HEADER AD

HEADER AD

BARABARA YA IGOMBE – KAHAMA INAVYOWATESA WANANCHI


>>Wabeba mabegani majeneza yenye miili kwa sababu ya ubovu wa barabara

>> CCM kupata ugumu kuwanadi wagombea uchaguzi serikali za mitaa

>>Watamani barabara ijengwe kwa kiwango cha lami 

>>Meneja TARURA azungumza


Na Dinna Maningo, Mwanza

UBOVU wa Barabara ni moja ya sababu inayorudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Wananchi wanapokosa miundombinu bora ya barabara hupata kero na karaha wanaposafiri au kusafirisha bidhaa zao kwa kutumia Gari, Pikipiki , Baiskeli, Toroli na Mkokoteni .

Ubovu wa barabara kwa baadhi ya maeneo unawakwamisha wananchi kuyafikia malengo yao ya kimaisha, badala yake kubaki katika mateso huku mitaa na vijiji navyo vikiwa nyuma kimaendeleo kutokana na kutofikiwa na huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa sababu ya ukosefu wa barabara zenye ubora.

            Barabara mtaa wa Bujingwa ikiwa imeharibika

Ni Mwendo wa takribani kilomita 16 nilipoianza safari mimi na abiria wenzangu kutoka mjini Mwanza kwenda Igombe kata ya Bugogwa, iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, mkoani Mwanza.

Tunasafiri kwa dakika kadhaa na kufika stendi ya Igombe, nashuka na kusogea katika maegesho ya pikipiki nakuomba kupelekwa mtaa wa Bujingwa na Kilabela iliyopo katika Kata hiyo.

Nauliza gharama za kunifikisha katika mitaa hiyo. Dereva wa pikipika ananiambia nauli ni elfu tatu, namuuliza ni umbali wa km ngapi ?  ananijibu kwa kukadilia ni zaidi ya km 3. 

Anasema bei imepanda toka Tsh.1000 hadi Tsh. 3000 kutokana na ubovu wa barabara.

Napanda pikipiki na kuianza safari. Inanishangaza kuona licha ya Kata ya Bugogwa ni maarufu kwa shughuli za uvuvi na kilimo lakini baadhi ya mitaa hali ya barabara inatisha, zinapitika kwa shida.


 Mwendesha pikipiki akipita barabara ambayo ni mbovu.

Tukiwa tunaelekea mtaa wa Bujingwa nalazimika kumwambia dereva anishushe nitembee kwa miguu kuvuka sehemu korofi. Ni baada ya kutaka kudondoka.

Nalazimika kushuka na kutembea kwa miguu maeneo yenye makorongo huku nikizungumza na watumiaji wa barabara. Tukifika penye unafuu napanda pikipiki kisha tunaendelea na safari.

Ubovu wa barabara unawakera wananchi akiwemo  mkazi wa Bujingwa Eva Misalaba,‘’ Barabara ni mbovu imejaa makorongo tunapishana na pikipiki kwa tabu. Watoto wanapita kwa hofu kwenda shuleni.

"Hakuna karavati, msimu wa mvua maji yanajaa wanafunzi hawaendi shuleni’’ anasema Eva.

Wananchi wakipita barabara ambayo imekuwa kero.

Revocatus Malendeka anasema ‘’ Usafiri wa pikipiki ulikuwa Tsh. 1,000 kwenda Bujingwa saizi ni Tsh.  2,000 hadi Tsh.3,000 na ukiwa na mgonjwa nyakati za usiku nauli si chini ya Tsh.10,000 kwenda kituo cha afya Karume’’ anasema Revocatus.

Nafika mtaa wa Bujingwa kisha nasogea hadi ilipo ofisi ya serikali ya mtaa wa Bujingwa, kwa bahati nzuri namkuta Mwenyekiti wa mtaa huo, Shija Habari na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Bujingwa Shaban Nkungu tunasalimiana na kuzungumza.

Ubovu wa barabara ni changamoto kwa wagonjwa wanaosafiri kwenda kupata huduma ya afya. Hali hiyo inasababisha wananchi kuwalaumu viongozi wa serikali za mitaa kuwa wamewachagua lakini wameshindwa kutatua kero zao.

Fares Huzunya ni mjumbe wa Serikali ya mtaa wa Kilabela anakerwa na ubovu wa barabara ‘’Ukienda hospitali ni shida pikipiki  zinapita kwa shida wagonjwa wanahangaika.

Tukiitisha mikutano wananchi               wanatulaumu viongozi, tunaonekana sisi sio watetezi wao. Wakati mwingine tunakuwa waoga wa kuitisha mikutano maana utawaambia nini wakati wanaona changamoto walizozipigia kelele hazitatuliwi  " anasema Fares.

Wananchi wabeba mabegani majeneza yenye miili

Kero ya barabara inaelezwa kujadiliwa kwenye vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Kata ( WDC ) lakini bado hakuna utatuzi, huku wananchi wa mtaa wa Bujingwa wakilazimika kubeba mabegani majeneza yenye miili kituo cha afya Karume kilichopo mtaa wa Bugogwa kupeleka nyumbani kwaajili ya maziko.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Bujingwa, Shija Habari anasema barabara ni mbovu ina makorongo. Wananchi wanapita kwa shida na kwamba, tangu iharibike kusafirisha marehemu ni shida gari hazipiti. 


           Mwenyekiti wa mtaa wa Bujingwa Shija Habari, akionesha eneo la barabara ya Igombe- Kahama ambalo limekuwa kero kwakuwa hakuna karavati, wakati wa mvua maji hujaa na kusababisha adha kwa wapitaji na wanafunzi kushindwa kuvuka kwenda shuleni.


"Mgonjwa akifariki watu wanalazimika kutembea kwa miguu wakiwa wamebeba mabegani marehemu akiwa ndani ya jeneza.
 

Mwili hubebwa kwa gari au Bajaji kutoka mochari kituo cha Afya Karume" anasema Shija.

Anaongeza kusema " Wananchi wakifika mtaa wa Kigote, bajaji haiendelei na safari kwenda mtaa wa Bujingwa. Mwili unashushwa chini wananchi wanabeba jeneza mabegani hadi nyumbani kisha makabulini.

'' Tangu mwezi wa nne mwaka huu hadi sasa tulipata misiba minne ambayo tulisafirisha majeneza yenye miili kwa kubeba mabegani mwendo wa takribani km 3.’’anasema Mwenyekiti.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kilabela John Mang'ombe anasema '' Gari hazipiti, mgonjwa akiugua kusafirishwa ni mateso. Pia usafirishaji wa vifaa vya ujenzi, mazao toka mashambani na mahitaji mengine kutoka na kwenda Igombe ni shida

Tunaomba Serikali hijitahidi kuboresha miundombinu. "Serikali itekeleze miradi kwa wakati maana uchaguzi uliopita Chama kilitunadi tukaahidi kutatua changamoto kwenye mitaa ambazo baadhi hazijatatuliwa '' anasema John.

 Wataka barabara ya Lami kurahisisha maendeleo

Baadhi ya wananchi akiwemo Shija Tarima wanaiomba Serikali kujega barabara ya Igombe- Kahama kwa kiwango cha lami kutokana na kwamba matengenezo ya mara kwa mara katika barabara hiyo yanaigharimu serikali pesa nyingi.

       Mwananchi akieleza kero ya barabara ya Igombe- Kahama

" Hii barabara inaenda hadi makao makuu ya wilaya ya Ilemela, ikijengwa kwa ubora itawapunguzia wananchi mwendo, muda  na gharama za nauli kuzunguka kupita Sabasaba.

" Sisi wakazi wa kata ya Bugogwa ili uende wilayani unalazimika kupanda gari nauli Tsh. 1,000, ushukie Sabasaba ulipe tena nauli gari za kwenda Buswelu wilayani Tsh.600 jumla kwenda na kurudi ni  Tsh 3,200, unatumia muda mwingi kwenda wilayani " anasema Shija.

Salome Cleophace anaongeza " Barabara ya Igombe - Kahama kuelekea wilayani ikijengwa kwa ubora na kuwekwa lami itatupunguza mwendo na gharama za usafiri.


Salome Cleophace mkazi wa Bujingwa 

"Ukipita barabara hiyo ya Igombe-   Kahama inayofika hadi zilipo ofisi za wilaya ya Ilemela unapita mtaa wa          Bugogwa, Igombe B, KigoteBujingwa, Kilabela, Igogwe, Ilalila, Kahama kisha  Buswelyalipo makao makuu ya wilaya ya Ilemela.

" Barabara hiyo ikijengwa kwa kiwango cha lami, nauli kwa usafiri wa haice inaweza kuwa kati ya Tsh. 800- 1,000,  Bajaji Tsh. 1,000, Pikipiki Tsh. 3,000                            anasema.

Anaongeza " Serikali itutendee haki. Kata yetu inaipa serikali mapato mengi yakiwemo yatokanayo na shughuli za uvuvi lakini wavuvi wanateseka kusafirisha mazao yao.

" Mwandishi Tunaomba utusaidie waulize TARURA  kwanini hawakarabati barabara kwa wakati na ni lini barabara itajengwa kwa kiwango cha lami ? " anauliza .

CCM kupata wakati mgumu kuwanadi wagombea

Wakati wa kampeni za uchaguzi vyama vya siasa hujinadi mbele ya wananchi katika mikutano ya hadhara, ambapo hutoa ahadi kwa wananchi kuwa endapo wakiwachagua watahakikisha katika uongozi wao kunakuwa na maendeleo katika maeneo wanayoyaongoza.

Baadhi ya ahadi ni pamoja na kuhakikisha serikali inafanymaendeleo ikiwemo huduma za jamii kama vile ujenzi wa barabara bora, maji , umeme , ujenzi wa vituo vya afya na shule.

Ubovu wa Barabara kuanzia Igombe hadi Igogwe huenda ukakitesa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kuwanadi wagombea uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba, 27 , mwaka huu kwakuwa kero ya ubovu wa barabara imekuwa mwiba kwa wananchi.

Shaban Nkungu ni Mwenyekiti wa CCM Tawi la Bujingwa anaeleza ubovu wa barabara utakavyowapa ugumu kuwanadi wagombea endapo Serikali haitatengeneza barabara.


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Bujingwa, Shaban Nkungu akionesha ubovu wa barabara

" Ubovu wa hii barabara utatukwamisha kisiasa, tutakapowanadi wagombea wananchi hawatatuelewa. Tuliahidiwa tangu mwezi wa saba kuwa zimetengwa Milioni 47 kutengeneza barabara lakini hadi sasa hatujaona hata greda likilima barabara na hakuna maelekezo yoyote.

" Kata ya Bugogwa ni miongoni mwa kata zinazoongoza kuwa na mitaa mingi ipatayo 15. Mitaa yenye changamoto ya ubovu wa barabara hiyo ni pamoja na Igombe B, Kigote, Bujingwa, Kilabela na Igogwe, ukiwa unaelekea wilayani " anasema.

Anaongeza " Watu wanatamani wavutiwe maji majumbani lakini vifaa  kwa maana ya miundombinu ya maji itafikaje kwenye mitaa wakati barabara ni mbovu!. 

TARURA yatenga fedha za matengenezo

Nafunga safari hadi ofisi ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Ilemela iliyopo kata ya Buswelu kuzungumza na Meneja wa TARURA. 

Naelezwa kuwa hayupo ofisini kwamba amekaimu ofisi ya TARURA mkoa wa Mwanza.

Nafika hadi mtaa wa Kapripoint iliko ofisi ya TARURA mkoa. Naingia mapokezi, naomba kuonana na Meneja TARURA wilaya ya Ilemela Mhandisi Sobe Makonyo aliyekuwa amekaimu ofisi ya TARURA mkoa wa Mwanza.

Punde si punde bila kuchelewa naruhusiwa kuinga ndani kuonana naye.

Tunasalimiana kisha tunazungumza na kueleza changamoto ya barabara inayowapa kero na karaha watumiaji wa barabara.

Bila hiana anaeleza mpango wa ukarabati wa barabara ya Igombe- Kahama.

Mhandisi Sobe anasema barabara hiyo ya Igombe – Kahama ni ya urefu wa km 9.2 na kwamba Serikali kupitia TARURA imeitengea fedha za matengenezo kiasi cha Tsh. Milioni 25 . 
 

Meneja TARURA wilaya ya Ilemela Mhandisi Sobe Makonyo.

"Hiyo Barabara ipo kwenye bajeti ya fedha ya 2024/2025, ipo kwenye mpango wa matengenezo imetengewa Tsh. Milioni 25 kwa kiwango cha              changarawe. Kazi kubwa zitakazofanyika ni kukarabati, kuweka karavati tano, mitaro mita 300 hasa sehemu korofi ili ziendelee kupitika.

Aeleza manufaa ya barabara

Anasema barabara ikifanyiwa matengenezo itarahisisha wanafunzi kwenda shuleni bila kupata adha , itavutia watu kuwekeza kandokando ya Kahama na Igombe na itachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

" Kazi ipo katika hatua ya manunuzi itakapokamilika kazi ya matengenezo itaanza mara moja. Barabara hiyo ni muhimu itawarahisishia wavuvi wa Igombe kufikisha mazao yao sokoni maana makao makuu ya wilaya yapo Buswelu hivyo itasaidia kupunguza gharama na muda kuzunguka Sabasaba.

Kuhusu ombi la wananchi kujengewa barabara kwa kiwango cha lami Mhandisi Sobe anasema kuwa ujenzi wa barabara hiyo utagharimu si chini ya Bilioni 5, hivyo pesa zikipatikana itajengwa kwa kiwango cha lami.

Kwa mujibu wa Tovuti ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoa wa Mwanza,www.ilemelamc.go.tz, inaelezwa kuwa Kata ya Bugogwa ni miongoni mwa kata 19 zinazounda halmashauri . 

Upande wa mashariki imepakana na kata ya Sangabuye , Kusini na Magharibi imepakana na kata ya Shibula, upande wa kaskazini imepakana na Ziwa Victoria.

Kata ya Bugogwa ina jumla ya mitaa 15. Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 kata ina jumla ya kaya 7,108 zenye jumla ya wakazi 38,698 kati yao wanawake ni 22,666 na wanaume ni 16,032.

        DIRA WIZARA YA UJENZI 

Kuwa na miundombinu bora na            endelevu itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

No comments