HEADER AD

HEADER AD

MWANAFUNZI AUAWA KWA KUKATWA MAPANGA NA MWILI KUTELEKEZWA KICHAKANI

Na Alodia Babara, Bukoba

MWANAFUNZI wa darasa la sita shule ya msingi Kilima Elius Antony (13) anadaiwa kuuawa kikatili kwa kukatwa  mapanga shingoni na kisha mwili wake kutelekezwa kichakani katika kijiji cha Kilima  kata Nyakato halmashauri ya  Bukoba mkoani Kagera.

Kamanda wa  Jeshi la Polisi mkoa Kagera Brasius Chatanda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa tukio limetokea Aprili 12, 2024 baada ya mwili wa mtoto huyo kukutwa umetelekezwa kichakani ukiwa na majeraha ya kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu ya shingo.

Amesema mtoto huyo alipotea Aprili 10, 2024 na mwili wake kupatikana ukiwa na majeraha uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha mauaji hayo na ukikamilika jeshi la polisi litatoa ufafanuzi zaidi.

      Kamanda wa  Jeshi la Polisi mkoa Kagera Brasius Chatanda

Mwenyekiti wa Kijiji cha kilima Izidory Kaiza amesema alipokea taarifa ya kupotea kwa mtoto kwenye kitongoji cha Mwizi tangu Aprili 10 kutoka kwa wazazi wa mtoto kwa kushirikiana na wananchi walianza kumtafuta. 

Amesema kuwa walimtafuta siku ya kwanza na ya pili bila mafanikio na siku ya tatu ambayo ilikuwa ni Aprili 12,2024 walifanikiwa kupata mwili wake ukiwa umetelekezwa kichakani na kufunikwa nyasi.

Izidori amesema wakati wakiendelea kumtafuta mama mmoja aliyekuwa anakata nyasi alisema alimuona mtoto huyo akiwa ameshika mfuko wenye rangi ya njano akiwa na kijana ambaye hakumfahamu akiwa ameshika panga wakielekea eneo lenye vichaka lakini hadi mama huyo anafunga nyasi anaondoka anarudi nyumbani hakuwaona tena wanatoka vichakani.

"Tulifuatilia kwa makini eneo ambalo mama huyo aliona wakielekea tulipoingia kichakani tukaona sehemu nyasi zimerundikwa na juu zimejaa nzi tulipokaribia eneo tukaona nguo na mguu na mwili wake.

"Nikatoa taarifa polisi wakafika eneo la tukio wakiwa na gari pamoja na vifaa vya kubebea maiti,kumfunua tukakuta amefariki na alikuwa amepigwa panga shingoni na mbele mara mbili pande zote"amesema Izidori

Beatrida Antony ni mama mzazi wa marehemu Elius Antony, amesema baba yake alikuwa ameenda naye kwenye majukumu yake ya kikazi ya kuchoma mkaa walipofika huko baadaye mtoto alirejea nyumbani kufuata simu na fedha kiasi cha 10,000 kwa ajili ya kununua unga.

“Baba yake alimtuma nimpe fedha ambayo alikuwa ameiacha kwenye koti lake ili apite dukani anunue unga na simu ilikuwa inachajiwa kwenye vibanda vya kuchaji simu hivyo alipotoka nyumbani aliipitia na akanunua unga dukani.

" lakini kabla hajatoka nyumbani aliniomba baada ya kumpelekea baba yake hivyo vitu aende kulala kwa baba yake mkubwa katika kitongoji cha Mwizi kijijini Kilima lakini ilipofika asubuhi nilipiga simu huko nikaambiwa hayupo” amesema Beatrida.

Baada ya kupata taarifa kuwa hayupo kwa baba yake mkubwa mama yake mzazi alitoa taarifa kwa mwenyekiti wa kijiji cha Kilima na juhudi za kuanza kumtafuta zikaanza wakishirikiana na wanakijiji na baada ya siku tatu mwili wake ulipatikana ukiwa na majeraha ya kukatwa mapanga.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kilima Reginah Richard,amesema kuwa, wamepokea kwa masikitiko taarifa za mauaji ya kikatili ya mwanafunzi huyo Elius Antony ambaye alikuwa anasoma darasa la sita katika shule hiyo.

Amelaani vikali wote waliohusika na tukio hilo maana  tangu awepo shuleni hapo alikuwa hajawahi kushuhudia tukio kama hilo la kikatili hilo shuleni hapo.

No comments