walimu.
" Kutokana na changamoto hizo tunaomba utatuzi, tunaomba ukarabati wa majengo makongwe, tunatumaini utapokea maombi yetu na kuyafanyia kazi" amesema Mwl. Amos.
Katika kuunga juhudi za ujenzi wa madarasa, Airo ametoa Tsh. Milioni moja kuchangia ukarabati wa shule ya msingi ya Masara na Tsh. Milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Masara huku akiahidi kuzichukua changamoto hizo kuzifanyia kazi.
Mbunge mstaafu Lameck Airo akizungumza na wananchi
" Ndugu zangu watu wa kushukuru sana ni wazazi wake huyu bwana , wapo wazazi wanazuia watoto wao kutoa misaada kijijini wazazi wenye roho mbaya wanaongoza kwa kupiga simu kwa watoto wao na kuwaambia nisije kusikia umetoa msaada.
"Wazazi wa Gilbert hawajamzuia ameleta umeme kijijini, maji, kajenga madarasa, vyoo vizuri, madarasa haya ni ya kiwango " amesema Lakairo.
Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Rorya, Charles Ochele amesema ni wachache wenye moyo wa kusaidia licha ya kuwepo wengi wenye fedha na hivyo kumpongeza Gilbert kwa kujenga madarasa.
Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Rorya, Charles Ochele akizungumza na wananchi
" Lameck aliniambia kuwa kuna kijana wetu alikuwa anasoma ameamua kusaidia Masara kujenga madarasa mawili. Niwachache wenye moyo wa kutoa, walio na fedha ni wengi mno , ukienda kumuomba hata elfu 10 atajifikilia kutoa.
" Lakini mimi nilivyoalikwa kufika hapa kushuhudia tukio la kukabidhi madawati siwezi kujifikilia kutoa namuunga kijana wetu kwa kuchangia Tsh. 800,000 keshi kwa ajiri ya ukarabati wa shule ya msingi Masara na Tsh. Milioni moja keshi kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Masara. Niwahakikishie tutashirikiana kwenye maendeleo" amesema Ochele.
Mkuu wa shule ya msingi Masara William Peter amemshukuru Gilbert aliyesoma katika shule hiyo kuamua kurudisha fadhila kwa jamii kwa kile kidogo alichokipata.
Mkuu wa shule ya msingi Masara William Peter amemshukuru Gilbert akishukuru ujenzi wa madarasa.
" Niwashukuru wazazi wa Gilbert , malezi mazuri ndiyo yamemfikisha hapa upendo aliooneshwa nyumbani namna ya hukarimu aliouonesha kwa vitendo " amesema mkuu wa shule.
Mkuu huyo wa shule ameomba msaada wa ukarabati wa majengo ili na yenyewe yafanane na madarasa mawili waliyokabidhiwa huku uongozo huo wa shule ukimkabidhi Gilbert cheti cha pongezi kwa ujenzi wa madarasa na choo.
" Pia katika hali ya taaluma tukisema tusubiri michango ya wazazi itatuchukua muda sana kukamilisha, tunaomba pia tusaidiwe mashine ya kudurufu kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mara kwa mara na sisi taaluma ya Masara ipande nimesisitiza hilo" amesema William.
Choo ambacho walimu na wanafunzi walikuwa wanakitumia kabla ya walimu kujengewa choo kipya chenye matundu manne
Gilbert Nyamita wapili kulia akizungumza na wananchi.
Gilbert Nyamitah akiwa katika picha ya pamoja na Walimu, wanafunzi wa shule ya msingi Masara katika darasa alilolijenga.
Madawati yaliyonunuliwa na Gilbert Nyamita yakiwa katika darasa alilolijenga
Baadhi ya wananchi na wanafunzi wakiwasikiliza viongozi
Mbunge mstaafu Lameck Airo akimkabidhi cheti cha pongezi Gilbert Nyamita kilichotolewa na uongozi wa shule ya Masara baada ya kujenga madarasa na choo
Post a Comment