MADEREVA, MAKONDAKTA ZIGO LINALOWATESA WANAFUNZI
>> Ni kutokana na baadhi ya madereva, makondakta wa magari ya shule kujihusisha kimapenzi na wanafunzi
>> Vitendo vya ukatili ndani ya magari ya wanafunzi vyatajwa
>>Wimbi la wanafunzi kusimama ndani ya gari la shule lilivyo kero kwa wanafunzi
Na Daniel Limbe, Geita
MIAKA ya hivi karibuni nchini matukio mengi ya ukatili wa kijinsia,
kimwili, kiakili, kingono na kisaikolojia yamekuwa yakiripotiwa huku yakiwahusisha baadhi ya wanawake, wanaume na watoto.
Kwa tafsiri ya haraka neno "Ukatili" ni kitendo chochote anachofanyiwa mtu au mtoto ambacho kinachoweza kuleta madhara ya kimwili, kiakili, kingono na kisaikolojia.
Baadhi ya ukatili huo umekuwa ukiripotiwa kwenye madawati ya jinsia yaliyopo kwenye vituo vya polisi, taasisi za umma,taasisi zisizokuwa za kiserikali zinazojihusisha na utetezi haki za binadamu,madhehebu ya dini na viongozi wa Kata, vijiji na mitaa.
Kusudio kubwa la kuripotiwa kwa matukio hayo ni kuhakikisha jamii inaishi kwa salama na amani sambamba na kuongeza furaha ya nafsi ambayo ni msingi mkubwa wa maendeleo ya watu, badala ya kuishi kwa hofu na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.
Bila shaka kila nafsi inahitaji utulivu katika harakati za kuyakimbilia maisha bora, lakini yanapotokea mafarakano, migogoro, ugomvi na malumbano mambo huenda kombo na kusababisha ongezeko la umaskini katika jamii.
Mbali na hilo, baadhi ya watu wameathiriwa kisaikolojia, kijinsia, kiakili na kimwili hali iliyosababisha baadhi yao kupata majereha ya kudumu na wengine kukumbwa na vifo, jambo linalopaswa kupingwa kwa nguvu zote pasipo kutazama umri, cheo, jinsia, rangi wala uchumi wa mtu.
Ni kutokana na ukweli kwamba ukatili hufanywa na baadhi ya watu wenye malengo tofauti wakiwemo wenye kuamini imani potofu za kishirikina, tamaa za mwili, kulipiza visasi, madawa ya kulevya na wengine hufanya matendo hayo kutokana na sababu za malezi na makuzi kingali wakiwa watoto.
Mwandishi wa makala hii anazugumzia ukatili kwa watoto unaofanywa na baadhi ya madereva na makondakta wa magari ya kubeba watoto wa shule,kwa kuwabaka na kuwalawiti wawapo mashuleni.
Ni kutokana na baadhi ya vyanzo vya habari kueleza kuwa baadhi ya madereva na makondakta hujihusisha kimapenzi na watoto wadogo kinyume cha sheria za nchi, huku watoto hao wakiogopa kusema hadharani kutokana na vitisho vinavyotolewa na wahusika wa ukatili huo.
Hata hivyo unaweza kujiuliza chimbuko kuu la haya yote linatoka wapi, wakati wa enzi za Babu na Bibi zetu hayakuwepo kwa wingi huo, Je, jamii imepoteza ubinadamu na kushindwa kutoa malezi ya watoto kwa pamoja..? Je, jamii haioni haja ya kupambana na ukatili huo, je jamii imeyachukulia uzito upi mambo haya?
Kwa mtazamo wa haraka unaweza kuona kuwa chimbuko kubwa la mambo haya linatokana na malezi na makuzi ya mtoto, maana wote wanaofanya ukatili huo wanatoka mikononi mwa wazazi waliowalea kabla ya kufikia hatua ya utu uzima.
Itambulike kuwa kila aliye na umri wa utu uzima, ametokana na kuwa mtoto mdogo kwa wazazi wake na kwamba iwapo mzazi hakutimiza wajibu wake wa malezi bora kwa mtoto, matunda ya uharibifu huo ndiyo yanayoshuhudiwa na jamii wakati huu.
Kwa lugha nyepesi ni kwamba watu wanaofanya ukatili huo kwa watoto wadogo, inatokana na malezi mabovu waliyoyapata kutoka kwa wazazi wao na kwamba umefika wakati wa kurejea malezi na makuzi ya Babu na Bibi zetu ili kuinusuru jamii ya sasa na ijayo ili isije kuangamia kwa ukatili unaoanza kuonekana jambo la kawaida.
Ni vyema ifahamike kuwa jukumu la kupambana na ukatili huo, siyo la baadhi ya kikundi cha watu wachache wala Mamlaka flani badala yake jamii yote inapaswa kutambua ukubwa wa madhara yanayoendelea kwa watoto wa shule na kuchukua hatua za haraka kwa wahusika.
Wahenga walisema Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, pia Kidole kimoja hakivunji chawa" misemo yote hiyo inakusudia kuonyesha kuwa ili jambo flani lifanikiwe kwa ufanisi mkubwa ni vyema kushirikiana kwa kuunganisha nguvu za pamoja badala ya watu wachache.
Kutodhibitiwa kwa ukatili huo ni kutengeneza usugu kwa jamii inayoendekeza upuuzi huo hali ambayo ni hatari kubwa kwa kizazi kijacho,na kwamba upo uwezekano wa Taifa kuangamia siku za usoni kutokana na kutokuwepo kwa wazazi na wazalishaji wa baadaye.
Wananchi Geita wafunguka
Makala hii imefanikiwa kuzungumza na baadhi ya wanafunzi wanaotumia usafiri wa mabasi ya shule mkoani hapa (majina tunayahifadhi) wanasema kuna wakati magari hayo hubeba wanafunzi wengi kupita kiasi na kulazimika kubebana, jambo linalosababisha kufika nyumbani wakiwa wamechoka sana.
"Kuna wakati tunabebwa wengi sana kwenye gari na hata wengine kuanza kubebana kutokana na upungufu wa viti vya kukalia, hata hivyo baadhi ya wanafunzi husinzia ovyo ndani ya gari kutokana na uchovu".
"Tunabebana kwa sababu wenzetu wanachoka kusimama na kondakta wa gari la shule anatuambia tuwanyanyue wenzetu na kama wewe haupo tayari kumbeba mwenzako unaambiwa utoke kwenye kiti ili akae mwingine atakaye kubeba"anasema mwanafunzi wa darasa la tatu(shule imehifadhiwa).
Hata hivyo wanakiri kuwa mabasi wanayotumia kwenda shule na kurudi nyumbani hayana usimamizi wa wahudumu tofauti na kondakta na dereva pekee.
Mwalimu mkuu wa shule binafsi ya True Vision, Octavian Mutta, anawataka wamiliki wa shule binafsi kuhakikisha watoto wanabebwa katika mazingira rafiki kabla na baada ya kutoka shule ili kudhibiti unyanyasaji ambao umekuwa ukitajwa kutokea hasa kwa miaka ya hivi karibuni.
Anasema shule yake imeanza kutekeleza maagizo yaliyotolewa na serikali kuhakikisha mabasi ya wananfunzi yanakuwa na wahudumu wawili wenye jinsia tofauti ili kuwalinda watoto dhidi ya ukatili kwa kingono.
"Tunaishukuru sana serikali kuendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa shule ili kuhakikisha maelekezo yanayotolewa na Wizara yanafuatwa ili kupunguza vitendo vya unyanyasaji na ukatili kwa watoto na makundi mengine" anasema Mwl.Mutta
Wapinga vitendo vya kikatili
Katika kukabiliana na ukatili huo baadhi ya taasisi binafsi zimekuwa mstari wa mbele kukemea na kupinga kwa nguvu zote vitendo hivyo ikiwemo taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya NELICO ambayo inapinga baadhi ya ukatili kwa wanafunzi mashuleni.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo inayojihusisha na kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto mkoani humo, Paulina Alex, anasema moja ya haki ya mtoto ni kupata elimu bora,ikiwa ni pamoja na kuwa katika mazingira rafiki ya upatikanaji elimu hiyo.
Mbali na ukatili wa kulawitiwa na kubakwa, Paulina anasema kitendo cha watoto kujazwa wengi kupita kiasi kwenye magari ya shule nao ni ukatili na kwamba baadhi ya watoto hulazimishwa kuyasukuma magari hayo baada ya kuwa yameharibika njiani.
"Ili kukabiliana na ukatili huu inapaswa kila mtu kwa nafasi yake kuhakikisha kuwa mtoto hakumbani na ukatili nje au ndani ya magari hayo na kwamba hilo linawezekana kabisa"anasema
Paulina anaeleza kuwa mpango mkakati wa taasisi hiyo ni kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa na kwamba hawatakuwa tayali kuona zinakanyagwa kwa lengo la kuwanufaisha baadhi ya watu kinyume cha sheria.
"Licha ya kwamba ni jukumu letu kumlinda mtoto lakini pia jamii inawajibu mkubwa sana katika kudhibiti unyanyasaji huu,sambamba na kuimalisha malezi na makuzi ili kuwa na jamii iliyostaarabika na yenye kuthaminiana".
Jeshi la Polosi laanza kuchukia hatua
Katika kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kingono na kujazaji wa wanafunzi kupita kiasi kwenye mabasi ya shule za watoto wadogo vinadhibitiwa, jeshi la polisi limeanza kuchukua.
Hatua hizo ni pamoja na kutoa elimu kwa wamiliki wa shule, watoa huduma za kusafirisha wanafunzi pamoja na waratibu elimu kata.
Mpango huo unalenga kuwa na elimu ya pamoja kati ya wamiliki wa shule binafsi, madereva, makondakta, wasimamizi wa elimu na jamii kwa ujumla ikiwa ni kutafuta mwarobaini wa vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto.
Mkuu wa kitengo cha usalama barabarani mkoani hapa,Nelson Ndifwa, anasema jeshi hilo limeanza kutekeleza kwa vitengo maelekezo ya serikali ya kila basi la kubeba watoto wa shule liwe na wahudumu wawili mmoja wa kike na mwingine wa kiume.
"Tumeanza na utoaji elimu kwa makundi niliyoyataja hapo awali,na tumefikia wilaya zote tano za mkoa wa geita na kuwapatia elimu kupitia vikao mbalimbali na kwamba utekelezaji wake umeanza tangu julai 3 mwaka 2023 na tunaendelea na ukaguzi kwa mabasi yote yanayokiuka sheria na mwongozo halali wa serikali.
"Maelekezo ni kwamba mabasi yote ya kubeba wanafunzi yawe na rangi ya njano, yawe na wahudumu wawili watu wazima wenye jinsia tofauti, na viti lazima viwe na mikanda kwaajili ya usalama wa mtoto"amesema.
"Nitumie fursa hii kuwataka wamiliki wa shule kuacha haraka tabia ya kuwasimamisha watoto ndani ya magari yao, tumeshatoa maelekezo kwa wamiliki wa shule kuhakikisha magari yote yanakuwa na mikanda na watoto wakae kulingana na viti vilivyomo,siyo kubeba zaidi ya uwezo wa gari"anasema Ndifwa.
Aidha anashauri kila shule kuajili Ofisa usafirishaji ambaye atakuwa na jukumu maalumu la kuratibu safari za kila siku kwa mabasi ya shule kwa kuzingatia ratiba ya masomo sambamba na kuhakikisha magari hayo yanafanyiwa uchunguzi wa matengenezo kwa wakati sahihi.
"Ni vizuri wamiliki wa shule wahakikishe wanakuwa na watoa huduma wawili kwenye magari yao,huwezi kusajili wanafunzi wengi halafu una magari machache,tutafuatilia kila hatua, kwani kitendo cha kuwajaza watoto kwenye gari moja huo ni ukatili pia ambao haukubaliki kwa karne huo.
Mkuu wa dawati la jinsia, wanawake na watoto wilayani Geita, Mkaguzi msaidizi wa polisi, Christina Katana, anataja baadhi ya watoto wanaokuwa hatarini zaidi kufanyiwa ukatili wa ngono kuwa ni yule anayetangulia kuingia kwenye gari na anayekuwa wa mwisho wakati wa kurejea nyumbani jioni.
"Mtoto wa kwanza kuingia kwenye gari ndiye anakuwa kwenye hatari zaidi kufanyiwa ukatili kwani anachukuliwa nyumbani mapema, na mtoto wa mwisho anazungushwa kwenye gari zaidi sa saa mbili hadi anachoka, naye yupo kwenye wakati mbaya wa kufanyiwa vitendo hivyo.anasema Katana.
Waraka wa Elimu
Ikiwa ni mpango mkakati wa kukabiliana na ukatili kwa watoto, 28 februari mwaka jana, Serikali kupitia wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia ikalazimika kutoa waraka namba 1 wa mwaka 2023 unaohusu uboreshaji wa huduma ya mabasi yanayotumika kusafirisha wanafunzi.
Waraka huo unawataka wamiliki wa magari ya wanafunzi kuwa na watoa huduma wawili (Ke na Me) ikiwa ni mkakati wa kudhibiti unyanyasaji na ukatili kwa watoto nchini,kutokana na ukweli kwamba dereva na kondakta wake wanaweza kuamua kufanya lolote ikiwemo ukatili wa kingono.
Kwa mujibu waraka huo uliosainiwa na Kamishna wa elimu Tanzania, Dkt. Lyambwene Mtahabwa, unaeleza kuwa thamani ya raslimali mtoto ni kubwa kuliko thamani ya raslimali yoyote ambayo tumejaliwa kubwa nayo nchini.
Mbali na ukweli huo, baadhi ya watoa huduma kwa watoto wamekuwa na tabia zenye mwelekeo wa kuleta mmomonyoko wa maadili, kuathiri ukuaji na ujifunzaji hali inayotishia ustawi wa makuzi ya mtoto kwa ujumla.
Hata hivyo,waraka huo ulianza kutumika machi 1 mwaka 2023,huku wamiliki wa shule wakitakiwa kuhakikisha wanakomesha vitendo vya ukatili kwa wanafunzi wakiwa kwenye magari yao na kwamba kuwe na ratiba rafiki itakayosaidia watoto kupumzika kwaajili ya ukuaji wao.
Kadhalika waraka huo umepiga marufuku kuweka miziki au nyimbo na picha za runinga zinazokwenda kinyume na maadili, mila, tamaduni na desturi za kitanzania.
Majukwaa ya ulinzi shuleni
Mwongozo wa Taifa wa Dawati la Ulinzi na Usalama wa mtoto ndani na nje ya shule wa mwaka 2022 uliotiliwa saini na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu,Dkt. Dorothy Gwajima, umeagiza kuwa na majukwaa ya watoto katika shule za msingi na sekondari yanayoshughulikia masuala ya ukatili.
Lengo kuu ni kumshirikisha mtoto mwenyewe kwenye ulinzi na usalama wake kama ilivyoainishwa katika sera, sheria na mikataba ya kimataifa na kikanda inayohusu uwepo wa mfumo wa usalama dhidi ya vitendo vya ukatili kwa mtoto.
Pia kuimalisha malezi, ulinzi na unasihi kwaajili ya watoto katika shule za msingi na sekondari na kuhakikisha mtoto anapata elimu na ujuzi katika mazingira salama na rafiki bila aina yoyote ya ukatili.
Kwa mujibu wa takwimu za jeshi la Polisi za mwaka 2021 zinaonyesha jumla ya matukio ukatili kwa watoto yaliyotolewa taarifa katika vituo vya polisi nchini ni 11,499.
Mikoa iliyoongoza ikiwa ni Arusha(808) Tanga(691) Shinyanga(505) Mwanza(500) na Ilala(489) na kwamba makosa yaliyoongoza kwa idadi ni matukio ya ubakaji(5,899) Mimba(1,677) Ulawiti(1,114) kukatisha masomo(790) na shambulio la kimwili(390).
Aidha Takwimu za Elimu (BEST 2020) zinaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi wa shule za msingi 1,135 na sekondari 5,340 waliacha masomo kwa sababu ya ujauzito.
Mikoa yenye namba za juu kwa mimba za utotoni kwenye shule za msingi ni Mwanza(98) Tanga(97) Ruvuma(84) Geita(78) na Morogoro(71) wakati kwenye shule za sekondari ni Mwanza(491) Morogoro(389) Dodoma(381) Mara(369) na Ruvuma(327).
Kadhalika Takwimu zinazotokana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 nchini, zinaonyesha kuwa idadi ya watoto walio chini ya umri wa 0-4 ni 9,484,170 huku watoto walio kati ya miaka 5-9 wakiwa ni 8,918,580 sawa na aslimia 42.76 ya watoto wote.
Hata hivyo katika utafiti uliofanywa na shirika la kimataifa la UNICEF mwaka 2011 ulionyesha kwamba kiwango cha ukatili shuleni na nyumbani ni uwiano wa aslimia 40 kwa 60.
Kwa upande wake Mtaalamu wa saikolojia tiba, Saldin Kimangale anasema tafiti nyingi zinazohusu ukatili kwa watoto(Adverse Childhood Experiences) zinaonyesha kubwa watoto ambao hawakupata malezi bora kutoka kwa wazazi.
Watoto waliofanyiwa ukatili, kushuhudia ukatili, kuishi na mwanafamilia mwenye uraibu wa pombe au madawa ya kulevya pamoja na ufukara wako katika hatari ya takribani mara tatu zaidi ya kupata magonjwa ya akili ukilinganisha na wale ambao hawakupitia hali hiyo.
Aidha tafiti nyingi zinabainisha kuwa aslimia 50 ya watu waliotambuliwa kuwa na magonjwa ya akili,waliyapata wakiwa chini ya umri wa miaka 14 lakini hawakutambuliwa mapema.
Inaelezwa kuwa watu wengi wanaopata magonjwa ya akili wamekua katika hatari tangu wakiwa watoto wadogo.
Shirika la Afya Duniani(WHO) limeripoti kuwa aslimia 25 ya watoto wote duniani wanaishi na changamoto ya akili,hali inayosababisha kufanya maamuzi yasiyofaa katika jamii ikiwemo kujiua ambacho ni chanzo cha nne cha vifo vya vijana kati ya miaka 14 hadi 25.
Sheria ya mtoto
Kwa mujibu wa sheria ya mtoto ya mwaka 2009 kifungu cha 13(1) Mtu hatamsababishia mtoto mateso au aina nyingine ya ukatili, kumpa adhabu zisizo za kibinadamu au kumdhalilisha mtoto ikijumuisha mila na desturi zozote zenye madhara kwa mtoto kimwili au kiakili.
Ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kifungu (1) Binadamu wote huzaliwa huru ,na wote ni sawa,(2) Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
Katika Ibara ya 13(1) Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki, bila ubaguzi wowote,kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
Mkataba wa Kimataifa
Mkataba wa kimataifa wa Haki ya mtoto(UNCRC) unazitambua haki za watoto kwa marefu na mapana yake katika nyanja mbalimbali ambazo ni muhimu katika maisha ya binadamu.
Haki zote za mtoto zimewekwa kwenye makundi muhimu matatu(3) ambayo ni kundi la haki ya kulindwa, haki ya kupatiwa mahitaji na haki ya kushirikishwa, ambapo ndani ya makundi haya matatu ndimo haki zote zimazowahusu watoto zimejumuishwa.
Mkataba huu umejikita katika misingi mikuu minne(4) ambayo ni kuyaweka mbele maslahi ya mtoto, kukomesha ubaguzi, kuzingatia maoni ya mtoto katika kufanya maamuzi dhidi ya mambo yanayomhusu pamoja na kukua, kuishi na kuendelezwa.
Kudumishwa kwa haki za mtoto ni kujenga jamii na taifa lenye raia wenye kuheshimiana,wenye uzalendo, fikra chanya,uendelevu,
Inaelezwa kwamba watoto wakithaminiwa, kuheshimiwa na kuendelezwa wakingali wadogo, hukua na ustawi vyema hali inayowawezesha kuifurahia dunia na kuona ni mahali salama pa kuishi.
Nini kifanyike
Baadhi ya wadau wa watoto wanapendekeza jamii kulejea kwenye malezi ya zamani kuwalea watoto kwa ushirikiano na jamii badala ya ilivyo sasa.
Wazazi na walezi wasizidishe mapenzi yanayoweza kuwadekeza watoto kupita kiasi na kwamba wawapatie malezi bora kwa manufaa ya sasa na baadaye.
Serikali iendelee kuwachukulia hatua kali watu wote wanaothibitika kufanya vitendo vya ukatili wa kingono,kimwili,kihisia,kiakili na kisaikolojia.
Jitihada ziongezwe kuhakikisha mabasi ya kubeba watoto yanakuwa na wahudumu wa kike na kiume wakati wa kupanda na wakati wa kushuka ili kuwakinga watoto dhidi ya ukatili kwa baadhi ya madereva na makondakta.
Serikali itenge bajeti ya kutosha ili kuongeza wataalamu wa afya na magonjwa ya akili ili wapatikane kwenye kliniki za huduma ya Baba, Mama na Mtoto (Preventive Measure).
Serikali ihakikishe kila shule ya msingi na sekondari inapatiwa Mshauri nasihi ili kukinga,kulinda na kutoa afua kwa wale wenye mahitaji kwa kuzingatia kwamba umri wote wa watoto tunautumia tukiwa shuleni.
Post a Comment