SERIKALI YA UJERUMANI YAVUTIWA NA MAVUNO PROJECT KARAGWE INAVYOWASAIDIA WANANCHI VIJIJINI
Na Daniel Limbe, Karagwe
SERIKALI ya Ujerumani imevutiwa na shirika lisilo la kiserikali la "Mavuno Project" lililopo wilayani Karagwe mkoani Kagera kutokana na jitihada kubwa za kuwawezesha wananchi waishio vijijini kujikwamua na umaskini wa kipato.
Hatua hiyo imetajwa kuwa mkombozi kwa jamii ambayo awali haikuwa na uhakika wa kipato ikilinganishwa na sasa ambapo baadhi ya wananchi wamefanikiwa kujikwamua kiuchumi, kuwa na uhakika wa chakula pamoja na kusomesha watoto wao.
Hayo
yamebainishwa na Meya wa jiji la Furth Munich nchini Ujerumani, Andreas
Horsche, baada ya kuwatembelea baadhi ya wanufaika wa miradi inayotekelezwa na
shirika la mavuno.
Mbali na kiongozi huyo pia ameambatana na wahandisi wasio na mipaka kutoka Ujerumani na Swiden pamoja na marafiki wa Afrika kutoka nchini Ujerumani.
Hata hivyo Horsche, amevutiwa pia na namna wananchi walivyonufaika na ufugaji wa mifugo mbalimbali ikiwemo kuku, mbuzi na ng'ombe ambapo kinyesi cha mifugo hiyo kinatumika kwa matumizi ya kurutubisha mazao mashambani pamoja na kuzalisha umeme utokanao na gesi asilia.
Philimon
Noel mkazi wa kijiji cha Lukole wilayani Karagwe, ameeleza namna alivyonufaika
baada ya kupata mafunzo mbalimbali kutoka shirika la Mavuno, amesema maisha
yake ya sasa ni bora ikilinganishwa na awali ambapo hata makazi yake yalikuwa
duni zaidi.
"Ukweli ninawashukuru sana watu wa shirika la mavuno kwa kunisaidia kufika hapa nilipo, maana nilianza na ufugaji wa mbuzi tatu na baada ya kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa shirika hilo nilizalisha mifugo mingi na sasa ninamiliki ng'ombe watatu wa maziwa.
"Nimefanikiwa kujenga nyumba yangu hii na nilitumia mbao kutoka miti niliyopanda mwenyewe na sasa ninasomesha watoto wangu bila wasiwasi wowote"amesema Noel.
Afisa kilimo wa shirika hilo, Happiness Benson,amesema zaidi ya wakulima 55935 vikiwemo vikundi 1865 wamenufaika na shirika la mavuno kwenye wilaya ya Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera kutokana na kupata mafunzo mbalimbali ya wataalamu wa kilimo na mazingira.
"Shirika limekuwa likiwahudumia wakulima kwa kuwapa mafunzo mbalimbali ya kilimo,uhifadhi wa chakula,ufugaji,uhifadhi wa mazingira pamoja na namna bora ya kutunza kumbukumbu ili kuwa na kilimo endelevu"amesema Happiness.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Wallence Mashanda,mbali na kulipongeza shirika hilo amesema limekuwa mkombozi kwa jamii na serikali kwa ujumla kutokana na kutekeleza miradi ambayo ilipaswa kufanywa na serikali.
"Uchumi wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe unategemea zaidi kilimo, ndiyo maana tunalishukuru shirika hili kwa kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja,wananchi wanapozalisha kwa tija inatusaidia na siye kukusanya mapato yanayokwenda kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jamii"amesema Mashanda.
"Takribani asilimia 85 ya wananchi wetu wanajishughulisha na kilimo.Changamoto iliyokuwepo awali ni wakulima kutozalisha kwa tija ambapo walikuwa wakitumia gharama kubwa ya kuandaa mashamba lakini mavuno yanakuwa kidogo sana ukilinganisha na hali ilivyo sasa" amesema.
Post a Comment