HEADER AD

HEADER AD

OFISI YA CCM INAYOJENGWA NA MBUNGE RWEIKIZA KUKAMILIKA DESEMBA




>>Ofisi hiyo itagharimu Milioni 150

Na Alodia Babara, Bukoba

MBUNGE wa jimbo la Bukoba vijijini Jasson Rweikiza, amesema kuwa pamoja na shughuli nyingi za maendeleo anazozifanya kwa wananchi wake pia anaendelea na ujenzi wa ofisi ya chama cha mapinduzi CCM Bukoba vijijini katika kata ya Kemondo ambayo itagharimu Tsh. Milioni 150.

Rweikiza ameyasema hayo jana wakati akiwa mgeni rasmi katika mkutano mkuu maalum wa jimbo la Bukoba vijijini uliofanyika kwa lengo la kutoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa kipindi cha miaka mitatu 2021 hadi 2023 iliyosomwa na mbunge huyo.

Amesema ujenzi wa ofisi umefikia kati ya asilimia 60 hadi 70, huko hatua ya uezekaji na kwamba katika jengo hilo kuna ofisi mbalimbali Uvccm, UWT, Jumuia ya wazazi, ofisi ya mwenyekiti, ofisi ya  katibu wa wilaya na tehama pamoja na ukumbi ambao utakuwa na uwezo wa kubeba zaidi ya watu 200.

  Aliyevaa skafu ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera Nazir Kalamagi akisalimiana na mbunge wa jimbo la Bukoba vijijini Jasson Rweikiza

Amesema ujenzi ulianza June mwaka jana na utakamilika mwishoni mwa mwaka huu, utagharimu Tsh. 150 fedha za ujenzi zinatolewa na mbunge huyo.
 
Ametaja vitu  vingine alivyofanya yeye binafsi kwa wananchi kuwa ni pamoja na kulipa posho za walinzi katika zahanati zilizopo kwenye jimbo hilo kwa mwezi Tsh. milioni 3.1, mashine za kuprint na kutoa kopi shule za sekondari na msingi, televishen 20 maeneo mbalimbali jimboni.

"Ninalipia vingamuzi kila mwezi Tsh. Milioni 2.1, nimegawa gesi katika shule za msingi 147 na sekondari 35, nimejenga uwanja wa mpira Kemondo wenye viwango  nimeuwekea nyasi, nimeweka magori mapya  kwa shilingi milioni 28" amesema Rweikiza. 

Aidha, mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Kagera Nazir Kalamagi amewataka viongozi wa chama kuanzia ngazi ya majimbo hadi vitongoji kubainisha changamoto zilizopo kwenye maeneo yao ili ziweze kutatuliwa kabla ya uchaguzi.

         Wajumbe wakiwa ukumbini

"Nyinyi kama viongozi wa chama katika maeneo yenu, diwani kama kiongozi katika eneo lako inabidi kuanza kubaini changamoto ambazo zipo ndani ya kata zenu kusudi ziweze kufika mahala kama tunaweza kutumia halmashauri zetu ama vikao vyetu kuzitatua kabla ya chaguzi zenyewe" amesema Kalamagi.

Amesema kuwa, wanapokutana kwenye kikao cha pamoja waangalie changamoto za eneo kwa eneo ambazo zisipotatuliwa wananchi wanaweza kukata tamaa na kutowapitisha wagombea wa CCM na au hata wakipita zikatumika nguvu nyingi.

Amewatahadharisha makatibu wa matawi na kata kutoegemea upande wowote hasa kipindi cha kugawa fomu kwa wagombea kwani kufanya hivyo inaweza kusabibisha kupata wagombea wasio na sifa na wasiokubalika kwa jamii na hivyo kuwapa nafasi wagombea watakaotokana na vyama vingine kushinda katika uchaguzi huo.

" Nyinyi makatibu ndiyo mnafahamu watu, tuseme kwamba tukimuweka bwana huyu akasimama CCM tunapita asubuhi, kwa sababu nyie ni viongozi mnajuana, mnajua tukimuweka fulani hatupati lolote, kwa hiyo tuteulieni watu wanaokubalika kwenye maeneo" amesema Kalamagi 

Ameongeza kuwa, Bukoba vijijini hakuna upinzani wa aina yoyote lakini unapofika muda wa uchaguzi wapinzani wamekuwa wakiwapa shida hiyo ni kwa sababu wanakuwa wameteua vibaya.

Kwa upande wake mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa (MNEC) mkoa wa Kagera Karimu Amri Amir amesema kuwa, mtu yeyote anayetafuta madaraka kwa misingi ya dini na ukabira wanachama wa chama cha mapinduzi CCM wampuuze.

      Mjumbe wa mkutano mkuu taifa (MNEC) mkoa wa Kagera Karim Amri Amir akizungumza na wajumbe katika mkutano mkuu maalum Bukoba vijijini

Amewaomba watanzania kuwa na upendo na amani na kuwapuunza watu wanaotaka kuwasambaratisha na  ametoa shukrani nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suruhu Hassan kwa pikipiki nyingi alizotoa mkoa wa Kagera na Tanzania kwa ujumla.

"Shukrani hizo zinahitaji kura za kutosha  kwanza katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwaka kesho, nawaomba sana mzilinde ziendelee kuwepo kwa niamba ya chama cha mapinduzi" amesema Amir.

Hata hivyo Jimbo la Bukoba vijijini ni moja kati ya majimbo mawili ya uchaguzi yaliyopo wilaya ya Bukoba, jimbo hilo lina tarafa nne, kata 29, vijiji 94 na vitongoji 515 ina jumla ya wakazi 322,448.




No comments