HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI WATAKA MABADILIKO DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2025-2050


Samwel Mwanga, Maswa

WANANCHI katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wana ndoto na matarajio makubwa kuhusu Tanzania ya kesho hasa katika kipindi cha Mwaka 2025 hadi 2050 ili waweze kupiga hatua ya maendeleo ya kiuchumi katika sekta mbalimbali.

Wameonyesha hali hiyo wakati wakitoa maoni yao mbalimbali  juu ya Dira ya taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025-2050 katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya (DCC) kilichofanyika Agosti 17, mwaka huu katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa.

Wamesema kuwa katika maendeleo ya kiuchumi wanatarajia kuona uchumi imara na endelevu unaoleta ajira nyingi, kupunguza umasikini na kuboresha hali ya maisha kwa watu wote.


         Baadhi ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu waliohudhuria kikao cha kutoa maoni juu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025-2050 katika Ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo.

Imeelezwa kuwa ili matamanio hayo yafikiwe ni lazima yafanyike maboresho makubwa katika Dira ya Taifa ya maendeleo “Pamoja na kuwa serikali imefanya mambo makubwa katika sekta mbalimbali lakini napenda katika dira ijayo suala la Elimu bora ni muhimu sana.

‘’ Kwa sasa miundo mbinu katika shule mbalimbali za msingi na sekondari ipo ya kutosha na elimu hutolewa bila malipo kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita  hivyo tunahitaji tuwe na mfumo wa elimu unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuendeleza ubunifu,sayansi na teknolojia,”amesema Jerry Nyabululu.

Wamesema kuwa ili wananchi waweze kufikia katika ndoto hizo ni muhimu wakawa na Afya bora  kwa huduma bora za afya zinazopatikana na vituo vyote vya kutolea huduma hiyo ambazo kila Mtanzania anaweza kuzimudu  sambamba na uboreshaji wa miundo mbinu ya afya na Vifaa tiba.


          Wadau mbalimbali wa maendeleo wilaya ya Maswa waliohudhuria kikao cha ushauri cha wilaya(DCC) juu ya kutoa maoni yao katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025-2025

Pia walieleza kuwa ni vizuri mifumo bora ya Utawala  iwe ya uwazi na isiyo na rushwa,ambayo inasikiliza wananchi na kutatua matatizo yao.

“Kwa ujumla Watanzania wanataka kuona nchi yao ikipiga hatua kubwa kuelekea kuwa taifa lenye maendeleo na ustawi kwa watu wake, hivyo hatuna budi kuimarisha suala la mifumo yetu ya utawala katika kuendesha serikali yetu sambamba na kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania wote,”amesema Josephat Membo.

Akifungua kikao hicho Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge amesema kuwa Dira ya maendeleo ni kichocheo kikubwa kwa maendeleo nchini na Rais Samia Suluhu Hassan anapotoka hadharani na kuwaruhusu wananchi kutoa maoni yao juu ya Tanzania wanayoitaka kwa miaka 25 ijayo na kudhihirisha dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha Taifa linatoka hapa lilipo na linakwenda mbele zaidi kimaendeleo.


Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge akiwaongoza wananchi wa wilaya hiyo kutoa maoni yao juu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025-2050.

“Tunataka kama Taifa miaka 25 ijayo tuwe mahali pazuri zaidi ya hapa na ndiyo maana tunashirikisha katika jambo hili na hatutaki hata kumuacha mtu mmoja na tunapokwenda kwenye utekelezaji tutafanya wote kwani  tumeshiriki wote katika kutengeneza Dira hii.

‘’ Hilo ndilo lengo la Rais wetu na misingi ya utawala bora ni uwazi na ushirikishwaji wa wananchi katika kufanya maamuzi ndicho hiki tunachokifanya hapa ukumbini,”amesema.

Kikao hicho kiliwashirikisha zaidi ya wadau mbalimbali 150 wa wilaya hiyo wakiwemo viongozi wa serikali,mashirika na taasisi za serikali,Sekta binafsi,Waganga wa tiba asilia,Viongozi wa vyama vya msingi vya Ushirika,Viongozi wa Vyama vya siasa, Viongozi wa madhebu mbalimbali ya dini na wananchi.

No comments