HEADER AD

HEADER AD

VIJANA UVCCM RORYA WAGAWANYIKA KUONDOLEWA UONGOZI KATIBU HAMASA WILAYA


>>Wengi wasema taratibu za vikao hazikufuatwa 

Vijana wamshukia Makanaki Katibu wa UVCCM wilaya ya Rorya

>Wakerwa na kauli yake  " Mimi ni Alfa na Omega hakuna mtu anayeweza kufika kwa baba bila kupitia kwangu "

>>Dhuluma za posho ziara,mikutano ya viongozi, mwenge kilio kwa vijana wa Hamasa, Itifaki

Na Dinna Maningo, Rorya

HALI ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Rorya, mkoani Mara sio shwari kufuatia kuwepo kwa mgawanyiko wa vijana baada ya aliyekuwa Katibu wa Hamasa na Chipukizi wilaya ya Rorya, Emmanuel Paulo Njiro kuondolewa madaraka.

Mwezi Januari, 08, 2024, katibu wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Rorya, Siri Makanaki alimwandikia barua  Emmanuel Onjiro ya Maazimio ya Baraza la Vijana wilaya ya Rorya la Desemba, 23, 2023 lililomuondoa kwenye nafasi ya Katibu wa Hamasa na Chipikizi (W).

       Katibu wa UVCCM wilaya ya Rorya Siri Makanaki

Katibu huyo wa UVCCM wilaya amekaimu pia ofisi ya CCM wilaya ya Rorya kutokana na Katibu wa CCM wilaya hiyo Loth Hilemeirut ni mgonjwa na yupo nje ya ofisi kwa matibabu .

Katika barua hiyo ilielezwa kuwa kikao cha baraza la vijana la wilaya kilichoketi tarehe 23, 12, 2023 katika ofisi ya CCM wilaya, pamoja na mambo mengine ya uhai wa jumuiya, kikao hicho kiliweza kupitia tabia na mienendo ya Onjiro kama kiongozi wa ngazi ya juu.

Mienendo hiyo ikiwemo ya utapeli na ubadhilifu wa mali za watu kwa nyakati tofauti, tabia ambayo ilipelekea kikao cha baraza kumuondoa kwa kura 101 kati ya kura 108 za wajumbe waliohudhulia kikao hicho.

Hata hivyo January, 24, 2024, Katibu Hamasa wilaya hiyo ya Rorya, Emmanuel Paulo Onjiro aliyeondolewa madaraka ya nafasi hiyo ya uongozi alikata rufaa kwenda ofisi ya umoja wa vijana mkoa wa Mara akipinga kuhusika na utapeli na ubadhilifu wa mali za watu.
      Emmanuel Paulo Onjiro aliyeondolewa ukatibu hamasa na Chipukizi wilaya ya Rorya

Onjiro anakana tuhuma hizo na  kusema kuwa, kuondolewa kwake ni njama zilizopangwa na katibu wa UVCCM wilaya hiyo ambaye aliwashawishi wajumbe wamuondoe baada ya kusambaza uongo wa yeye kufanya utapeli na ubadhilifu wa mali, na kwamba kikao kilitawaliwa na vurugu kuhusu kuondolewa madarakani.

Vijana wa UVCCM wafunguka

DIMA Online imezungumza na Viongozi wa Chama na wa UVCCM wakiwemo wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya Jumuiya hiyo wilaya, viongozi wa Kata, Matawi, wakiwemo wenyeviti, makatibu, wakufunzi, vijana wa hamasa na Itifaki pamoja na Katibu Hamasa na Chipukizi mkoa wa Mara ili kufahamu wanachokijua juu ya kuondolewa katibu hamasa.

Baadhi yao wamezungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao wala kata watokako. Hivyo chombo hiki cha habari hakitawataja majina wala kata watokako isipokuwa tu kwa wale waliokuwa tayari kutajwa majina yao.

Kiongozi mmoja katika jumuiya ya UVCCM kutoka Kata ya Koryo anasema "Katibu wetu Makanaki hapendi mtu ambaye anakuwa mshauri wake mzuri wa mambo mema. Yeye ndiye alishawishi wajumbe kutoka kata mbalimbali ambao ni wajumbe wa baraza la wilaya kumkataa Onjiro, ndiye aliyetengeneza njia ambayo ilipelekea Onjiro kutolewa katika nafasi yeke ya uongozi" anasema kiongozi wa UVCCM.

Anaongeza " Taratibu za kumkataa hazikufuatwa maana lazima kuwepo na nakala au barua mbalimbali ambazo zilishatolewa katika hatua za mwanzo katika kumshitaki mtu au kumpa mtu onyo.

Kijana mwingine wa UVCCM katika kata hiyo anasema " Makanaki amevunja utaratibu wa kuendesha vikao anafanya kwa matakwa yake. Utaratibu ulioendeshwa wa kikao haukuwa sahihi maana ajenda hazikuorodheshwa moja baada ya nyingine bali Makanaki alikuwa anaongea kile anachokifikilia yeye  kutoka kichwani mwake " anasema.

Kiongozi mmoja wa UVCCM kutoka Kata ya Mirare anasema " Makanaki amekuwa na kauli akiisema kuwa yeye ni alfa na omega hakuna mtu anayeweza kufika kwa baba bila kupitia kwake. Kauli hii inatukera sana maana anatumia cheo chake kukandamiza walio chini yake.

" Suala la Onjiro kuondolewa kwenye nafasi yake lilitokana na urafiki wao kuvunjika pale ilipotokea Onjiro kafanya jambo ambalo hakumshirikisha. Hali hiyo imesababisha Makanaki kufanya maamuzi yasiyo sahihi kwa kushawishi wajumbe kwenda kupiga kura ya ndio kwaajili ya kumwondoa.

Kiongozi wa UVCCM kutoka kata ya Nyambori anasema Onjiro hajawahi kulalamikiwa kwenye baraza, yalikuwa ndio malalamiko ya kwanza na kwamba alipaswa kushauriwa na kuonywa na sio kuondolewa nafasi ya uongozi.

"Katibu wetu Makanaki ana fitina za hajabu na mambo yasiyo mazuri akishakuwa na fitina na wewe atatafuta figisu za kukuchomekea ili utolewe sehemu husika. Sisi vijana tunatamani tupige kazi lakini kuna mambo madogomadogo yanatukwamisha.

"Waandishi wa habari tusaidieni kutupazia sauti ili viongozi wetu wa CCM ngazi za juu wasikie watusaidie ili Jumuiya yetu ya Rorya vijana wasitawanyike. Ni kweli Onjiro alifanya baadhi ya makosa ya kiutapeli lakini tulitoa ushauri kwenye baraza kuwa kwakuwa ni kosa la kwanza aonywe lakini Makanaki akaenda moja kwa moja kushauri aondolewe" anasema.

Kiongozi wa UVCCM ngazi ya kata anasema " Kulingana na makosa ya Onjiro kama yalivyoelezwa kwenye baraza kuwa kamtapeli mtu bado njia iliyotumika kumtoa haikuwa sahihi, Makanaki alishauri wajumbe wapige kura ya kumtoa ukatibu hamasa. 

"Kanuni ya UVCCM inasema mtu akifanya kosa la kwanza lazima aonywe kwa barua na kabla ya kujadiliwa kwenye Baraza la vijana ilipaswa swala lake lijadiliwe kwanza kwenye kamati ya utekelezaji kisha liende baraza.

" Lakini haikufanyika hivyo, mjumbe mmoja aliibua hoja kwenye baraza kisha kura zikapigwa za kumkataa ambazo hatukutamkiwa ni ngapi zilizosema ndiyo au hapana na hatukuoneshwa barua za onyo alizowahi kupewa zaidi ya kuambiwa makosa yake kwa mdomo.

Kiongozi wa UVCCM kutoka Kata ya Rabuor anasema Baraza liliendeshwa kidikteta na ubinafsi. " Katibu wa UVCCM wilaya ni kama hajasomea uongozi tunaomba chama Taifa kimuondoe watuletee mwingine, istoshe sio kijana ni mkubwa kiumri na amekaa miaka mingi hapa Rorya tumemchoka.

" Istoshe tukiwa na shughuli za sherehe analazimisha ili afike kwenye shughuli yenu mpaka mkodi muziki wake. Tulimwalika kuja kwenye uzinduzi wa kutundika bendera akasema ili aje kwenye sherehe yetu tuchukue muziki wake tukakubali kukodi tukamlipa laki mbili lakini cha kusikitisha hakufika kwenye uzinduzi" anasema.

Kiongozi wa UVCCM kutoka kata ya Nyahongo anasema " Sababu za kumuondoa Onjiro kwenye ukatibu zilitajwa kwenye baraza na akapewa muda kujieleza lakini alishindwa kujitetea. Hoja ile ilikuwa ya dharura haikuwa ya Katibu Makanaki ilitolewa na wajumbe na alishawahi kupewa barua za onyo kutokana na utapeli wake." anasema.

DIMA Online imezungumza na viongozi wa CCM na UVCCM Kata ya Kirogo anakotoka Onjiro aliyeondolewa uongozi kwa tuhuma za utapeli na ubadhilifu wa mali ili kufahama kama amewahi kushtakiwa na jamii au wanachama katika kata hiyo kwa utapeli au ubadhilifu wa mali.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Kirogo Ronald Ernest anasema ofisi haijawahi kupata malalamiko ya Onjiro kujihusisha na utapeli au ubadhilifu na hawajawahi kupata barua yoyote kutoka wilayani ikimtuhumu kuhusika kwa vitendo vya utapeli.

"Hatujui amesimamishwa kwa tuhuma gani maana hatuna barua inayoeleza kuwa aliwahi kuhusika na utapeli sisi tunasikia ameondolewa uongozi ila hatujui sababu za yeye kuondolewa maana hatuna nyaraka yoyote ya barua iliyotufikia kama kata au Tawi anakotoka Onjiro, pia sisi Chama hatuingilii majukumu ya Jumuiya ya vijana " anasema.

Katibu Mwenezi CCM Kata ya Kirogo Jackson Odada anasema " Sisi kama jamii ya Kirogo sijasikia kuwa amewahi kufanya utapeli au kuchukua mali ya mtu yeyote wala kusikia kuwa ana tabia ya udokozi. Unajua haya mambo kama unamtuhumu mtu unatakiwa kuleta ushahidi wenye nyaraka uliotoka serikali ya kijiji, mtaa, Polisi au Chama kuwa umedhulumiwa na mtu fulani.

"Sisi kwenye Chama hatuna tatizo na Onjiro kama kuna figisu wanajuana wenyewe na katibu Makanaki. Mimi Mwenyewe nimesimamishwa na wilaya tangu mwaka jana eti tunamnadi mtia nia mwingine wa ubunge mara nimemtukana Mwenyekiti wa chama wilaya" anasema Odada.

Katibu wa UVCCM kata ya Kirogo Edward Oyombe anasema " CV ya ndani ya mtu ni vigumu kuijua, kwenye ofisi yangu sijawahi kupokea malalamiko yoyote. Istoshe kwenye lile Baraza kulikuwa na kelele nyingi mvutano.

"Unajua kwenye kura wanaweza kupiga watu watatu kutokana na baadhi kuegemea upande wa mtu fulani ikaonekana ukumbi mzima umepiga kura kumbe siyo. 

"Kura zilipigwa kwa kunyoosha mkono hazikupigwa kwa kuandika kwenye karatasi zilikuwa za kusema kwa mdomo, hata kwenye upigaji kura kulikuwa na mvutano na kura za ndio au hapana hazikutamkwa hadharani mbele ya wajumbe." anasema.

Anaongeza " Hata hizo taarifa za utapeli ni za kutengeneza hazikuwa rasmi kwasababu huyo Nyasembo wanaedai katapeliwa kwenye kikao cha baraza hakuwepo ili atueleze alivyotapeliwa na swala la shamba lisingejadiliwa kwenye baraza ni swala binafsi.

"Nyasembo alipaswa kuitwa kwenye kikao atoe uthibitisho kwamba katapeliwa vipi, huwezi kutoa fedha ya shamba kabla hujaona eneo likoje, mbona Nyasembo alikuja na gari akabeba magunia ya mahindi zaidi ya 10 sasa sijui huo utapeli ulikuwa ni wa aina gani!" anasema.

Kamati ya utekelezaji haikumjadili 

Kuhusu Baraza kumwondoa uongozi Onjiro pasipo kujadiliwa kwanza kwenye vikao vya kamati ya utekelezaji ya jumuiya ya UVCCM wilaya hiyo baadhi ya wajumbe wana haya ya kusema;

Mjumbe mmoja wa kamati ya utekelezaji anasema " Kesi ya Onjiro ilikuwa lazima iende kwenye Baraza kwasababu yeye alikuwa anatumikia baraza siyo wajumbe wa kamati.

" Baada ya wajumbe kumkataa ndio likaenda kwenye kamati kwa ajili ya kumteua katibu mwingine wa muda. Baraza limeshaamua kamati ya utekelezaji haina nguvu ya kumrudisha " anasema.

Mjumbe mwingine wa kamati ya utekelezaji anasema " Hatujawahi kukaa kwenye kamati ya utekelezaji kumjadili Onjiro, suala lake lilipelekwa harakaharaka sana bila hata sisi kamati ya utekelezaji kukaa kulijadili.

Anaongeza kuwa baraza lilifanya makosa kutoa maamuzi ambayo malalamiko yalitolewa na mjumbe mmoja tu ambaye hakuonesha ushahidi wa maandishi ya utapeli aliofanya Onjiro bali alikuwa anaongea tu kwa mdomo.

" Hatukukaa kikao chochote hata kama kafanya makosa kuna taratibu za vikao vilipaswa kukaa kujadiliana badala yake mjumbe mmoja aliibuka kwenye baraza akamtuhumu kisha maamuzi yakatolewa kumuondoa. Zile ni tuhuma nzito zilihitaji kupata muda kwanza zichunguzwe baada ya hapo ndio baraza lingetoa maamuzi" anasema.

Anaongeza "Kinachotutenganisha vijana ni baada ya jambo hilo kutolewa maamuzi na kiongozi wa UVCCM wilaya ambapo alipaswa kwanza yeye na viongozi wa chama wilaya walijadili lakini lilipoibuliwa na mtu mmoja kwenye baraza katibu UVCCM akalivalia njuga utadhani walilipanga na hivyo kumuondoa uongozi" anasema.

Baadhi hawakuwa wajumbe halali

Kiongozi mwingine wa UVCCM anasema " Katika kanunu ya UVCCM kuna namna ya kumtoa katibu hamasa akiwa ameenda kinyume na taratibu za chama au jumuiya lakini katika kipengele hicho Baraza lililoketi na kumjadili Onjiro kuna baadhi ya vijana walishiriki baraza  ambao hawakuwa wajumbe halali wa baraza.

" Mary Mbogo ni PS CCM wilaya alishiriki baraza la vijana na sio mjumbe, katibu UVCCM kata ya Kyangasaga sio mjumbe, hamna kanuni zinazowaingiza kwenye baraza la wilaya. Kuna jina lilionekana kwenye mahudhulio la Joshua S. Peter kuwa ameshiriki baraza wakati hakushiriki kwenye baraza. Kuhusu idadi ya wajumbe walioshiriki baraza yenyewe ilikidhi idadi" anasema.

"Sijaona kwenye kanuni kuna mahali panasema asiyekuwa mjumbe halali wa baraza anaweza kukaimu kuandika mhitasari wa kikao cha baraza nachofahamu anayetakiwa kukaimu awe ni miongoni wajumbe wa baraza. 

Anaongeza kusema " Nikweli Onjiro alifanya baadhi ya makosa lakini taratibu za kumuondoa hazikufuatwa, alishtumiwa kwa ubadhilifu wa fedha kati yake na rafiki yake aliyempatia pesa za kulima shamba lakini hakuzitumia ipasavyo. Rafiki yake akapeleka malalamiko kwenye chama na Makanaki akalileta kwenye Baraza na maamuzi yakatolewa ya kuondolewa.

"Hakuitwa kujadiliwa kwenye kamati ya utekelezaji ya UVCCM wilaya pale ndio wangemwita wamjadili wakiona maelezo yake hayaridhishi basi wanachukua maamuzi na kuwasilisha kwenye baraza ili wajumbe wajadili na kutoa maamuzi.

Kiongozi wa UVCCM kutoka kata ya Nyamagaro anasema " UVCCM ina vikao vitatu, kamati ya utekelezaji, baraza, mkutano mkuu. Baraza haliwezi kukaa bila kamati ya utekelezaji kukaa huyo anayesema kamati haikukaa ni muongo kamati ilikaa.

"Wanasema aliyeandika mhitasari wa kikao sio mjumbe ni kweli lakini katibu UVCCM wilaya anaweza kuwa na shida ambazo hazihepukiki au hali ya kiafya sio nzuri kumwezesha kuandika mhitasari, anauwezo wa kuchukau mtu mwingine kumwandikia.

"Katibu wa CCM Kyangasaga ana uzoefu na kazi, aliwahi kuwa kiongozi wa UVCCM kata . Katibu aliona amchukue ili aweze kuandika tu sio kuongeza wala kupunguza yeye ni kuandika yaliyozungumzwa na kujadiliwa kwenye baraza sasa hapo kuna tatizo gani?" anahoji.

"Wanasema kura hazikupigwa, si kweli kura zilipigwa zikahesabiwa na zikatangazwa kama hazikutangazwa sisi tulijuaje kuwa wajumbe waliopiga kura ni 108 ?. Kilichomwondoa Onjiro ni kutumia cheo chake kujipatia kipato malalamiko yalienda ofisini na mengine tulijionea wenyewe, fedha zinachangwa na viongozi Onjiro anachukuwa badala ya kugawia vijana" anasema.

Wakizungumzia kadi ya chipukizi inayodaiwa kuuzwa na Onjiro Tsh. 50,000 iliyopelekea kuondolewa nafasi yake ya katibu hamasa, baadhi ya wajumbe wa baraza wanasema hakuna uthibitisho kama iliuzwa kwa gharama hizo.

Mjumbe mmoja wa Baraza la vijana anasema " Eti wanasema Onjiro alimtapeli rafiki yake aitwaye Samson maarufu Nyasembo kuwa alimuuzia kadi sh. 50,000, huyu Nyasembo alipaswa kuleta malalamiko ile siku kabla ya uchaguzi wa chipukizi ambapo kwenye uchaguzi mtoto wake alishinda na kuwa mjumbe wa kamati ya uendeshaji chipukizi mkoa" anasema.

Mjumbe mwingine anasema " Huyo Nyasembo alipaswa kuhoji gharama za kadi siku ya uchaguzi wa Chipukizi  maana alikuja ofisini angemuuliza Makanaki mbona nimeuziwa kadi ya mwanangu kwa sh.50,000? ili Onjiro aitwe ajibu, lakini hakusema chochote, tumelisikia likiibuliwa na mjumbe mmoja kwenye baraza la vijana.

" Ishu ya Onjiro kuondolewa ilipangwa na Makanaki na timu yake na huyo aliyependekezwa kuwa katibu hamasa ndio alitoa hoja ya kuondolewa ambaye ni Meneja wa  Bar ya Nyasembo iliyoko kata ya Ikoma aliyedai kwenye kikao kuwa kamtapeli fedha Nyasembo" anasema.

Wapinga jina lililopendekezwa

Inaelezwa kuwa baada ya Onjiro kuondolewa kwenye uongozi, mwezi Januari mwaka huu, Katibu wa UVCCM wilaya ya Rorya, Siri Makanaki aliketi kikao na wajumbe wa kamati ya utekelezaji wa UVCCM na kupendekeza jina la katibu wa UVCCM kata ya Ikoma Alphaxad Mwizarubi kuwa katibu mpya wa hamasa wilaya.

Baadhi ya wajumbe wanapinga kuwa kikao hicho cha kamati ya utekelezaji hakikuwa halali kwakuwa baadhi ya watu walioshiriki kikao hawakuwa wajumbe halali wa kamati ya utekelezaji.

Mjumbe mmoja aliyehudhuria kikao cha kamati ya utekelezaji kilichopendekeza jina la katibu mpya wa hamasa wilaya litakalothibitishwa na wajumbe wa baraza anakili baadhi ya walioshiriki kikao hawakuwa wajumbe  halali.

"Wajumbe waliokaa kwenye kikao kupendekeza jina la katibu hamasa wilaya baadhi yao sio wajumbe halali. Makanaki aliita wajumbe wasio halali ambao ni rafiki zake waliolazimisha Onjiro atolewe uongozi. Katika kikao hicho Mwenyekiti wa kikao alikuwa huyohuyo katibu UVCCM wilaya ya Rorya na Katibu wa kikao alikuwa Makanaki.

" Mwenyekiti wa UVCCM kata ya Nyamagaro alishiriki kikao ambaye sio mjumbe. Mkuu wa mafunzo wa UVCCM kata ya Koryo alishiriki kikao ambaye sio mjumbe, hamna kanuni zinazowaingiza kwenye kamati ya utekelezaji.

" Aliyependekezwa kuwa katibu hamasa mpya wa wilaya ndiye aliyeibua hoja ya kumtuhumu aliyekuwa katibu hamasa wilaya Emmanuel Onjiro kuwa amefanya utapeli, hivyo huwenda alimtuhumu ili aondolewe na yeye ashike nafasi hiyo " anasema.

Katibu wa Hamasa na Chipukizi Kata ya Ikoma Alphaxad Mwizarubi ambaye jina lake limependekezwa kwenye kikao cha kamati ya utekelezaji kwa ajili ya kuthibitishwa na Baraza kuwa Katibu Hamasa na Chipukizi wilaya ya Rorya ambaye kwa sasa amekaimishwa nafasi hiyo hadi pale atakapothibitishwa anasema;

" Mimi sikuwa kwenye hicho kikao cha kamati ya utekelezaji kilichokuwa kinapendekeza jina la atakayekuwa katibu hamasa wilaya. Nilitumiwa ujumbe wa sms na katibu UVCCM wilaya kuwa jina langu limependekezwa kuwa katibu hamasa wilaya na akanikaimisha nafasi hiyo. Kwahiyo mimi ni kaimu tu bado sijathibitishwa" anasema Alphaxad.

Dhuruma ya posho kwa vijana

Baadhi ya vijana wa UVCCM wanasema wamekuwa wakinyimwa posho wanapokuwa katika ziara za viongozi licha ya baadhi ya viongozi kutoa fedha kama zawadi kuwalipa vijana wanaokuwa katika ziara na mikutano ya viongozi wa chama, serikali na mwenge.

Kijana wa UVCCM kutoka kata ya Bukwe anasema   " Katibu Makanaki amekuwa akiwadhurumu vijana fedha wanazopewa za pongezi zinazotolewa na viongozi kwenye ziara mbalimbali hususani kwenye mbio za mwenge na ziara za kichama za viongozi wa kitaifa.

" Kumekuwa na tabia vijana kutelekezwa kwenye maeneo ya mikutano. Mfano siku alipokuja Makonda aliyekuwa katibu Mwenezi Taifa tuliambiwa tumsindikize hadi Tarime.

" Tukabebwa na basi la Zakaria kutoka Utegi hadi Tarime likaturudisha hadi Utegi lakini baadhi hatukulipwa nauli kurudi majumbani kwetu wachache wakalipwa sh 10,000 wengine 5,000, vijana tunatumiwa kama daraja la watu wengine kuvuka.

Kijana mwingine anasema " Makanaki amekuwa akitumia nafasi yake kudhulumu vijana fedha wanazopewa kama zawadi na anagombanisha vijana kwa maslahi yake mnaweza kuongea jambo akalibadilisha, akawachonganisha na kuleta migogoro kwenye jumuiya.

Akizungumzia suala la Jumuiya kuyumba, kiongozi mmoja wa UVCCM kata ya Kitembe anasema " Suala la ukuaji wa Jumuiya halitegemei mtu mmoja ni jumuishi kwa viongozi wetu wote ngazi za juu na chini. Huko nyuma kulikuwa kukifanyika matamasha ambayo yaliwahamasisha sana vijana lakini kwa sasa hayapo, matamasha yalikuwa sehemu ya kuzalisha vijana" anasema.

Mwandishi wa makala hii akamtafuta kwa njia ya simu Samsoni Mkurunzi maarufu Nyasembo ili kufahamu tuhuma hizo zina ukweli gani baada ya baadhi ya wajumbe katika kikao cha baraza kumtuhumu Onjiro kumtapeli fedha.

Hata hivyo simu yake haikuwa hewani ambapo ilidaiwa yupo safarini nchini Kenya, na alipotafutwa kupitia whatsApp kwa namba yake ya nchi ya Kenya kueleza sakata hilo hakuweza kusema chochote.

Katibu UVCCM Wilaya azungumza

Katibu wa UVCCM wilaya hiyo Siri Makanaki amepinga vikali kuhusika na tuhuma hizo zilizoelekezwa kwake na kusema kuwa hana chuki na Onjiro bali kuondolewa kwake kulitokana na hoja za wajumbe waliomtuhumu kuhusika na utapeli likiwemo la kuuza kadi ya chipukizi sh. 50,000.

Anasema sio yeye aliyemuondoa madaraka bali ni baraza hivyo yeye kama kiongozi wa wilaya hana pingamizi lolote na maamuzi ya kikao cha baraza kwakuwa waliomuondoa ni wajumbe wa Baraza na kwamba hakuna dhuluma ya posho kwa vijana.

Katibu Hamasa mkoa wa Mara 

Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM mkoa wa Mara, Leonard Otuoma anakili kufahamu kuondolewa uongozi kwa Katibu Hamasa na Chipukizi wilaya ya Rorya, alipata nakala ya barua ya Emmanuel Onjiro ya kukata rufaa na kwamba jambo hilo limeshafika ofisi ya mkoa kwa ajili ya kutatuliwa.

Alipoulizwa kama ana taarifa ya kupendekezwa jina la Katibu Hamasa mpya Alphaxad Mwizarubi katika kamati ya utekelezaji ya wilaya ambaye ni Katibu Hamasa kata ya Ikoma, baada ya Onjiro kuondolewa na Baraza la Vijana na kwa sasa ndiye anakaimu nafasi ya katibu hamasa wilaya anasema;

" Sina taarifa ya kupendekezwa Katibu Hamasa mwingine wilaya ya Rorya, hatuna kanuni inayosema katibu hamasa atateuliwa kwa muda , kanuni inasema katibu hamasa atapendekezwa na Mwenyekiti atajadiliwa kwenye kamati ya utekelezaji na kuthibitishwa na Baraza.

" Kwahiyo kama yupo katibu hamasa ambaye hajathibitishwa na baraza huyo sio katibu hamasa na mimi sijapata taarifa rasmi za katibu hamasa mpya, sisi tunamjua katibu hamasa aliyekuwepo bado yupo " anasema Otuoma.



No comments