ZIMU LA MAPENZI LILIVYOSABABISHA VIJANA WA KIKE KUJIONDOA UVCCM RORYA
>> Vijana wa kike wafunguka mazito sababu za kuacha UVCCM
>>Wasema bora Katibu Makanaki wa UVCCM wilaya aondolewe abaki katibu Hamasa wilaya
>>Katibu Makanaki asema ahami Rorya
Na Dinna Maningo, Rorya
BAADHI ya Vijana wa Kike wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Rorya, mkoani Mara wameacha kuendelea na jumuiya kutokana na kulazimishwa kufanya vitendo vya mahusiano ya kimapenzi pamoja na vitisho.
Wakizungumza na DIMA Online, wamesema kwamba wameamua kuachana na shughuli za UVCCM kwakuwa wamechoshwa na vitendo vya Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Rorya, Siri Makanaki kuwataka kimapenzi na wanapokataa huwajengea chuki na kuwatukana huku akiwatishia viongozi wa kike kuwaondoa kwenye nafasi zao za uongozi.
Ikumbukwe kuwa mwezi January, 24, 2024, Katibu Hamasa na Chipukizi wilaya hiyo ya Rorya, Emmanuel Paulo Onjiro mkazi wa kata ya Koryo,
alikata rufaa kwenda ofisi ya umoja wa vijana mkoa wa Mara akipinga kuondolewa nafasi yake ya uongozi na kutohusika na utapeli pamoja na ubadhilifu wa mali za watu.
Ni baada ya Katibu wa UVCCM wilaya ya Rorya Siri Makanaki ambaye pia amekaimu ofisi ya Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya hiyo kumwandikia barua Onjiro ya kumtaka kutotumia cheo hicho kwa maslahi yake binafsi.
Katika barua iliyoandikwa na katibu huyo wa UVCCM Januari, 08, 2024 ilieleza kuwa ofisi ya UVCCM wilaya haina pingamizi na maamuzi ya kikao cha Baraza la vijana la wilaya cha Desemba, 23, 2023 kilichomwondoa katika nafasi yake kutokana na mienendo mibaya ikiwemo ya utapeli na ubadhilifu wa mali za watu.
Onjiro anapinga kuhusika na utapeli na ubadhilifu wa mali za watu na kusema kuwa, kuondolewa kwake zilikuwa ni njama zilizosukwa na Katibu UVCCM wila ambaye aliwashawishi wajumbe kumkataa na kwamba chanzo ni baada ya katibu huyo wa UVCCM wilaya kuwataka kimapenzi vijana wa Hamasa walioshitaki kwake kama kiongozi wa hamasa.
Katika barua hiyo ya Rufaa ya Onjiro amewataja kwa majina baadhi ya wasichana ambao Katibu UVCCM wilaya aliwataka kimapenzi na kumkatalia na hivyo wakamshitaki kwa Onjiro .
Onjiro anasema baada ya vijana hao wa kike kushtaki kwake alilazimika kumweleza katibu UVCCM wilaya malalmiko ya wasichana dhidi yake kitendo kilichomkera na hivyo kumuundia njama za kuondolewa uongozi .
"Juni, 7, 2023 wakati tunaandaa vijana kupokea mwenge alimtaka kimapenzi Zainabu Oketch mkazi wa kata ya Kirogo, huyo dada alilalamika kwangu. Tulipoenda kumpokea aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, Daniel Chongoro kule Mwanza wakati tunarudi binti alilazimika kushuka njiani saa sita usiku kwenda kwao akikwepa kushuka Utegi ili asikutane nae, kitendo kilichompa kero na kuamua kuachana na idara ya hamasa.
" Binti mwingine aliyejitambulisha kwangu kwa jina moja la Roina kutoka kata ya Baraki alishtaki kwangu kwamba katibu Makanaki anamtukana na kumtishia kumwondoa kwenye nafasi yake kisa kamtongoza kamkataa, dada huyo ameshasusa mambo ya chama" anasema.
"Kuna baba wa mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu shule ya sekondari Nyanduga alikuja kulalamika akaniambia nimwambie Katibu Makanaki kuwa aachane na binti yake kuwa anatembea nae nilipomwambia katibu akasema mimi namtangaza mambo yake.
Anaongeza " Tukiwa kambi la vijana Kirogo mwezi Septemba, 2023 Katibu Makanaki alimlazimisha dada anayeitwa Mage wakalale nje ya kambi dada alikataa akaja kuniambia, naye aliamua kuacha jumuiya.
"Pia Jemima Juma ambaye ni mjumbe wa kamati ya utekekezaji UVCCM naye huyo katibu alimtaka kimapenzi, alipomkataa akawa anamtukana na akamtishia kumwondoa kwenye nafasi yake ya uongozi.
" Kitendo cha mimi kuripoti ukatili unaofanywa na katibu UVCCM wilaya dhidi ya vijana hao wa kike kwa uongozi wa chama wilaya kimejenga chuki kubwa sana kati yangu na katibu Makanaki.
" Kitendo hicho kilipelekea Katibu Makanaki kunitishia mara kwa mara na kuapa kuniondoa kwenye nafasi yangu na kuazisha kampeni ya kunizushia uongo kwa wajumbe wa baraza na kuwaambia wasipomuunga mkono kuniondoa basi nafasi zao atazifuta na kweli wakafanya yao nikaondolewa kwenye nafasi yangu" anasema Onjiro.
DIMA Online imezungumza na baadhi ya vijana wa kike na vijana wa kiume wakiwemo wa hamasa na itifaki. Wameeleza manyanyaso ya kijinsia yanayotendwa na katibu Makanaki, huku wengine wakielezwa kutishiwa kuondolewa uongozi.
Vijana wa Kike wafunguka
Zainabu Oketch mkazi wa Kata ya Kirogo anasema " Nahisi mimi ndio chanzo cha Onjiro kukosana na Makanaki. Onjiro ndio alikuwa anatushauri, huyo Makanaki alinihitaji kimapenzi nikiwa natoka Mwanza kwenye ugeni wa aliyekuwa katibu mkuu wa CCM Bwana Chongolo, huyo mbaba alinilazimisha tukutane utegi tulale wote ilibidi nishukie njiani na ilikuwa usiku nikamkwepa.
"Alinisumbua sana ukimkatalia anakutukana matusi ya nguoni nikashindwa kuvumilia ikabidi niache. Kwakweli napenda chama changu ila nitarudi huko UVCCM siku nitakayosikia Makanaki amehama " anasema Zainabu.
Anaongeza kusema " Makanaki anasema eti niligonganisha wanaume sio kweli, wakati tunataka kwenda Mwanza alituambia vijana tukalale kwenye nyumba ya Onjiro Utegi ili tuwahi mapema safari ya mwanza ya mkutano wa Chongoro.
" Alinitumia sms kuniuliza kama nimefika Utegi nikasema bado nikawaambia wenzangu Makanaki akiwauliza kuwa nimekuja Utegi waseme sikuja. Alimuuliza kijana mmoja kama nipo akamwambia sipo ndo akadhani kuwa sikuwepo.
"Mimi nipo tayari kutoa ushahidi hata kama ni mahakamani au kwa Rais Samia, bahati nzuri sms zipo alizokuwa ananitumia wakitaka kuzifuatilia kwa ajili ya ushahidi kupitia namba yangu ya voda na airtel watazipata labda watu wa mtandao wazifute.
" Wanaume ni wengi sasa kwanini nimuonee yeye ? alinitongoza kwa mara ya kwanza tukiwa Utegi kwenye kambi kwa ajili ya kwenda kupokea Mwenge kaya ya Ikoma, hakuacha aliendelea kunifuatilia nikaamua kuacha UVCCM" anasema Zainabu.
Mage Mussa Demba mkazi wa Kata ya Koryo anasema " Huyo Makanaki Katibu wa UVCCM kiuhalisia mimi tabia yake sikupendezwa nayo alinitaka kimapenzi nikamkataa akaanza kunitukana hadi anaunganisha familia yangu kwa hiyo sie wengine tukaona haina sababu ya kuendelea na Jumuiya.
" Unaingia kwenye chama kwa ajili ya uzalendo wa nchi yako lakini unajikuta unaingia kwenye changamoto mwisho wa siku unakuta unamjibu mtu na ni mtu mzima. Kuna kambi tulienda Kirogo lilikuwa kambi la vijana akawa ananisumbua akinitaka nikalale nae.
" Nikamfuata Onjiro nikamweleza kwasababu ndiye alinipeleka kwenye chama, nikamwambia na Katibu Hasama kata ya Koryo wakanishauri nimpuuze. Sikupeleka malalamiko kwa maandishi kwenye chama sikuwa najua huo utaratibu" anasema Mage.
Anazidi kueleza " Makanaki alisema wajaruo wana mambo mengi eti atawaondoa kwenye ofisi yake wabaki makabila. Makanaki ana tabia mbaya hata mkiniita mbele yake nitamwambia anatabia mbaya alisema mimi nafanya kazi ya ukahaba Dar.
"Anatembea na vitoto vidogovidogo hata huyo mdada anayetoka nae ambaye mzazi wake alipeleka malalamiko kwenye chama ni mtoto mdogo anasoma kidato cha tatu shule ya sekondari Nyanduga. Alimsumbua sana hata dada mmoja anaitwa Jemima akawa anamtishia kumuondoa uongozi kisa kamkataa.
"Hata kama wewe ni mzazi umesikia mtoto wako anatoka na yule mzee hautajisikia vizuri. Kiukweli anawaathiri wasichana kisaikolojia kutokana na vitendo vyake viovu " anasema Mage.
Anaongeza " Akikutongoza anakwambia ukimkubali atakutafutia kazi nzuri hata kama huna cheti utapata kazi na atakuweka kwenye kitengo kizuri. Kwahiyo mwili wangu ndio wa kuchezewa nipate kazi wee! kama Mungu amenipangia riziki itapatikana tu sio kwa mwili, alafu eti anasema hanifahamu muongo sana yule mzee.
"Hamasa nitaendelea nayo hata huku Dar nimejiunga, nikirudi Rorya nitaendelea na hamasa ila kama hatokuwepo Makanaki, akiondoka nitarudi tena maana chama langu nalipenda, kijani naipenda sana ila kama ataendelea kuwepo siwezi kutumikia UVCCM Rorya" anasema Mage.
Katibu wa Hamasa na Chipukizi ngazi ya kata ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kulinda nafsi yake ya uongozi anasema" Onjiro hana mambo ya kutongoza tongoza, Makanaki ndiye anatongoza vijana wa UVCCM.
" Kuna kauli anapenda kuisema kwamba yeye ndiye njia ya kupita kwenda kwa baba huwezi kupita popote bila kupita kwake, hata nafasi uliyohitaji bila kupita kwake huwezi kuipata.
" Alimsumbua sana Zainabu hadi akaacha mambo ya kushiriki kwenye mwenge, tulimshauri asiache akasema bora aache kuliko kuendelea kukosana na mtu. Makanaki anatongoza sana vijana wa kike amesababisha wengine kuacha Jumuiya.
Anaongeza kusema " Kama inafika wakati mtu anakwambia huwezi kupata nafasi mpaka ufanyiwe tendo hata mimi ilifika wakati nikataka kuacha uongozi ni baki tu kuwa mwanachama. Hajawahi kunitishia kuniondoa uongozi ila akikutongoza ukakataa jiandae kwa mabango.
"Bora Onjiro abaki Makanaki aondoke maana Onjiro anaelewana na watu wengi yeye ana uzoefu anaweza akakusanya watu pamoja hata kama mlikuwa hamuelewani anawapatanisha mnaelewana kitu ambacho Makanaki hawezi.
" Amesababisha wasichana wengi kwenye kata yangu wamejiondoa UVCCM kwasababu ya matendo yake yanayokera. Ukienda kata ya Koryo ndio inaongoza kwa vijana wengi walioacha Jumuiya " anasema.
Jemima Juma mkazi wa Kata ya Kigunga ambaye ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji UVCCM licha ya kutajwa na baadhi ya vijana wa kike kusumbuliwa kimapenzi na katibu Makanaki na hata kutishiwa kuondolewa nafasi yake ya uongozi anakanusha kutongozwa na Makanaki.
" Sijawahi kukutana na malalamiko ya vijana wa kike wakilalamika kutongozwa na Makanaki au kutishiwa kuondolewa uongozi pengine wanaogopa wanaona aibu kusema hadharani wanabaki kushitaki kwa mtu mmoja mmoja.
"Wakati mwingine katibu Makanaki anapenda utani. Pia jambo la mahusiano ni la siri bila kushirikishwa huwezi kujua kinachoendelea. Wadada wa Rorya hawasemi atamwambia tu mwanamke mwenzake au kijana wa kiume aliye na ukaribu nae lakini kusema hadharani kuwa anatongozwa ni vigumu sana wanaona aibu, mimi sijakutana na hiyo changamoto" anasema Jemima.
Katibu Hamasa Mwingine ngazi ya kata anasema " Makanaki anasema hataki makatibu hamasa wanawake, eti wengine wana mimba, nikajiuliza hii CCM haitaki watu wazae? inataka wakae UVCCM bila kuwa na watoto mpaka umri wa uzee ndio wazae? " anahoji.
Katibu hamasa mwingine ngazi ya kata anasema yeye hawezi kuacha chama kwasababu ya kiongozi kumtaka kimapenzi huku akiwashauri vijana wa kike kurudi kwenye Jumuiya kwakuwa lengo lao ni kukitumikia chama na sio mtu.
" Mimi na Makanaki hatupatani kwa sababu ya mapenzi, yule kwanza sio kijana ni mbabu anakutongoza na ukishakataa anakujengea bifu hata kama mpo kwenye kikao cha Baraza yupo tayari kukutukana kwa mafumbo ila wewe unaetongozwa utajua huyu mtu ananilenga mimi.
" Nimewahi kuwa mhanga wa jambo hili huu mwaka wa tano na uelewe kuwa nina mme, ukikataa anakuchukia alijitahidi sana kunikosanisha na Onjiro, mimi na Makanaki hatupigiani simu .
"Mimi sijawahi kulalamika kwenye chama. Unajua dada huwezi kulalamika maana unahofia kupoteza nafasi uliyo nayo maana akishajua umemsema mahali atakujengea fitina, atakutungia uongo na hata kukutishia kukufukuza uongozi " anasema.
Anaeleza " Mpaka Onjiro kuondolewa kwenye nafasi ni huyo babu Makanaki hata kama alikuwa mkosaji makosa yake hayakuwa ya kutisha, wote ni binadamu kila mtu anateleza anarekebishwa kazi inaendelea.
" Tukiwa kwenye kikao cha Baraza la Vijana Desemba, 2023 Makanaki alitoa kauli kwamba anataka kusimamisha makatibu hamasa wote wanawake maana ni mahawala wa Onjiro. Makatibu hamasa kata tupo wanawake wanne tu kati ya kata 27 za kichama, tunanyanyaswa sana na huyo Makanaki. Makatibu hamasa tulio wengi hatukupenda yule kaka aondolewe uongozi.
Anaongeza kusema kuwa wanawake wanapokuwa kwenye vikao hawana raha na hawachangii hoja kwa kuhofia kutukanwa na Makanaki.
" Yaani unaogopa kusimama kuchangia pointi ukihofia Makanaki atakupondea, akiwa amekutongoza ukakataa ukisimama kuchangia jambo anakupondea unashindwa kuchangia hoja kwenye vikao.
"Pengine ulikuwa na wazo zuri la kujenga Jumuiya unashindwa kulitoa mbele ya wenzako ukimhofia yule mzee Makanaki , na akikupondea anakupondea mpaka unaahibika kila mtu anakucheka. Anakupondea kiutani kumbe anakuchoma kweli. Kiukweli anatuathiri vijana wa kike kwa kiasi kikubwa sana" anasema.
Anaongeza " Unajua sisi wanawake hatupendi kudhalilishwa kwa maneno au kwa vitendo. Ila nawaomba wanawake wenzangu wasikate tamaa , katibu ni mwanadamu na anapita. Mimi siwezi kukata tamaa ningekuwa mtu wa kukata tamaa ningeshakata tamaa kitambo sana, alishanichukia na kujitahidi kunichonganisha na watu wengine lakini sikukata tamaa.
" Wasichana wenzangu msikate tamaa hatuajenda kwenye chama kwaajili ya mtu tunaenda kwaajili ya chama hatuendi kwa ajili ya Makanaki , ananiahibisha sijali japo upande mwingine inatusononesha " anasema kwa huzuni.
Roina Joseph mkazi wa kata ya Baraki alipotafutwa kuzungumza alipokea simu lakini hakuwa tayari kuzungumza hata alipotafutwa mara kadhaa hakusema chochote.
Vijana wa kiume wazungumza
Akizungumzia suala la vijana wa kike wa UVCCM kutongozwa na Katibu Makanaki, Kiongozi mmoja wa UVCCM kata ya Nyamagaro anasema " Makanaki hajatongoza kijana yeyote wa kike, hao wanaosema ni waongo.
"Kati ya watu wanaotumia madaraka yao vizuri ni Makanaki. Sisi kama UVCCM hatujaletewa hayo malalamishi. Kuna watu wanatengeneza migogoro kwa maslahi yao " anasema.
Kiongozi mwingine kutoka kata ya Koryo anasema " Katika kata hii ya Koryo kuna mabinti watatu ninaowafahamu wametongozwa na huyo katibu Makanaki na walileta malalamiko, alipoulizwa alisema hajafanya japo mabinti wana sms zake kama watakuwa hawajafuta alizokuwa akiwatumia za kimapenzi.
"Kata ya Koryo ndio inaongoza kuwa na vijana wengi lakini kutokana na vitendo vya katibu Makanaki vijana wengi wameacha hasa wa kike, tulikuwa vijana 120 vijana wa kike walikuwa wengi zaidi ya vijana wa kiume, walikuwa 78 sasa hivi wamebaki 20.
" Jumuiya inazidi kudorora tunaonekana sisi hatufanyi kazi kumbe kuna kizuizi kinachopelekea jumuiya kuyumba ambaye ni katibu Makanaki. Tunaomba ahamishwe aletwe katibu mpya ambaye anaweza leta mabadiliko katika jumuiya yetu" anasema .
Kiongozi mwimgine wa UVCCM kutoka kata ya Koryo anasema " Mimi nina mke ikifika wakati katibu Makanaki anaenda kumtongoza mke wako inajenga picha gani? ni dharau sana na ni rafiki yangu tunashirikiana mambo mengi.
"Alifanya hivyo lakini sikuwahi kumshitaki kokote wala kumtangaza kwa mtu na katibu wa CCM wilaya Loth ambaye yupo nje ya ofisi kwa matibabu analijua hilo mwanzo mwisho " anasema.
Vijana wa UVCCM walioacha Jumuiya wakiwemo wa kike wanasema watarudi kwenye umoja huo mpaka pale Makanaki atakapohamishwa huku Makanaki naye akisema hawezi kuondoka Rorya hadi atakapotaka yeye.
Kiongozi wa UVCCM kutoka Kata ya Koryo anasema " Makanaki anasema hawezi kuhama mpaka atake mwenyewe sasa na sisi tunasema akikaa kwenye ofisi kwa ukandamizaji anaoendelea nao tutamwachia Jumuiya yake aendelee na wengine sisi ni watu wazima tunajitambua sana " anasema.
Mwandishi wa makala hii akamtafuta mzazi wa mwanafunzi anayedaiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Makanaki majina yanahifadhiwa ambaye ilielezwa kuwa alienda kushitaki ofisi ya chama na kwa katibu hamasa kuhusu katibu Makanaki kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanae ili kufahamu nini anachokijua dhidi ya mwanae licha ya kuahidi kuzungumza lakini alibadili mawazo na kutosema chochote.
Makanaki apinga vikali
Katibu Siri Makanaki anapinga vikali kuhusika na kitendo cha kuwatongoza kwa nia ya kuwataka kimapenzi vijana wa kike hasa wa Hamasa na Itifaki na kusema habari hizo ni za uongo hazina ushahidi.
Ameendelea kusisitiza kuwa Onjiro ameondolea kwa makosa ya kutapeli na ubadhilifu wa mali za watu likiwemo la kuuza kadi ya chipikizi sh. 50,000 wakati hutolewa bure.
"Hivyo ni vitu vya kutunga vile vitoto ukiviangalia siwezi kuvitongoza, mimi nilimuomba Onjiro anipe ushahidi na mkoani walimuomba ushahidi, niliwaambia wasihangaike na hao watano aliowataja kwenye rufaa yake awalete hata wawili lakini hakuleta ushahidi.
"Huyo Zainabu anayesema nilimtongoza si kweli nakumbuka niliwaambia walale Utegi kwa ajili ya kuwahi safari ya Mwanza kwenye ugeni wa Chongoro Zai akagonganisha wanaume nikamwambia hiyo ni fedheha usituletee mambo ya umalaya, nikamwambia nitakuondoa kwenye jumuiya umekuja kugonganisha wanaume" anasema Makanaki.
Makanaki anaongeza kusema " Huyo Mage hata simjui nasikia yupo Dar anafanya kazi za ndani, na huyo wa Baraki simjui na hatuna mtu wa itifaki anayetoka kata ya Baraki, sisi tunachukua vijana wa itifaki kutoka kwenye kata za karibu angalau akilipwa elfu 10,000 anabaki na nyingine maana Jumuiya hatuna mradi hata mmoja.
"Mimi sitembei na mwanafunzi nilidhani unakuja kuniuliza kuwa nimempa mtoto wa shule mimba kumbe unaniambia habari za hao watu wazima wanaojielewa ambao wengine wamezaa wana watoto na wengine wana waume.
"Nina miaka 11 Rorya sijawahi kupata kashfa yoyote ,mimi ninatafuta mizigo iliyoenda shule , mapenzi ni siri ya watu wawili , kutongozwa wanasema lakini kusema nilimpa hawasemi. Sindani kama Onjiro anaweza kupata mwanamke alafu mimi akanikataa " anasema Makanaki.
Anaongeza " Onjiro ana kikundi chake ambacho anajua kitamsaidia. Ile barua yake ya rufaa alikosea kuandika ndio maana unaona barua za wengine zimejibiwa na wameandikiwa wito kufika kwenye kamati ya maadili .
" Nilikuwa namtafuta kwenye 18 ajilengeshe nimkamate, kadi aliyouza kwa 50,000 ndio imemuondolea sifa, tuhuma zingine zote ni mafuta tu . Siwezi kuhama Rorya hadi nitake mwenyewe maana aliyeniajiri ndiye atakayeniondoa Rorya.
" Istoshe Rorya ni pagumu sana watu wanaletwa wanakaa siku chache wanahama, tangu nimekuja Rorya wameshahama makatibu wa CCM wilaya wapatao sita lakini mimi bado nipo hivyo nitaondoka nitakapotaka mimi " anasema Makanaki.
Post a Comment