ACT WAZALENDO MARA YAISHUKIA SERIKALI INAYOONGOZWA NA CCM
>> Wasikitika Polisi Mugango kuishi kwenye majengo yaliyozeeka
>> Wakwerwa kuona wanufaika wa TASAF wakigeuzwa kuwa makatapila wa kulima barabara
>> Milioni 400 zilitolewa ujenzi kituo cha afya Mugango lakini wananchi wakachangishwa fedha
>>Wawashangaa wanaomchagia fomu Rais Samia mwenye uwezo wa fedha
Na Dinna Maningo, Musoma
CHAMA cha ACT Wazalendo mkoa wa Mara kimeitaka Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi ( CCM) kutatua changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo kukomesha vitendo vya uuzaji holela maeneo ya wazi na wizi wa fedha katika halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini.
Viongozi hao wa Chama cha ACT Wazalendo ngazi za majimbo na mkoa wa Mara, Mei, 26, 2024, wakiwa katika viwanja vya Madukani kijiji cha Kwibara, Kata ya Mugango, jimbo la Musoma vijijini wakieneza Chama na kusajili wanachama, wameikosoa serikali inayoongozwa na CCM kutokana na madhaifu yaliyopo kata ya Mugango na fedha kutafunwa halmashauri lakini serikali haichukui hatua.
Viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo wakiwa katika mkutano wa hadhara kijiji cha Kwibara, Kata ya Mugango jimbo la Musoma Vijijini
Mgeni rasmi katika mkutano huo ambaye ni Katibu wa chama hicho mkoa wa Mara na mjumbe wa kamati kuu ACT Wazalendo Kanda ya Ziwa, Karume Mgunda, ameushukia uongozi wa serikali ya kijiji cha Kwibara, na halmashauri ya wilaya Musoma.
" Mwenyekiti wa kijiji hiki haitishi mikutano ya wananchi, mradi wa maji Mugango- Kiabakari wananchi hawakushirikishwa kwenye mchakato wa mradi huo ,Mwenyekiti wa kijiji anauza kiholela maeneo ya serikali bila kushirikisha wananchi kupitia mikutano " amesema.
Chama hicho kimeshangazwa kwa kitendo cha askari wa jeshi la Polisi Mugango kutokuwa na jengo la kisasa la kituo cha Polisi pamoja na nyumba za kisasa za kuishi askari Polisi na badala yake wanaishi kwenye majengo yaliyokuwa ya kiwanda cha pamba kilichojengwa mwaka 1934 ambayo yamechakaa.
"Mazingira wanayoishi askari wetu hapa Mugango sio mazuri. Polisi wanafanya kazi nyingi wamelundikiwa kazi zingine zisizowahusu. Polisi wamegeuka kuwa wasuluhishi wa ndoa kwenye madawati ya jinsia ya polisi badala ya kulinda raia na mali zake " amesema Karume.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo mkoa wa Mara, Charles Mwera amesema " Nashangaa kuona watu wanakaa kumchangia Rais Samia fedha za fomu kwani aliwaambia kuwa hana uwezo wa kununua fomu? Rais ni tajiri unamchangiaje fedha za kuchukua fomu.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo mkoa wa Mara, Charles Mwera akizungumza na wananchi wa Kata ya Mugango
" Eti viongozi wanaenda kupokea ndege utadhani hiyo ndege ni binadamu kwamba inazungumza kisha wanalipana posho ambazo ni kodi za wananchi , ndege ikija ifike kesho yake ipangiwe safari sio kuandamana kwenda kuipokea " amesema Charles.
Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo Ameongeza kusema " Tunawapa watu madini yetu lakini ndo haohao tena tunaoenda kuwaomba misaada, fedha zinatafunwa ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Musoma hatua hazichukuliwi " amesema Charles.
Katibu Mwenezi ngome ya akina mama ACT Wazalendo mkoa wa Mara, Tekra Johanes amemtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu kuingilia kati mikopo ya kausha damu ambayo imekuwa mwiba kwa wanawake na kuhatarisha ndoa.
" Maisha ni magumu sana kwa wananchi wenye vipato vidogo, akina mama wanakimbia nyumba zao wameacha watoto, kuna watu wamejinyonga, nataka nitume meseji hii mwambieni rais Samia ni mwanamke kausha damu imewaacha watanzania wakiwa hoi.
"Tena wanalalamika kipindi cha mwanamke ambaye ni Rais mwanamke kimekuwa kipindi kigumu kuliko vipindi vyote . Kwa muda uliobaki ajitathimini awaangalie akina mama " anasema Tekra.
Tekra akagusia ubovu wa stendi ya Mugango " Stend ya Jimbo la Musoma vijijini ni mbaya namtumia meseji mbunge wa Musoma Vijijini akae mguu sawa ACT tutatia timu hapa na mgombea ubunge atakayekwenda kutetea jamii ya Musoma Vijijini " amesema.
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo jimbo la Musoma Vijijini Sebastian Makakira, amesema katika kata ya Mugango maeneo ya wazi yameuzwa kiholela huku akilalamika kitendo cha Serikali kutoa fedha Tsh. Milioni 400 ujenzi kituo cha afya Mugango lakini wananchi wakachangishwa fedha.
" Milioni 400 zililetwa na serikali kujega kituo cha afya Mugango lakini wananchi wakachangishwa fedha, tumesomba mchanga, kokoto, mawe, nguvu ya wananchi imetumika asilimia 60 na asilimia 40 ni fedha za serikali.
" Fedha zingine kwenye hiyo Milioni 400 zimeliwa . Maeneo ya wazi yameuzwa hakuna maeneo ya kufanyia mikutano , kule halmahauri fedha zinaliwa" amesema " Sebastiani.
Chama hicho kimekerwa na Kitendo cha wanaufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini ( TASAF) kulima barabara ambapo Katibu wa ACT Wazalendo Jimbo la Rorya Mzee Raphael Igogo amesema.
" Wengine wana uwezo lakini wameingizwa kwenye TASAF wakawaacha wasiojiweza.Watu wana BIMA lakini wakienda hospitali hakuna dawa " amesema .
Mwenyekiti wa Ngome ya Wazee mkoa wa Mara, Yohana Mwikwabe, amesema kwa sasa hali ni mbaya kodi zimepanda, hivyo ACT Wazalendo inataka kuwakomboa wafanyabiashara na wakulima huku akipinga kitendo cha wazee wanaonufaika na TASAF kulima barabara.
" Haki za wazee hazipo , mzee anaenda hospitali apate dawa anaambiwa Bima yake haifanyi kazi. Wazee ambao ni wanufaika wa TASAF wamegeuzwa kuwa matrekta wanalima barabara. Unatoa fedha kwa wasiojiweza na unajua huyo mtu hajiwezi bado unampa kazi ya kulima barabara " amesema.
Mwenyekiti wa Ngome ya akina mama mkoa wa Mara, Pendo Kuboja amewashauri wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi ikiwa ni pamoja na kuwapa fursa za uongozi watu wenye ulemavu.
"Wanawake wenzangu tupambane tujipambanie, kule kwetu wanasema CCM ina wenyewe, sisi huku ACT haina wenyewe ni ya kwetu wote. Akina mama ingieni kwenye siasa inakufunua , inakupambanua na unakuwa na uwezo wa kuhoji" amesema.
Ameongeza " Katika majumba yetu kuna watu wenye ulemavu tumewaficha ndani, watu hawa wana karama kubwa za kutufikisha mbali msiwafiche ndani washirikisheni kwenye siasa " amesema Pendo.
Chama hicho kimewasisitiza wananchi kujisajili katika daftari la wapiga kura kwani bila hivyo hawatapata nafasi ya kuwapigia kura viongozi wanaowahitaji.
Pia kimewasisitiza wanachama kujitokeza kuomba nafasi za uongozi katika serikali za mitaa zikiwemo za uenyekiti wa vitingoji, vijiji na mitaa.
Katika mkutano huo wameshiriki pia viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA) kata ya Mugango ambapo wameishukuru ACT Wazalendo kuwaalika kushiriki mkutano.
Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA) Kata ya Mugango wakisikiliza mkutano wa ACT Wazalendo
Picha za Wanachama wa ACT Wazalendo wakiburudika
Post a Comment