KATIBU UVCCM MARA : SIFANYI KAZI NA WAANDISHI WA HABARI, HUNA MAMLAKA YA KUNIHOJI
Na Dinna Maningo, Rorya
KUMEKUWEPO ukimya katika Ofisi ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Mara juu ya sakata la kuondolewa uongozi Katibu wa Hamasa na Chipukizi wilaya ya Rorya , Emmanuel Paulo Onjiro, hali ambayo imesababisha vijana kugawanyika.
Mwezi Januari, 24, 2024, Onjiro mkazi wa Kata ya Kirogo wilayani Rorya, alikata rufaa kwenda UVCCM mkoa wa Mara akipinga kuhusika na vitendo vya utapeli na ubadhilifu wa mali za watu.
Ni baada ya kuondolewa madaraka ya ukatibu hamasa na chipukizi wilaya ya Rorya na Baraza la UVCCM wilaya hiyo kwa madai ya mienendo mibaya ikiwemo ya utapeli na ubadhilifu wa mali za watu.
Katibu wa UVCCM wilaya ya Rorya, Siri Makanaki ambaye pia amekaimu ofisi ya Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya hiyo alimwandikia barua Onjiro ya kumtaka kutotumia cheo hicho kwa maslahi yake binafsi.
Katika barua iliyoandikwa na katibu huyo wa UVCCM ya Januari, 08, 2024 ilieleza kuwa ofisi ya UVCCM wilaya haina pingamizi na maamuzi ya kikao cha Baraza la vijana cha Desemba, 23, 2023 kilichomwondoa katika nafasi yake kutokana na mienendo mibaya ikiwemo ya utapeli na ubadhilifu wa mali za watu.
Nakala ya barua hiyo ilitumwa pia kwa Katibu wa CCM wilaya hiyo na nyingine ofisi ya Katibu UVCCM mkoa wa Mara.
Tuhuma hizo zilipingwa vikali katika rufaa ya Emmanuel Onjiro huku akimtuhumu katibu UVCCM wilaya hiyo kusuka njama kwa kushirikiana na wajumbe wachache wanaomuunga mkono ambao anasema walimtungia uongo na hivyo kufanikiwa kumuondoa pasipo hata kujadiliwa kwenye kamati ya utekelezaji ya Jumuiya hiyo.
Kufuatia kuwepo mgogoro baina ya viongozi hao wa UVCCM wilaya ambao umesababisha kuwagawa vijana wa UVCCM wilayani humo, Mwandishi wa DIMA Online akawasiliana na viongozi wa chama ngazi ya mkoa kufahamu nini wanachokijua juu ya sakata la Onjiro kuondolewa madaraka, je tuhuma hizo zilizoelezwa katika barua ya katibu wa UVCCM wilaya na Rufaa ya Emmanuel Onjiro zina ukweli gani?
Kauli za Viongozi CCM Mara
Katibu wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Mara Ibrahim M.Ibrahim alipoulizwa kama ofisi yake ina taarifa ya Emmaanuel Onjiro kuondolewa nafasi ya katibu hamasa wilaya ya Rorya anasema suala hilo lipo ofisi ya UVCCM mkoa wa Mara.
" Hilo suala linaanzia kwenye Jumuiya mkoa kisha ndio litakuja kwangu baadae, hivyo halijafika kwangu, mtafute Katibu wa Vijana wa mkoa kwasababu mimi siwezi kuingilia jumuiya wakati halijafika kwangu wao wakimaliza kulishughulikia litaletwa kwangu, ndo utawala bora huo " anasema Katibu Ibrahim.
Mwandishi wa habari wa chombo hiki cha habari akawasiliana na Katibu wa Umoja wa Vijana wa (UVCCM) mkoa wa Mara, Wambura Igembya kufahamu kama ofisi yake imepokea malalamiko ya Onjiro ya kuondolewa uongozi na barua kutoka kwa katibu UVCCM wilaya ya Rorya ya kutokuwa na pingamizi na maamuzi ya Baraza na kama imeshughulikia jambo hilo.
"Unaniuliza wewe kama nani ? kama Mwandishi wa habari kwanini usiulize wilaya iliyomsimamisha ? " Katibu huyo anahoji kisha akakata simu.
Mwandishi wa habari akamtumia ujumbe wa maneno (SMS) akimwomba kueleza nini anachokifahamu katika jambo hilo la kuondolewa uongozi Katibu Hamasa wilaya ya Rorya.
Mwandishi wa Habari : Nimekupigia simu ukaniuliza nasemaje nilivyoanza kukueleza umekata simu.
Katibu UVCCM Mara : Nenda kashtaki Polisi, tena achana na mimi kama umetumwa karibu kwani uliniajili ?
Mwandishi wa Habari : Kumbe mnawathamini waliowaajiri pekee?
Katibu UVCCM Mara : Nenda kashitaki, pia sifanyi kazi na waandishi wa habari nafanya kazi kwa mujibu wa Katiba na Kanuni. Huna mamlaka ya kunihoji wewe, kwanza sikujui, haya sasa nimejitahidi kukujibu, achana na mimi mfate aliyekuajili unipigie simu.
Mwandishi wa Habari : Kama hufanyi kazi na Waandishi wa habari sawa ila Chama chako kinafanya kazi na Waandishi wa habari akiwemo Rais Samia.
Katibu UVCCM Mara: Nimekwambia achana na mimi au umetumwa ? kama unalo nimekwambia karibu aliyekuajili hajakulipa? unataka nini kwangu? sipo tayari na wewe nenda polisi kashtaki nimekataa kuongea na wewe.
Mwandishi wa Habari : Yaishe sio lazima uzungumze ndugu.
Katibu UVCCM Mara : Nenda kashtaki kama unajua hivyo umekazana kunichatisha nini ? naona una lako jambo koma kunitumia sms.
Kanuni ya UVCCM ya mwaka 2017, Toleo la 10, Ibara ya 65 (a) inasema Katibu wa Vijana wa CCM mkoa atafanya kazi zake kwa mujibu wa kanuni za UVCCM na Katiba ya CCM.
(c) Atakuwa na wajibu wa kuitisha mikutano yote ya vikao vya umoja wa vijana wa CCM mkoani kwa kushirikiana na Mwenyekiti.
Mwandishi wa habari hii hadi anawasiliana na Katibu huyo wa UVCCM mkoa wa Mara, Mei, 01, 2024 hakuna kikao kilichoketi cha UVCCM mkoa kujadili kuondolewa madaraka katibu hamasa licha ya ofisi kuwa na taarifa kutoka kwa katibu UVCCM wilaya ya Rorya, katika barua yake ya Januari, 08, 2024 ya baraza kumuondoa madaraka pamoja na barua ya rufaa ya Onjiro ya mwezi Januari, 24, 2024.
Katibu Hamasa azungumza
Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Mara, Leonard Otuoma anakili kufahamu kuondolewa uongozi kwa Katibu Hamasa na Chipukizi wilaya ya Rorya na kwamba alipata nakala ya barua ya Emmanuel Onjiro ya kukata rufaa.
" Kwa utaratibu wa chama barua zote zinazokwenda mkoani zinakwenda kwa Katibu wa Jumuiya, nafikiri katibu ndiye anatakiwa kuita kikao cha kamati ya utekelezaji ili kujadili na kuona kilichotokea Rorya kilikuwa sahihi au siyo sahihi na kama hayo malalamiko yana ukweli au hayana ukweli.
Alipoulizwa kama ana taarifa ya kupendekezwa jina la Katibu Hamasa mpya Alphaxad Mwizarubi katika kamati ya utekelezaji ya wilaya ambaye ni Katibu Hamasa kata ya Ikoma, baada ya Onjiro kuondolewa na Baraza la Vijana na kwa sasa ndiye anakaimu nafasi ya katibu hamasa wilaya anasema;
" Sina taarifa ya kupendekezwa Katibu Hamasa mwingine wilaya ya Rorya, hatuna kanuni inayosema katibu hamasa atateuliwa kwa muda , kanuni inasema katibu hamasa atapendekezwa na Mwenyekiti atajadiliwa kwenye kamati ya utekelezaji na kuthibitishwa na Baraza.
" Kwa hiyo kama yupo katibu hamasa ambaye hajathibitishwa na baraza huyo sio katibu hamasa na mimi sijapata taarifa rasmi za katibu hamasa mpya, sisi tunamjua katibu hamasa aliyekuwepo bado yupo " anasema Otuoma.
Anasema taarifa ya kuondolewa kwa Onjiro ya Katibu Hamasa haijafika kwenye kamati ya utekelezaji zaidi ya yeye kuandikiwa tu barua na katibu wake wa wilaya hiyo, na kupewa nakala.
" Ni swala ambalo ni la kufuatiliwa kujua kama kuna uteuzi mpya wa katibu hamasa, hawezi kuwa katibu hamasa kama hajathibitishwa na baraza " anasema Otuoma.
Akizungumzia suala la utaratibu wa CCM endapo mtu akimlalamikia mwanachama anasema " Anatakiwa kuandika barua kwenda kwenye uongozi ngazi husika, hiyo ndio itatuthibitishia kuwa hayo malalmiko yapo na yanakuwa halali kujadiliwa kwenye baraza tofauti na hapo ni jambo la kufikiria au la mdomo.
"Lazima iwepo barua ya maandishi ya mtu anayelalamika na ingewezekana anatakiwa awepo mlalmikaji na mlalamikiwa wote wasikilizwe kwa pamoja sasa kama kuna jambo limefanyika wakati mwingine linakuwa ni la mkumbo " anasema.
Kiongozi huyo wa hamasa na chipukizi mkoa wa Mara anasema Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Mara, Mary Daniel alikuwa masomoni nje ya mkoa na amesharudi hivyo anaahidi kuwa watalifuatilia suala hilo.
"Nakupongeza kwa kufuatilia kujua kinachoendelea sisi kama jumuiya ya vijana tunahitaji waandishi kama ninyi kuendelea kufuatilia na kuibua maswala mbalimbali.
" Tutaona kama kuna haja ya kufuatilia kama jumuiya ili tushuke huko chini kwenye mabaraza hayo na kamati ya utekelezaji ili kujua ukweli" anasema Otuoma.
Mwenyekiti UVCCM Mara
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Mara, Mary Daniel anasema " Kwa vile amekata rufaa mimi binafsi siwezi kuongea chochote ni jambo ambalo tayari limefika kwenye taasisi tuendelee kuachia vikao kisha tutakupa mrejesho" anasema Mary.
DIMA Online Mwezi Mei , 20 na 21, 2024 imeripoti habari kuhusu sakata la kuondolewa madaraka katibu hamasa na chipukizi wilaya ya Rorya ambapo imezungumza na vijana wa UVCCM na wakaeleza wanachokifahamu kuhusu kuondolewa uongozi Emmanuel Onjiro.
Post a Comment