WAADVENTISTA WASABATO WAOMBWA KUWAWEZESHA KIELIMU, MAHITAJI WATU WENYE ULEMAVU
>>Waliomba kanisa kutafsiri vitabu ikiwemo lesoni kwa maandishi ya Nukta Nundu
>>Wahimiza yanapojengwa makanisa kuwepo
na miundombinu rafiki kwa walemavu
>>Wenye ulemavu walipongeza kanisa la Nyamongo Kati kuwajengea miundombinu mizuri ya vyoo
Na Dinna Maningo, Tarime
WAADVENTISTA Wasabato nchini, wameombwa kuwasomesha watu wenye ulemavu wa viungo ili wapate ujuzi wa kuwawezesha kujitegemea pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili.
Ombi
hilo limetolewa na Bhoke Orindo mwenye ulemavu wa macho ambaye ni Katibu wa
idara ya watu wenye ulemavu wa viungo katika kanisa la Nyamongo Kati, wilaya ya
Tarime, mkoani Mara wakati akihudumu huduma kuu iliyoendeshwa na watu wenye
ulemavu wa viungo iliyofanyika jumamosi ya wiki iliyopita katika kanisa hilo.
Amesema
kuwa makanisa mengi hayana miundombinu rafiki zikiwemo ngazi zinazowapa
usumbufu wakati wa kuingia ndani ya kanisa kuabudu, mimbari isiyo rafiki pamoja
na vyoo visivyo rafiki kwao huku wakilipongeza kanisa la Nyamongo kati kujenga
vyoo kwaajili ya watu wenye ulemavu.
Ameomba
watu wenye uhitaji maalum wapewe nafasi za kuhudumu katika ibada mbalimbali
ikiwemo shule ya sabato, huduma kuu, mahubiri, semina zitolewe za kuelimisha
watu kutowaficha ndani wenye ulemavu, kanisa litenge bajeti kwa ajili ya watu
wenye ulemavu ili watekeleze majukumu yao ndani ya kanisa.
“ Tuna idara ya watu wenye ulemavu wa viungo kanisani , tunaomba iwezeshwe ili kutekeleza majukumu yake, walemavu tupewe nafasi za kuhudumu ndani ya kanisa kama walivyo watu wengine .Walemavu wanashindwa kutekeleza majukumu yao ndani ya kanisa kwakuwa hawajapewa semina.
‘’
Kanisa litenge bajeti kusaidia watu
wenye ulemavu, Jimbo la Mara lianzishe makambi ya watu wenye ulemavu,watu wenye
mahitaji maalumu wasomeshwe shule na vyuo maana wengi wameshindwa kusoma
kwakuwa hawana uwezo wa kwenda shule kutokana na ulemavu walionao.
Ameyaomba
makampuni na mashirika, watu wenye uwezo wa kifedha wasaidie walemavu wa viungo
kuwapa mitaji kuwainua kiuchumi ili waachane na mambo ya ombaomba pamoja na
kuwapa ajira.
Ameongeza
kuwa watu wenye ulemavu wanapitia changamoto nyingi wengine wanatengwa na
kunyanyapaliwa na familia zao huku baadhi wakitamani kwenda kanisani kuabudu
lakini wanashindwa kwakuwa hawana watu wa kuwapeleka kanisani.
“
Wapo wanaotamani kwenda kanisani wakiwemo vipofu, viwete lakini wanashindwa
kwakuwa hakuna wa kuwatoa majumbani kwao na kuwapeleka kanisani.
Walemavu
wa mikono, vipofu wanakosa mtu wa kuwafanyia usafi, kuwafulia nguo zao, hawana magodoro
na vyandarua wanaishi maisha magumu sana “ amesema Bhoke.
Amewaomba
wazazi na jamii kwa ujumla kutowatenga walemavu na badala yake wawasaidie
mahitaji yao huku akiwapongeza wazazi wake,kaka zake na wadogo zake kwa
kutomtenga ambao wamekuwa ni tumaini na msaada katika maisha yake.
Amewatia
moyo watu wenye ulemavu kujikubali na kujisimamia na kwamba wasitumie muda
mwingi kuomboleza, kulia na kukata tamaa kutokana na hali zao na badala yake
wamsifu Mungu ndiye tumaini lao huku akisoma maandiko matakatifu ya biblia
kitabu cha Mathayo 9:1-3, Mathayo 15:30-31, Luka 4:17-18 , Mathayo 25 :35-36,
Yohana 14, 1-3.
Mwenyekiti
wa Chama cha Wasioona wilaya ya Tarime Mseti Mwita ameuomba uongozi wa jimbo kutafsiri
vitabu mbalimbali na masomo ya kujifunza biblia (Lesoni) kwa maandishi ya Nukta
Nundu ili kuwezesha wasioona kujifunza maandiko kwani masomo ya lesoni
yametafsiriwa kwa lugha ya kingereza tu ambapo wasioona wengi hawafahamu
kingereza.
Mwenyekiti
wa Chama cha wasioona mkoa wa Mara Nyamlanda Lwakatale amesisitiza wazazi na jamii kuhakikisha
watu wenye ulemavu wa viungo wanapata haki ya elimu ili iweze kuwa mkombozi wa
maisha yao.
Mwenyekiti
wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu wilaya ya Bunda, Mwl.Wilbrod
Msumange amesema kuwa yeye ni mtaalamu wa kubadili maandishi katika lugha ya
kingereza na kiswahili kuwa maandishi ya nukuta nundu na kuwaomba viongozi wa
kiadvetista Jimbo la Mara kushirikiana ili viandaliwe vitabu vya maandishi ya
Nukta Nundu.
Askofu
wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo kuu la Mara, Joseph Matongo amevutiwa
na ibada iliyoendeshwa na watu wenye ulemavu wa viungo na kusema jambo hilo ni
la kihistoria na kupongeza wote waliotoa fedha zao kufanikisha mahubiri
yanayoendeshwa na watu wenye ulemavu.
“Kwakweli
nimevutiwa na programu iliyoendeshwa na watu wenye ulemavu wa viungo,ndio mara
yangu ya kwanza kuona watu wenye ulemavu wa viungo wakiungana na kufanya
mahubiri yanayosimamiwa na wao wenyewe.
“Nampongeza
Bhoke haoni lakini amekuwa na maono ya kufanya mahubiri ya walemavu na
akatafuta wafadhili ambao wamewezesha fedha kufanikisha mahubiri. Mtu wa
kuhurumiwa duniani ni yule ana macho ya kuona ila hana maono” amesema askofu
Joseph.
Amewapongeza
wafadhili na washiriki waliotoa fedha kuunga mkono mahubiri huku akiahidi kuwa
uongozi umepokea maoni ya watu wenye ulemavu wa viungo na kuahidi kuzitatua .
Askofu
huyo amesema kuwa watashirikiana na mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya watu
wenye ulemavu ili vichapishwe vitabu vya maandishi ya Nukta Nundu Pamoja na
kuanzisha makambi ya watu wenye ulemavu jimbo la Mara.
Katibu
mkuu wa jimbo la Mara, Benjamini Ngarama amesema ni mara yake ya kwanza kuona
ibada kuu ikiendeshwa na watu wa mahitaji maalum na imemvutia huku akimpongeza
Bhoke kwa wazo lake la kuanzisha mahubiri ya watu wenye ulemavu huku Mhazini
mkuu wa Jimbo la Mara, Padon Kikiwa akiwapongeza watu wenye ulemavu kwa kuendesha
ibada nzuri iliyowavutia wengi.
Mbali
na ibada kuu iliyoendeshwa na watu wenye ulemavu pia wanaendesha mahubiri kwa
wiki tatu yaliyoanza Agasti, 4, 2024 hadi Agasti 24, mwaka huu ili kuongoa roho
ambapo mnenaji mkuu ni Mwijilisti Richard Kasagara.
Mahubiri
hayo yamefadhiliwa na Charles Mseti,
Joshua Mrimi ambao ni wakazi wa Dar es Salaam waliotoa Milioni 10 ambapo washiriki
kanisa la Nyamongo kati wamewaunga mkono kwa kuchangia Tsh. Miilioni 5.
Vilevile uongozi wa jimbo la Mara umevutiwa na mahubiri hayo nakuchangia Tsh.
500,000 kufanikisha mahubiri.
Post a Comment