KATIBU UVCCM RORYA ALIVYOKIUKA KANUNI NA KUTUMIA MADARAKA VIBAYA KUONDOLEWA UONGOZI KATIBU HAMASA
>> Makanaki aitupilia mbali Kanuni ya UVCCM
>> Uchunguzi uliofanywa na DIMA Online umebaini
Na Dinna Maningo, Rorya
SIKU chache zilizopita DIMA Online imeripoti habari kadhaa juu ya Katibu Hamasa na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi ( UVCCM) wilaya ya Rorya, mkoa wa Mara, Emmanuel Paulo Onjiro kuondolewa nafasi yake ya uongozi na Baraza la Umoja wa Vijana la wilaya kwa tuhuma za utapeli na ubadhilifu wa mali za watu.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi ( UVCCM ) wilaya ya Rorya, Siri Makanaki amekaimu pia ofisi ya Katibu wa CCM wilaya ya Rorya kutokana na Katibu wa wilaya hiyo, Loth Hilemeirut ni mgonjwa na yupo nje ya ofisi kwa matibabu. Pia Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Rorya Junior Lameck Airo yupo masomoni nje ya nchi.
Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Katibu wa UVCCM Siri Makanaki ya Januari, 8, 2024 , katibu huyo amemzuia Emmanuel Onjiro kutumia cheo cha Katibu hamasa kwa manufaa yake binafsi.
Makanaki anaeleza kuwa Baraza la vijana lililoketi, Desemba, 23, 2023, ofisi ya CCM wilaya lilipitia mienendo ya Onjiro kama kiongozi wa ngazi ya juu ikiwemo ya utapeli na ubadhilifu wa mali za watu kwa nyakati tofauti tabia ambayo ilipelekea kikao cha Baraza kumuondoa kwa kura 101 kati ya kura 108 za wajumbe waliohudhuria kikao hicho.
Katibu UVCCM katika barua hiyo anasema kuwa kikao kilichomvua madaraka ndicho kilichompatia wadhifa huo hivyo ofisi haina pingamizi na maamuzi ya kikao cha Baraza ya kumwondoa ukatibu hamasa.
Hata hivyo, Emmanuel Paulo Onjiro Januari, 24, 2024 alikata rufaa kwenda ofisi ya UVCCM mkoa wa Mara na nakala kwenda kwa Katibu wa CCM wilaya ya Rorya, Katibu Hamasa Taifa na Katibu mkuu UVCCM Taifa.
Katibu uhamasishaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Rorya, Emmanuel Paul Onjiro aliyeondolewa uongozi
Onjiro anapinga tuhuma zilizoelekezwa kwake za utapeli na ubadhilifu wa mali za watu mbalimbali huku akimtuhumu Katibu Makanaki kuwa alifanya njama na genge lake yeye kuondolewa uongozi.
Pia Vijana wa Umoja wa Chama cha Mapinduzi wilaya, Kata na Matawi wakiwemo vijana wa hamasa, itifaki, makatibu, wenyeviti na viongozi wa chama pamoja na baadhi ya viongozi wa UVCCM mkoa wa Mara wamezungumza na chombo hiki cha habari.
Vjana wa UVCCM wameeleza wanachokifahamu juu ya utata uliopo wa kuondolewa madaraka katibu hamasa. Hali ya uhai wa jumuiya, na changamoto zinazowakabili vijana wa UVCCM wakiwemo vijana wa kike, habari zilizoripotiwa siku chache zilizopita katika chombo hiki cha habari.
Uchunguzi uliofanywa na DIMA Online
DIMA Online imefanya uchunguzi wa tuhuma zilizoelekezwa kwa Emmanuel Onjiro na zilizoelekezwa kwa Siri Makanaki na kubaini haya ;
Uchunguzi umebaini kuwa tangu ofisi ya UVCCM wilaya ya Rorya kuandika barua Januari, 08, 2024 kwenda ofisi ya UVCCM mkoa wa Mara kutaarifu maamuzi ya Baraza ya kumuondoa madaraka katibu hamasa wilaya, na Emmanuel Onjiro aliyeondolewa madaraka kuandika barua ya rufaa Januari 24, 2024 kwenda ofisi ya UVCCM mkoa wa Mara, UVCCM Mara haijashughulikia barua hizo.
Imebainika kuwa licha ya Onjiro kukata rufaa kwenda ofisi ya UVCCM mkoa wa Mara, uchunguzi umebaini kuwa hadi Mwandishi wa habari wa DIMA Online anakamilisha uchunguzi wa makala hii Mei, 3, 2024, Ofisi ya UVCCM mkoa wa Mara imekaa kimya haijafanya kikao chochote kujadili rufaa ya Onjiro.
Kwa mujibu wa Kanuni ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM ), Ibara ya 65 (a) inasema Katibu wa Vijana wa CCM mkoa atafanya kazi zake kwa mujibu wa kanuni za UVCCM na Katiba ya CCM.
(c) Atakuwa na wajibu wa kuitisha mikutano yote ya vikao vya umoja wa vijana wa CCM mkoani kwa kushirikiana na Mwenyekiti.
Pia Kanuni ya UVCCM Ibara ya 57 inasema katibu wa Vijana wa CCM wilaya atafanya kazi zake kwa mujibu wa kanuni ya UVCCM na Katiba ya CCM na atakuwa na wajibu wa kuitisha mikutano yote ya umoja wa vijana wa CCM wilaya kwa kushirikiana na Mwenyekiti na atakuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya CCM wilaya.
Uchunguzi umebaini kuwa Katibu wa UVCCM wilaya ya Rorya, Siri Makanaki amekiuka utaratibu wa vikao ambapo baadhi ya watu wasio wajumbe halali walishiriki Baraza la vijana la wilaya lililoketi Desemba, 23, 2023 lililofanya maamuzi ya kumuondoa Onjiro katika nafasi yake ya katibu hamasa na chipukizi wilaya.
Kwa mujibu wa Kanuni ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Ibara ya 54 inasema Baraza la Vijana wa CCM la wilaya litakuwa na wajumbe ambao ni Mwenyekiti wa vijana wa CCM wilaya, katibu wa vijana wa CCM wa wilaya, wajumbe 3 wa Baraza la wilaya waliochanguliwa na mkutano mkuu wa wilaya.
Mwenyekiti wa Chipukizi wa wilaya, katibu wa uhamasiahaji na chipukizi wa wilaya, katibu wa CCM wilaya na mwakilishi wake, wajumbe wawili wa baraza la mkoa waliochaguliwa katika wilaya hiyo, mjumbe mmoja kutoka kila Jumuiya ya CCM, wajumbe waliochaguliwa na mkutano mkuu wa wilaya.
Wengine ni Wenyeviti wa vijana CCM Kata, makatibu wa vijana wa CCM Kata, mjumbe mmoja mmoja wa kuwakilisha umoja wa vijana katika jumuiya zinazoongozwa na CCM, mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilaya anayetokana na umoja wa vijana wa CCM.
Pia Wenyeviti wa chipukizi wa Kata, Makatibu uhamasishaji na chipukizi wa kata, Wenyeviti wa UVCCM wa majimbo, makatibu wa UVCCM wa majimbo, makatibu wa uhamasihaji na chipukizi wa majimbo pamoja na wajumbe wawili wa kuwakilisha jimbo kwenye wilaya.
Imebainika kuwa katibu Makanaki alikiuka kanuni hiyo kwa kumwalika katibu wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Kyangasaga, Ramadhani Mabari kuandika mhitasari wa kikao cha Baraza. Mery Mbogo ambaye ni Katibu Mhitasi ofisi ya CCM wilaya ya Rorya (PS) si mjumbe lakini alishiriki kikao.
Uchunguzi umebaini kuwa katika kikao cha Baraza kilichomuondoa madaraka Emmanuel Onjiro, walishiriki vijana wa itifaki (Green Guard) kutoka Kata ya Koryo wasio wajumbe halali wa Baraza la vijana ambao ni Norah Patrick Igogo, Damaris Kelvin Odongo,Godfrey Joseph Lazaro, Kalonzo Samwel Kalonzo, Jacob Matara, Grace Joseph Opanga, Pamela odongo Charles, Christina Justin Owuor, Jofrey J. Matara.
Wengine ni mjumbe wa kamati ya siasa wilaya ambaye pia ni afisa tehama wilaya ya Rorya, Levina Simba huku jina la Joshua S. Peter likionekana kwenye orodha ya mahudhulio ya wajumbe walioshiriki baraza licha ya kutokuwepo katika kikao hicho.
Uchunguzi wa DIMA Online umebaini kuwa katika kikao hicho cha Baraza, Katibu UVCCM wilaya hakuwatamkia hadharani wajumbe idadi ya kura zilizopigwa za kumkubali au kumkataa Onjiro.
Katika kikao hicho kiligubikwa na vurugu kutokana na baadhi kutaka Onjiro apewe onyo, wengine kutaka asamehewe na wengine kutaka aondolewe madaraka.
Imebainika kuwa kabla ya kikao cha Baraza la vijana la wilaya kuketi inatakiwa ajenda za kikao zijadiliwe kwenye kikao cha kamati ya utekelezaji ya UVCCM wilaya lakini hakikuketi na hivyo kikao cha Baraza la Vijana kuketi kabla ya kufanyika kikao cha kamati ya utekelezaji.
Uchunguzi wa DIMA Online umebaini kuwa katika kikao hicho cha Baraza la Vijana, Katibu wa UVCCM wilaya Makanaki hakuwasomea wajumbe ajenda zinazopaswa kujadiliwa kwa mtiririko kwa mujibu wa taratibu za vikao isipokuwa alikuwa anasimama na kuzungumza jambo moja kisha anahama na kuzungumza jambo lingine ambapo kubwa zaidi yeye na baadhi ya wajumbe walijikita katika kumjadili Onjiro ajenda ambayo haikuwepo bali iliibuliwa kikaoni.
Uchunguzi umebaini kuwa utapeli na ubadhilifu wa mali ulioelezwa na mjumbe Alphaxad Mwizarubi mbele ya wajumbe wa Baraza hauna uthibitisho wa kutosha.
Hakuna barua iliyooneshwa kwa wajumbe wa Baraza kuwa Samson Mkurunzi maarufu Nyasembo aliyedaiwa kutapeliwa na Onjiro amewahi kumlalamikia Onjiro ofisi ya serikali ya kijiji, Kata, Polisi au kwenye chama kuwa amemtapeli pesa au mali.
Mwandishi wa DIMA Online akiwa anazungumza na katibu UVCCM wilaya hiyo Siri Makanaki, alimtuhumu Onjiro kuiba na kuharibu mali za chama, kumtapeli Nyasembo Tsh. Milioni 2.9 na kuuza kadi ya chipukizi ya mtoto wa Nyasembo Tsh. 50,000.
Hata hivyo, hakuna barua za kiofisi za maandishi za watu au chama zikionesha onjiro amewahi kulalamikiwa kwa utapeli na ubadhilifu wa mali au barua za onyo lolote ambalo chama au Jumuiya imewahi kumuonya kutokana na tuhuma za utapeli au ubadhilifu wa mali za watu.
Katibu UVCCM wilaya alipoulizwa kuwa kwanini Onjiro hakuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili awajibishwe kwa makosa yake alisema Chama huwa hakiwapeleki wanachama wake polisi, isipokuwa huyamaliza kichama zikiwemo adhabu, lakini hakuweka bayana adhabu alizowahi kupewa Onjiro kabla ya kuondolewa madaraka.
Katibu huyo wa UVCCM wilaya alitolea mfano wa adhabu kwa kuonesha barua iliyokuwa ndani ya bahasha ikiwa na maandishi juu ya jina la Sango Kasera na bahasha za viongozi wengine wa chama, na kusema barua hizo ni za wito wa watu hao wanatakiwa kufika kwenye kamati ya maadili na usalama lakini hakuonesha barua ambazo Onjiro amewahi kushtakiwa kwa utapeli au kuitwa kwenye kamati ya maadili.
Akizungumza na DIMA Online Katibu huyo wa UVCCM wilaya alimwambia mwandishi wa makala hii kuwa nafasi ya ukatibu hamasa haikatiwi rufaa, kwamba mtu akishaondolewa madaraka anatakiwa kukaa kando, hivyo Onjiro alikosea kukata rufaa na ndiyo sababu hadi sasa rufaaa yake imetupiliwa mbali na UVCCM mkoa wa Mara na hata Taifa bila kufanyiwa kazi .
Kauli hiyo ya Katibu wa UVCCM ni ya ukiukwaji wa Kanuni ya UVCCM Ibara ya 13 (e) inayompa haki mwanachama wa jumuiya hiyo kukata rufaa katika kikao cha juu yake endapo hakuridhika na uamuzi uliotolewa.
Mwezi Januari, 2024 baada ya kikao cha baraza la vijana la wilaya kumwondoa madaraka Onjiro, Katibu wa UVCCM Makanaki aliitisha kikao cha kamati ya utekelezaji ya wilaya na kumpendekeza Katibu wa Hamasa kata ya Ikoma Alphaxad Mwizarubi kuwa Katibu mpya wa hamasa wilaya atakayekwenda kuthibitishwa na baraza la vijana litakalofanyika hivi karibuni ambaye hata hivyo wajumbe wa kamati ya utekelezaji walimkataa.
Mwizarubi ndiye aliyeibua hoja katika baraza la vijana lililomuondoa madaraka Onjiro akimtuhumu kumtapeli fedha na mali mwanachama wake wa kata ya Ikoma Nyasembo pamoja na kuuza kadi ya chipukizi Tsh. 50,000 tuhuma ambazo hazina ushahidi wa nyaraka yoyote.
Kuna uwezekano wa kufanyika njama za kumwondoa Onjiro kwenye nafasi yake zilizofanywa na katibu UVCCM wilaya ya Rorya kushawishi wajumbe kumuondoa madaraka kijana huyo.
Imebainika kurekodiwa kwa mazungumzo ya sauti baina ya Makanaki na baadhi ya wanaccm akijigamba kuwa yeye ni kiongozi mkubwa anao uwezo wa kutafuta watu wanne wenye nguvu wa kumuunga mkono ili kummaliza Onjiro na kusema kuwa ndicho kilichofanyika kwenye baraza la wilaya lililomuondoa madaraka.
Katibu huyo alisikika akisema kuwa yeye ndio bosi wa vijana, katibu wa uhamasishaji ni kataasisi kadogo hivyo ana uwezo wa kumuondoa Onjiro kwakuwa yeye ndio mwenye baraza na kwamba yeye ndie aliyeshawishi baraza kumuondoa.
" Mimi ndio nilishawishi baraza kwakuwa tulikuwa tunajua nguvu yake ni kubwa watu watampa hela, tukamzunguka tukakaa kimya alafu likazuka kwenye baraza, inamana alikuwa hana uwezo wa kufurukuta " Makanaki alisikika akisema.
Kuhusu kadi ya chipukizi ambayo mjumbe mmoja kwenye kikao cha baraza alieleza kuwa Onjiro kamuuzia mtoto wa Nyasembo kadi ya Chipukizi Tsh. 50,000 madai hayo ni ya uongo, kwani fedha hizo Onjiro alimuomba Nyasembo kwa ajili ya kudurufu fomu za uchaguzi wa chipukizi na gharama za usafiri kuzipeleka ofisi ya CCM mkoani Mara.
Imebainika kuwa katibu Makanaki alisikika akizungumza kwa njia ya simu na Onjiro akimuomba fedha kiasi cha Tsh 30,000 kati ya kiasi hicho cha Tsh 50,000, sauti hiyo ya mazungumzo tunayo.
Katibu Makanaki aliponyimwa kiasi hicho cha fedha ndipo alimzushia uongo kwa baadhi ya wajumbe kuwa ameuza kadi ya chipukizi Tsh. 50,000 ambapo katika kikao cha baraza mjumbe mmoja aliibua hoja ya kuuzwa kadi ya chipukizi kwa Tsh 50,000 ili kuhalalisha utapeli uliopelekea Onjiro kuondolewa uongozi.
Uchunguzi wa DIMA Online umebaini kuwa katika kikao cha kamati ya utekelezaji cha UVCCM wilaya kilichofanyika Januari, 2024 kwa ajili ya kupendekeza jina la katibu hamasa mpya wa wilaya, vijana wawili walishiriki kikao hicho ambao si wajumbe halali.
Vijana wa UVCCM walioshiriki kikao hicho na si wajumbe halali ni Jophrey J. Matara ambaye ni mkuu wa mafunzo kata ya Koryo pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM kata ya Nyamagaro Hindia Manzu pesa.
Wajumbe halali wa kamati ya utekelezaji walioshiriki kikao hicho ni Jemima Juma, Elisha Joseph, Joseph Charles ambaye ni Mwenyekiti wa Chipukizi wilaya na katibu wa UVCCM wilaya Siri Makanaki.
Katika kikao hicho cha kamati ya utekelezaji Mwenyekiti wa kikao alikuwa ni katibu wa UVCCM wilaya Siri Makanaki wakati huo huo akishiriki pia kama katibu wa kikao hicho.
Kikao hicho kilikiuka Kanuni ya UVCCM Ibara ya 55 ambayo inasema kutakuwa na kamati ya utekelezaji ya umoja wa vijana kwa kila wilaya, kamati hiyo itakuwa na wajumbe ambao ni Mwenyekiti wa vijana wa CCM wa wilaya, katibu wa vijana wa CCM wa wilaya.
Wengine ni wajumbe wawili wa kamati ya utekelezaji ya wilaya waliochanguliwa na baraza la vijana wa CCM la wilaya kutoka miongoni mwa wajumbe watatu wa baraza la vijana wa CCM la wilaya, katibu wa CCM wilaya au mwakilishi wake, katibu wa uhamasishaji na chipukizi wa wilaya pamoja na mwenyekiti wa Chipukizi wilaya.
Ibara ya 58 inasema Katibu wa uhamasishaji na Chipukizi atateuliwa na kamati ya utekelezaji ya vijana wa CCM wa wilaya na kuthibitishwa na Baraza la vijana wa CCM wilaya. Atakuwa ndiye msimamizi mkuu wa shughuli zote za chipukizi, uenezi, uhamasihaji, sera, utafiti na mawasiliano chini ya katibu wa umoja wa vijana wa CCM wilaya.
Kanuni inasema Katibu Hamasa atawajibika kwa baraza kuu la umoja wa vijana wa CCM wa wilaya kwa kazi na shughuli zake zote na atakuwa mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya vijana wa CCM wilaya.
Kuhusu Makanaki kutumia vibaya madaraka yake kuwataka kimapenzi vijana wa kike wa UVCCM na kuwanyanyasa kwa kuwatolea maneno ya fedheha, baadhi ya vijana wa kike wamekiri katibu Makanaki kuwataka kimapenzi ambapo Makanaki aliwatongoza kupitia mazungumzo ya ana kwa ana na kwa njia ya ujumbe wa maneno ( SMS ) jambo ambalo limesababisha baadhi yao kuacha jumuiya.
Uchunguzi umebainika kuwa vitendo vya vijana wa kike wa UVCCM kutongozwa na kiongozi huyo havijawahi kuripotiwa kwa maandishi katika ofisi za chama wilaya au UVCCM ngazi ya Kata au Tawi. Wanaolalamika kutongozwa huishia kulalamika kwa mdomo kwa viongozi wa UVCCM kata na kwa kiongozi wa Hamasa na Chipukizi wilaya ambaye ameondolewa uongozi.
Sababu ya kutoshitaki kwa maandishi ili kujadiliwa kwenye vikao vya juu vya chama ni kutokana na kuliona jambo hilo kama ni fedheha kwao na aibu wao kujadiliwa kwenye vikao, wengine huishia tu kusema kwa wasichana wenzao huku baadhi yao wakilazimika kuficha ili waume zao wasifahamu kwakuwa wakifahamu basi wanaweza kuwazuia kuendelea na Jumuiya hiyo.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya vijana wa kike kuogopa kutoa maoni yao mbele ya vikao kutokana na kiongozi huyo wa UVCCM wilaya kuwatolea matamshi yanayowafedhehesha baada ya kukataliwa kimapenzi.
Vijana hao wa kike wanakosa haki ya kutoa maoni kwa mujibu wa Kanuni ya UVCCM Ibara ya 13 inayosema kila mwanachama atakuwa na haki ya kuhudhulia na kutoa maoni katika mikutano yote ya umoja wa vijana wa CCM pale ambapo mwanachama anahusika kwa mujibu wa kanuni.
Katika kikao cha baraza la vijana cha Desemba, 23, 2023 lililomuondoa Onjiro, katibu huyo wa UVCCM wilaya aliwatishia kuwaondoa uongozi makatibu hamasa wanawake ngazi ya kata kwamba wamekuwa wakimtetea Onjiro licha ya kwenda kinyume na taratibu za UVCCM jambo ambalo ni kinyume na Kanuni ya UVCCM ibara ya 13 inayompa haki mwanachama kutoa maoni.
Ibara ya 8 ya Kanuni ya UVCCM inasema miongoni mwa kazi za umoja wa vijana wa CCM ni pamoja na kutetea na kudumisha haki na maslahi ya vijana katika fani mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Vijana wa Jumuiya hiyo wamekuwa hawatendewi haki na viongozi wa jumuiya hiyo ngazi ya wilaya kwani wanapokuwa kwenye ziara za mwenge na ziara za viongozi wakati mwingine hawalipwi chochote na hata wakilipwa baadhi huambulia posho ya Tsh. 5000 - 10000 kwa shughuli waifanyayo kutwa nzima.
Pia uongozi wa Jumuiya ngazi ya wilaya umekuwa hausomi mapato na matumizi ya fedha za jumuiya inazopata zimiwemo za michango inayotolewa na wadau mbalimbali kufanikisha shughuli za Jumuiya.
Kumekuwa hakuna uwazi juu ya fedha zinazotolewa na viongozi wakati wa ziara zao kama zawadi maarufu posho ambapo viongozi wachache wa jumuiya hunufaika na fedha hizo huku wengine wakikosa chochote jambo ambalo ni kinyume na Kanuni ya UVCCM.
Mfano, wakati wa Ziara ya Makamu Mwenyekiti Abdulrahman Kinana alipofika Musoma kikazi vijana walipewa posho kama zawadi ambapo Katibu Hamasa aliyeondolewa madarakani alipewa sh. 110,000 kuwagawia vijana wa hamasa na itifaki walioshiriki kwenye mkutano wake lakini baadhi ya vijana hawakupewa posho hiyo.
Uchunguzi umebaini kuwa vijana wa UVCCM wamekuwa wakijituma katika Jumuiya lakini pindi wanapopewa fedha kama zawadi ama posho hudhulumiwa na baadhi ya viongozi wa Jumuiya. Mfano, hivi karibuni baadhi ya Vijana wa UVCCM walienda Musoma kupakia pikipiki kwenye gari zilizotolewa na Rais Samia kwa ajili ya makatibu wa Chama cha CCM.
Pikipiki zilisafirishwa na kushushwa ofisi ya CCM wilaya iliyopo Utegi ambapo kiongozi mmoja wa CCM wilaya ya Rorya alitoa kiasi cha fedha ili vijana walipwe lakini Katibu wa UVCCM wilaya aliwadhulumu fedha baadhi ya vijana huku baadhi yao wakiambulia sh. 5000.
Ibara ya 10 ya kanuni ya UVCCM inamtaka kijana kutotoa wala kupokea rushwa au mapato mengineyo kwa kificho. Ibara ya 18 (a) inasema ni mwiko kwa kiongozi wa umoja wa vijana wa CCM kutumia madaraka aliyopewa kwa manufaa yake binafsi au kwa upendeleo au kwa namna yotote ambayo ni kinyume na lengo lililokusudiwa na madaraka hayo.
(c) Ni mwiko kwa kiongozi kupokea mapato ya kificho, kutoa au kupokea rushwa au kushiriki katika mambo yoyote ya magendo.
Ibara ya 96 inasema umoja wa vijana utakuwa na mapato kutokana na kiingilio na ada za wanachama wake pamoja na mapato mengine yanayotokana na shughuli mbalimbali pamoja na michango ya hiari iliyochangishwa kwa madhumuni yoyote yaliyohidhinishwa na vikao.
Kwa mujibu wa Ibara ya 15 ya Kanuni ya UVCCM inasema kiongozi wa umoja wa vijana wa CCM ni mwanachama mwenye dhamira yoyote katika jumuiya aliyokabidhiwa kwa mujibu wa kanuni na Katiba ya CCM.
Pia awe mwadilifu, mkweli na mwaminifu kwa umoja wa vijana wa CCM na Chama cha Mapinduzi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Post a Comment